Mahakama: Rostam anakamatika


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Rostam Aziz

SIRI kuhusu ushiriki wa Rostam Aziz, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mbunge wa Igunga, katika ufanikishaji mkataba tata wa Dowans, zinazidi kuanikwa.

Nyaraka kadhaa za Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), iliyoketi jijini Dar es Salaam, zinaonyesha Rostam ndiye alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika “dili” la Dowans Holdings SA na hata Richmond.

“Itoshe tu, kwa ajili ya kuweka rekodi sawa, kusema kuwa tumebaini kwamba Bw. Aziz alikuwa na ushawishi mkubwa, hata kama hauonekani wazi, kwenye mchakato mzima wa suala hili na hadi kufikia hapa tulipo sasa kwenye mgogoro huu,” inaeleza hukumu ya ICC katika kifungu cha 156, kilichopo ukurasa wa 38.

Majaji watatu waliosikiliza shauri hilo – Gerald Aksen kutoka Marekani, Swithin Munyantwali kutoka Uganda na Sir Jonathan Parker wa Uingereza – wanasema, “…baada ya kusikiliza kwa makini maelezo ya Henry Surtees, Mtunza Fedha wa kampuni ya Caspian (inayomilikiwa na Rostam Aziz), tumeridhika kwamba Surtees ndiye aliyekwenda Marekani kujadiliana na wamiliki wa Richmond na alitumwa kufanya kazi hiyo na Bw. Rostam Aziz.”

Akiwa mwajiriwa wa Caspian, Surtees alifunga safari ya kwenda Houston, Texas, nchini Marekani tarehe 7 Oktoba 2006 kuzungumza na wawakilishi wa kampuni ya Richmond na Portek International Limited.

Lakini katika maelezo yake ya awali kwa mahakama hiyo, Surtees kama Rostam, alificha taarifa sahihi juu ya aliyemtuma. Awali alidai kuwa aliombwa na kampuni ya Al Adawi kwenda Houston kwa ajili ya kuangalia na kuchambua uwezo wa kifedha na kibiashara wa Richmond iliyokuwa imepewa zabuni ya kufua umeme wa dharula nchini.

Hata hivyo, alipobanwa na wakili wa TANESCO kutoka kampuni ya Reed LLP ya Uingereza, Anthony White, kueleza ni nani hasa kutoka Al Adawi aliyemtuma kwenda Houston, Surtees “alijiumauma” na kutaka kukwepa kujibu swali hilo kabla ya kumtaja Rostam.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini wanasema kutajwa kwa Rostam katika hukumu ya Dowans kuwa ndiye alifanikisha mkataba huu, kumeondoa moja kwa moja kiwingu kilichotanda juu ya ushiriki wake katika suala hilo.

Tarehe 3 Mei 2009, Rostam alilitangazia taifa kupitia mkutano wake na waandishi wa habari katika hotel ya Kilimanjaro Kempinski, kutoifahamu Dowans; kutohusika na Richmond na kutojua lolote juu ya wizi wa Sh. 40 bilioni uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mahakama ya ICC ilielezwa kuwa siku moja kabla ya Surtees kwenda Marekani, Mwanasheria wa TANESCO, Subira Wandiba aliandikia Richmond kueleza kusikitishwa kwake na hatua ya kushindwa kutekeleza mkataba wake.

Kampuni ya Richmond iliahidi kuleta nchini majenereta ya kuzalisha umeme wa dharura Novemba mwaka 2006, lakini hadi Oktoba 2006, kampuni hiyo ilikuwa haijaweza kuzalisha hata megawati moja za kuingiza katika Gridi ya Taifa.

Katika mazingira hayo ya safari hiyo ya Surtees ya tarehe 7 Oktoba, 2006, ICC ilifikia maamuzi ya kuona kuwa Dowans ilinufaika na Rostam kuwa na uwezo wa kupata taarifa za ndani ya serikali na ndiyo maana ilifanya haraka kwenda Marekani mara baada ya barua ya TANESCO.

“Tunakubaliana na maelezo ya Surtees kuhusu mkutano wa Oktoba mwaka 2006 uliofanyika Houston. Tunaona kwamba mkutano huo wa Houston uliitishwa na Rostam mwenyewe mara baada ya kuwa amefanya mawasiliano ya namna fulani na Gire (Mohamed, anayetajwa kuwa mmiliki wa Richmond). Hata hivyo, si kazi ya ICC kwa sasa kujua nini hasa Rostam na Gire walizungumza,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine mahakama imeeleza kuwa Surtees alishindwa kujibu swali kuhusu vipi yeye – mwajiriwa wa Caspian – aliweza kufanya kazi kwa niaba ya Dowans Holding SA (DHSA), wakati hakuna mahali popote panapoonekana kuwapo ubia kati ya Dowans na Caspian.

Kwa mujibu wa ICC, Surtees alieleza kuwa alichojua ni kwamba anayetajwa kuwa mmiliki wa DHSA, Brigedia Suleiman Al Adawi, ni rafiki na mshirika wa kibiashara wa Rostam na kwamba mwanasiasa huyo alikuwa akimsaidia tu rafiki yake kupata kazi hiyo ya kuuza umeme nchini.

Hata hivyo, Surtees alipoulizwa tena na White kutaja mahusiano ya kibiashara kati ya Rostam na Al Adawi, alishindwa kueleza, badala yake akaishia kusema, “Mahusiano hayo ya kibiashara nilielezwa na Rostam mwenyewe.”

Tangu kuibuka kwa sakata la Dowans, Rostam amekuwa akikana kuhusishwa kwake na kampuni hiyo, akisema alichofanya ni kukubali kupewa nguvu ya kisheria (Power of Attoney)  na Dowans.

Kwa nguvu ya kisheria aliyopewa, Rostam ndiye mwenye mamlaka ya kukusanya fedha, kuajiri, kudai na kufungua kesi zinazohusu Dowans, jambo ambalo si la kawaida kwa watu wanaopewa nguvu za kusimamia kampuni.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: