Mahakama mkono wa chuma wa serikali?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KUDHARAU mahakama ni kutenda kinyume cha amri au maelekezo yake wakati ikiendesha au ikisikiliza shauri (tafsiri yangu).

Pale mtu anapodharau mahakama, hakimu au jaji anatoa adhabu kwa mhusika kwa kitendo kinachokuwa kimesababisha usumbufu au uvunjifu wa heshima kwa mahakama.

Hata hivyo lazima tendo la kudharau mahakama lionekane wazi au lithibitike kabla ya kutoa adhabu.

Swali: Nani anaweza kuchukuliwa hatua kwa kosa la kudharau mahakama; na wakati gani? Je, pamoja na uhuru wake, mahakama inaweza kuiadhibu serikali au bunge?

Serikali, mahakama na bunge ni mihimili ya dola. Ni mhimili gani wenye uwezo na mamlaka ya kuadhibu mhimili mwingine?

Bunge

Machi mwaka huu, mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) aliandaa hoja binafsi akitaka serikali itoe maelezo, imekuwaje imeangushwa kortini na kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba ‘hewa’ kutoka Richmond.

Hata kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa bungeni, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kujali maslahi ya chama chao, waliandaa mikakati kuikwamisha.

Walikaririwa wakisema, “Spika atasema bunge haliwezi kujadili suala linaloshughulikiwa na mhimili mwingine wa dola (Mahakama).”

Hakika hoja hiyo ilipowasilishwa, Spika Anne Makinda aliinyonga, akisema Bunge haliwezi kuingilia suala lililoko katika mhimili wa mahakama. Hoja ikafa.

Ni kweli, kesi ilikuwa mahakamani kutokana na wadau mbalimbali – mwandishi wa habari Timothy Kahoho na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC); wote wakipinga Dowans kulipwa fidia ya Sh. 94 bilioni kama tuzo baada ya “kuishinda” TANESCO katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa biashara (ICC).

Serikali

Katika kesi hiyo iliyoko mahakama kuu, Jaji Emilian Mushi alitoa amri kuzuia serikali na mmiliki wa Dowans kufanya mazungumzo ya aina yoyote kuhusu mitambo hiyo, ikiwemo kuiwasha bila ya ruhusa ya mahakama.

Lakini 20 Mei 2011, suala ambalo bunge lilijizuia kujadili (amri iliyowekwa na mahakama kuu), ilivunjwa na serikali.

Serikali iliratibu mazungumzo na mitambo ya Dowans ikauzwa kwa kampuni ya Kimarekani ya Symbion Power.

Kila kitu kikafanyika chapuchapu. TANESCO ikazungumza na Symbion ili iwauzie umeme; mmiliki wa Symbion Power akaitwa ikulu kuhakikishiwa ‘dili;’ mkataba ukasainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton akaja ‘kutia muhuri.’

Uko wapi uhuru wa mahakama? Kwanini Watanzania walipododosa suala hilo walizuiwa kwa madai kesi iko mahakamani; na bunge likadai haliwezi kuingilia mhimili mwingine? Mbona sasa ‘mzungu’ amevunja amri na mahakama iko kimya?

Kwa nini tusiseme kuwa mahakama si mhimili huru unaojitegemea,bali uko kwenye kwapa la serikali? Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na majaji wote wanateuliwa na Serikali (Rais). Kwa mfumo huu pekee, uhuru wa mahakama ni wa kinadharia.

Mfano mwingine kuthibitisha mahakama haiko huru, ila kama polisi, ni mkono wa chuma wa serikali, ni ilivyopuuzwa katika mgogoro wa umiliki wa ardhi ya machimbo ya madini ya dhahabu Bulyanhulu wilayani Kahama, Shinyanga.

Serikali ilijali vipande vya fedha mwaka 1996; ikadharau amri halali ya mahakama; ikaamrisha jeshi la polisi, watu 52 wakauawa.

Hadi leo mahakama haijalalamika kwamba ilidharauliwa na serikali kwa vile iko kwenye kwapa la serikali.

Ilikuwa hivi. Baada ya serikali kuuza kwa siri eneo la wachimbaji wadogowadogo kwa kampuni ya Kahama Mining Corporation (KMC) na kutaka waondoke bila fidia, walifungua kesi mahakama kuu kanda ya Tabora, kupinga kuondolewa katika eneo hilo.

Wakati kesi ikiendelea kortini, Julai 31, 1996 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Shija alitangaza kupitia Redio Tanzania (RTD sasa TBC Taifa), kwamba wachimbaji hao wanatakiwa kuhama katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kauli hiyo iliwashtua wachimbaji. Agosti 2, 1996, kupitia kamati yao, wachimbaji waliomba mahakama itoe amri ya kuzuia kusudio la serikali kuwaondoa mpaka kesi ya msingi itakapoisha.

Baada ya Jaji Lawrence Mchome wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kuridhishwa na hoja za waombaji, alitoa amri hiyo. Wachimbaji walirudi nyumbani wakishangilia na kuishukuru mahakama kwa kupima uzito wa hoja zao.

Jaji Mchome, katika uamuzi wake, alisema wachimbaji wadogowadogo wasihamishwe kwenye maeneo yao mpaka pande mbili hizo zitakapokutana tena kwenye mahakama yake.

Alisisitiza, “Kwa kuheshimu demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu, serikali inazuiwa kuingilia masuala ambayo bado yako kortini.”

Aliongeza, “Haki ya kimsingi inataka kwamba hata mchimbaji mdogo maskini asikilizwe kwanza kabla ya kutoa uamuzi ambao unaweza kuathiri maisha yake.”

Kiongozi wa serikali aliyekuwa anasimamia operesheni ya kuondoa wananchi ili kutoa nafasi kwa KMC, alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Meja Jenerali Tumainiel Kihwelu. Huyo ndiye alipelekewa amri ya muda ya mahakama kuizuia serikali kuhamisha wachimbaji.

Lakini mkuu huyo wa mkoa alikataa kupokea amri hiyo kwa madai kwamba yeye si mwajiriwa wa mahakama na kwa hiyo hawezi kufuata amri hiyo.

Ni kweli. Kilichotokea Agosti 7, 1996 kabla hata kwisha siku 30 walizotangaziwa; na kwa kudharau zuio halali la mahakama, maelfu ya watu walitimuliwa na wengine 52 kufukiwa kwenye mashimo wakiwa hai kwa ajili ya kufurahisha matajiri wa KMC – kampuni tanzu ya Sutton ya Canada.

Kwanini serikali ilidharau amri ya mahakama? Kwanini mahakama haikulalamika kokote kuwa imedharauliwa? Kama serikali inaweza kupuuza na isifanywe chochote, uhuru wa mahakama uko wapi?

Ni wakati gani tendo la kudharau mahakama linapewa uzito? Nani anapaswa kuheshimu uhuru huo na katika mazingira yapi?

Katika kile kilichoitwa kutekeleza amri ya mahakama ya Arusha, wiki tatu zilizopita, polisi jijini Dar es Salaam walimkamata na kumweka rumande, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe; halafu serikali ikatoa ndege ya kumpeleka Arusha mbele ya mahakama.

Kipindi hichohicho, mahakama hiyohiyo, ikatoa amri Askofu Valentine Mokiwa wa Kanisa la Anglikana, akamatwe kwa kudharau mahakama. Yeye, Askofu Mokiwa alisema, wanaotaka kumkamata waende!

Mbona hakuna vishindo vya polisi katika kumkamata Askofu Mokiwa, kama ilivyokuwa kwa Mbowe? Dharau ya Askofu Mokiwa ni tofauti na ile ya Mbowe?

Je, ni nani akidharau mahakama anaadhibiwa na nani akidharau mahakama anachekewa tu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: