MAGUFULI, Prof. TIBAIJUKA: Zigo la CCM mabegani mwenu


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Dk. John Pombe Magufuli

KATIKA kipindi chake cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakikuahidi mabadiliko makubwa.

Mgombea wa urais Jakaya Kikwete, aliahidi kuendeleza kile alichokifanya toka mwaka 2005 hadi sasa; kuboresha na kuendeleza mazuri kwa “ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.” Hicho ndicho alichoahidi wananchi.

Kutokana na kutowahidi wananchi mabadiliko makubwa, CCM imejikuta ikikataliwa na wapiga kura kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu taifa hili lipate uhuru!

Wapo wanaoweza kutoa sababu nyingine kuelezea kilichosababisha chama chao kukataliwa kiasi hiki. Lakini wakiwa wakweli watasema, “Ni kwa sababu, hatukuahidi wananchi mabadiliko.

Hata hivyo, japo hawakuahidi mabadiliko, lakini baraza la mawaziri lililotangazwa wiki iliyopita, limeashiria kelele zilizopigwa kwenye sanduku la kura zimesikika.”

Baraza la mawaziri limebeba watu ambao wanaweza ama kuizamisha CCM au kuiokoa.

Miongoni mwao, ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, Waziri Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka.

Mathias Chikawe: Anaingia akitokea Wizara ya Sheria na Katiba ambako alishindwa kutimiza kile wananchi walichotarajia.

Kazi kubwa ambayo anayo sasa tofauti na wizara ya sheria na katiba ni kusimamia Idara ya Usalama wa Taifa na masuala mengine ya utawala bora.

Katika nchi yoyote duniani, usalama wa taifa ndiyo ngao ya kwanza ya kulinda uhuru, hazina na utu wa watu wa taifa.

Ukishakuwa na idara dhaifu ya usalama wa taifa au yenye kutumika kisiasa, basi unadhoofisha kwa kiasi kikubwa uhuru na ulinzi wa taifa hilo.

Hivyo, changamoto kubwa ambayo Chikawe anayo sasa, ni kukisukuma chama chake kiandike sera mpya ya usalama wa taifa. Sijui kama wengi wanajua kuwa serikali ya CCM haina sera iliyoandikwa na kufafanuliwa juu ya usalama wa taifa.

Siyo hivyo tu, neno lenyewe “usalama wa taifa” halitokei katika Ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Mtu mwenye hekima lazima ajiulize: Idara ya Usalama wa Taifa inaongozwa na maono gani kiutendaji? Inaoongozwa na sera zipi?  Hivyo kutengeneza sera ya usalama wa taifa ni jambo kubwa kwa Chikawe.

Jambo la pili ni kurudisha heshima, hadhi na weledi kwa wafanyakazi wa idara hii. Kwa sasa maajenti wetu wa idara hii wanajulikana kirahisi na wengine wanajitambulisha kiujiko mitaani.

Emmanuel Nchimbi: Anaingia katika wizara hiyo akitokea Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Akiwa wizara hiyo hakuwa katika nafasi ya kubeba lawama nyingine.

Mengi ambayo tumegongana na Nchimbi ni kutokana na nafasi yake akiwa kiongozi wa Umoja wa Vijana (UV-CCM). Binafsi nilitarajia kuwa Nchimbi angepewa wizara hii.

Sababu kubwa ya kwanza ni kuwa ni kada mzuri wa CCM, lakini la pili ni mtu pekee ambaye anaweza kuanzisha na kuendeleza mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari huru na kuvilazimisha virudi kwenye mstari.

Ninaamini jukumu la kwanza ambalo la Nchimbi ni jinsi gani vyombo huru vya habari na waandishi watashughulikiwa.

Lakini zaidi ni vipi maoni huru yatavumiliwa. Katika miaka hii mitano iliyopita, maoni huru na vyombo huru vya habari vimekuwa vyenye kuthubutu zaidi.

Lakini kwa maoni yangu Nchimbi ataanguka kwa jinsi atakavyoshughulikia vyombo vya habari, lakini atasimama na kuingia katika historia kwa jinsi atakavyoshughulikia masuala ya vijana na michezo.

Je, Nchimbi ataanza lini kuona maandalizi ya timu ya Olimpiki ya 2012 au hadi Januari 2012? Mara nyingi, tunapofanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa tunakimbilia kulalamika kuwa “maandalizi hayakutosha.”

Niliamini kama watawala wetu wangeanza kujiandaa wakati ule kwa kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 18 basi tutakuwa na miaka 4 ya maandalizi na lengo la kupata medali 20 tungeweza kufikia kabisa.

Lakini miaka miwili imepita hakuna kiongozi hata mmoja ambaye amezungumzia hilo na katika ilani za vyama vya siasa ni CHADEMA pekee ndio walikuwa na wazo hilo la London 2012.

Sasa, Nchimbi ni lazima aoneshe kuchangamkia utaratibu wa kuanza kuandaa timu ya uhakika ya Tanzania kwenda London na kurudi na medali tukome kuwa wasindikizaji. Hivyo hivyo kwa Brazili 2014.

Dk. John Magufuli: Anaingia wizara ya ujenzi akitokea Uvuvi. Lakini anaingia wizara ambayo tayari alishawahi kuiongoza kwa hiyo haingii kama mgeni.

Naweza kusema mengi juu ya ujenzi lakini Magufuli atahukumiwa kwa mambo machache sana.

Kwanza, naamini ni suala la barabara za jiji la Dar es Salaam na miundo mbinu ya majitaka. Ninafahamu kuwa wakazi wa Dar es Salaam wamezoea mafuriko na ndiyo sababu wanawarudisha watu wale wale miaka nenda rudi.

Siwezi kuwalaumu kwani ni demokrasia hiyo. Sasa wakati umefika wa kubadilisha siyo “anga” la Dar es Salaam bali kubadilisha mitaa ya jiji. Tumeweka mkazo mkubwa wa kujenga majengo marefu na yanapendeza, lakini hatujajenga miundo mbinu inayoendana nayo.

Hatuwezi kuwa na jiji la kisasa bila barabara na mifumo ya kisasa ya maji machafu. Magufuli akifanikiwa katika hili kwa Dar es Salaam na kwa miji mingine mikubwa atakuwa amefanya mambo yaliyoshindikana miaka 49 iliyopita.

Halafu kuna suala la kampuni ya simu ya taifa (ATCL)! Hapa Dk. Harrison Mwakyembe anaweza kuwa msaada.

Profesa Anna Tibaijuka: Amejenga jina lake akiwa na historia ndefu ambayo labda wengine hawaikumbuki. Wengi wanakumbuka kuwa ametokea umoja wa mataifa – mkurugenzi wa shrika la makazi duniani (UN Habitat).

Lakini kwa wengine tunakumbuka vizuri katika harakati za kuunda Baraza la Wanawake wa Tanzania (BAWATA) ambapo alikuwa mwenyekiti wa muda wa Baraza hilo.

Haikuchukua muda serikali iliingilia kati na kuzuia baraza hilo kuanza kama ilivyokuwa inasubiriwa na wanawake wengi nchini.

Mgongano ulitokea kati ya baraza hilo, CCM, na serikali kiasi kwamba kupelekwa kwake Umoja wa Mataifa, kwa wengine ilionekana kama namna ya kumnyamazisha.

Lakini hakunyamaza kabla ya kufungua kesi ambayo yeye na wenzake waliishtaki serikali. BAWATA ilishinda kesi yake mwaka jana.

Lakini kupelekwa kwake wizara ya ardhi kulitarajiwa vile vile kwani anapokuja kutoka UN-Habitat anakuja na ujuzi na mang’amuzi yanayohusiana sana na makazi ya watu.

Ameona mengi na amejifunza mengi. Tunaweza kusema kwamba kama kuna mawaziri wanaoingia katika wizara ambazo wana “ujuzi” nazo basi ni yeye.

Kwa maneno mengine, ukiondoa uwezo wa kiutawala na kiuongozi ambao bila shaka anao anaposhika wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi anaingia katika eneo ambalo anaweza kusema kwa ukweli kabisa kuwa anajua anachozungumzia.

Hivyo, mzigo wake mkubwa ni kushughulikia jambo moja ambalo limeathirika sana na ufisadi nchini nalo ni masuala ya ardhi na hasa bei ya ardhi. Katika hili kuna suala la migogoro ya ardhi mikubwa na midogo na yapo masuala yale ambayo yameumiza familia nyingi pale wanapoamka siku moja na kukuta kiwanja chao kimeuzwa.

Yapo masuala ya ardhi za vijiji na wawekezaji wakubwa. Lakini zaidi atapimwa kwa jinsi gani analisaidia taifa kuondokana na nyumba duni na makazi ambayo imeshindikana kuondokana nayo kwa miaka hamsini iliyopita.

Ni kwa kiasi gani tutaoondokana na nyumba za udongo na tembe kwa haraka zaidi na kuwahamisha watu wetu  kuelekea makazi bora na mazingira bora ya makazi?  Hili la mwisho ndilo swali kubwa ambalo naamini Prof. Tibaijuka atahitaji kutupatia majibu.

Ninaamini kwa kuanzia tu tuangalie sana utendaji wa kundi hili katika mwanga wa mambo yote mawili yaaani kisiasa na kiserikali.

Ninaamini nafasi walizopewa zitaamua serikali inaonekana vipi kwa wananchi lakini vile vile kundi hili litaamua kabisa CCM inaonekana vipi kwa wananchi kuelekea uchaguzi wa 2015.

Ninaamini kabisa kuwa jinsi kundi hili linavyokwenda ndivyo mtazamo wa Watanzania kuhusu serikali yao utakavyokuwa.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: