MAHAKAMA YA ICC: Imeundwa kwa ajili ya Afrika tu?


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

PAMOJA na kwamba mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai – International Criminal Court (ICC), imeundwa ili kutumika kote duniani, lakini kwa mwenendo wake wa sasa, katu huwezi kuacha kusema ICC haikuundwa kwa kazi mahususi ya kushughulikia raia kutoka Bara la Afrika pekee.

Ndiyo maana baadhi ya wananchi wanapendekeza mahakama hii ya ICC iitwe mahakama ya Afrika ya Makosa ya Jinai – African Criminal Court (ACI). Sababu ni nyingi.

Kwanza, tangu kuundwa kwake mwaka 2002, watuhumiwa wote 27 waliofunguliwa mashitaka katika mahakama hiyo, wanatoka Afrika.

Hata aliyekuwa rais wa Liberia, Charles Taylor, ambaye awali alishitakiwa katika mahakama maalum iliyoundwa mwaka 2000 kwa makubaliano kati ya serikali ya Sierra Leone na Umoja wa Mataifa, mwaka 2006 kesi yake ilihamishiwa ICC.

Mahakama maalum ya Sierra Leone iliundwa maalum kusikiliza kesi za watuhumiwa wa mauwaji yaliotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone. Kati yao, watuhumiwa saba akiwamo Taylor wanashikiliwa katika gereza la Scheveningen jijini The Hague, Uholanzi.

Wengine waliobaki ama wako nje kwa dhamana au hawajakamatwa, ingawa tayari hati za kuwataka mahakamani zimeshatolewa.

Watuhumiwa hao 27 waliofikishwa ICC, wanatoka katika nchi za Sudan (6), Kenya (6), Congo-DRC (6), Uganda (5), Libya (3) na Liberia (1).

Baadhi yao, ni pamoja na Thomas Lubanga (Congo-DRC), Jean-Pierre Bemba (Congo-DRC), Uhuru Kenyatta (Kenya), Joseph Kony (Uganda), Omar al-Bashir (Sudan), Callixte Mbarushimana (Congo-DRC), Abdallah Banda (Sudan), William Ruto (Kenya), Muammar Gaddafi (Libya), Germain Katanga, Saleh Jerbo (Sudan) na Saif al-Islam Gaddafi (Libya).

Waliokamatwa na kuwekwa rumande huko The Hague, ni Thomas Lubanga, Germain Katanga, Mathew Ngudjolo Chui, Jean Pierre Bemba, Callixte Mbarushimana, Charles Taylor na Raska Lukwiya (ambaye amefariki dunia akiwa gerezani.                    
Orodha ya watuhumiwa hawa isichanganywe na ile ya watuhumiwa wengine waliotoka nje ya Bara la Afrika, ambao kesi zao zimekuwa zikiendelea hapo hapo The Hague, hususan wale waliotokana na vita ndani ya iliyokuwa Yugoslavia.

Watuhumiwa wa mauaji ya Yugoslavia walifunguliwa mashitaka katika mhakama maalum ya jinai ya kimataifa ya Yugoslavia – International Criminal Tribunal for the former Yugoslavia (ICTY).

Pili, jumla ya nchi 44 ambazo ni wanachama wa umoja wa mataifa ama hazikutia sahihi mkataba wa kuwapo kwa mahakama hiyo, au hazikuridhia. Miongoni mwa nchi hizo, ni China, India na Marekani.

Ingawa Marekani ilishiriki kwenye mchakato wote wa awali wa mkataba wa kuanzishwa ICC wakati wa utawala wa Bill Clinton, lakini ilijitoa mwaka 2001 wakati wa utawala wa Rais George W. Bush.

Akitangaza uamuzi wa kuitoa nchi yake kwenye ICC, Rais Bush alizionya nchi zote duniani ambazo zitathubutu kuwakamata na kuwatoa raia wa nchi yake katika mahakama ya ICC.

Tatu, kifungu Na. 8(a) (i-viii) cha mkataba wa ICC kinaorodhesha makosa ya kivita – war crimes – ikiwa ni pamoja na kuuwa raia kwa makusudi, kutesa au kudhalilisha binadamu, kumpa maumivu makubwa hadi kuharibu afya au viungo vyake vya mwili; uharibifu mkubwa usio wa lazima kwa mali na miundominu, kuwakamata watu na kuwahamisha kwa nguvu na baadaye kuwaweka kizuizini bila kufuata sheria.

Kile ambacho Marekani imekifanya nchini Iraq hakiwezi kwenda tofauti na makosa haya. Karibu vitendo vyote vya jinai vilivyofanywa na Marekani nchini Iraq mwaka 2003, viko chini ya vifungu hivyo.

Kwa mfano, hatua ya Jemadari mkuu wa majeshi ya Marekani, Rais George Bush alipoamrisha vikosi vyake vya anga kudondosha mabomu katika mji wa Falluja, hatua ambayo ilisababisha mamia ya watu wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake kuuwa, haiwezi kuwa si uhalifu wa kivit?

Lakini hadi sasa, ICC haijasema lolote kuhusu uhalifu huo uliofanywa na Bush na mshirika wake, waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair. Badala yake, Marekani imekuwa ikishinikiza kukamatwa kwa viongozi na raia wa Afrika kama vile Rais wa Sudan Hassan Al-Bashir.

Kuhusu mateso juu ya binadamu, askari wa Marekani wanatuhumiwa kutesa na kuwadhalilisha mamia ya wafungwa waliokuwa wakishikiliwa katika gereza la Abu-Ghraib mwaka 2004 nchini humo.

Nako nchini Sri Lanka, kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya kimataifa, katika miezi ya mwisho ya vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2009, majeshi ya serikali yaliuwa maelfu ya raia wasiokuwa na silaha, wengine wakiwa wamechukuwa hosptalini walikokuwa wakitibiwa.

Lakini pale umoja wa mataifa ulipotaka kuundwa kwa tume ya kuchunguza mauaji hayo, serikali ya Sri Lanka iligoma na kisha ikaho: Mbona umoja wa mataifa haukufanya hivyo kwa Marekani kwenye mauaji ya Iraq?

Pamoja na Marekani kujitoa katika ICC, bado ina ushawishi mkubwa katika kuamrisha nani akamatwe na nani aachiwe. Kwa mujibu wa taratibu za ICC, ili raia akamatwe sharti mwendesha mashitaka mkuu atoe hati ya kukamatwa; hati hizo hutolewa kwa misingi ifuatayo:

Ni kama mwendesha mashitaka mkuu ataombwa na nchi mwanachama, au baraza la usalama la umoja wa mataifa, au na ICC yenyewe baada ya kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali na kisha kufanya uchunguzi wa awali.

Ndivyo hati ya kukamatwa kwa Gaddafi na wenzake ilivyotolewa. Hata hati ya kukamatwa kwa Al-Bashir ilitokana na ombi lililowasilishwa baraza la usalama na mmoja wa wanachama wake.

Tofauti kubwa kati ya ICC na mahakama maalum kama ile ya mauaji ya Yogoslavia – ICTY iliyoundwa 25 Mei 1993 chini ya Azimio Na. 827 la umoja wa inaundwa kwa shughuli maalum kama ilivyokuwa katika vita vya Sierra Leone, vita vya Rwanda vya mwaka 1994, au vile vya Cambodia ambapo mahakama maalum iliundwa mwaka 2003 baada ya makubaliano kati ya serikali ya nchi hiyo na umoja wa mataifa kuhusu wahalifu wa mauaji ya kimbari wa uliokuwa utawala wa Khmer Rouge kati ya mwaka 1975 na 1979.

Mahakama inayolalamikiwa kwa ubaguzi wa wazi wazi dhidi ya watu wa Afrika ni hii ya kudumu – ICC – ambayo iliundwa kutokana na mkutano wa kimataifa huko Roma, Italia mwaka 1998.

Katika mkutano huo, dhamira ya makubaliano ya kimsingi yanayojulikana kama Rome Statute yalifikiwa na mahakama hiyo ya kudumu ilianza kazi rasmi mwaka 2002. Lengo lilitajwa kesi za jinai watu mbali mbali duniani wanaotuhumiwa makosa ya mauaji ya kimbari, makosa dhidi ya ubinadamu, makosa ya kivita, na makosa ya kufanya uvamizi wa kivita.

Dhamira ya kuwepo kwa mahakama ya aina hii ya kudumu ilianza tangu baada ya vita vya pili vya dunia, wakati ambapo mahakama maalum ya kimataifa iliundwa kwa ajili ya kuwashitaki wababe wa kivita kama vile Hitler na wenzake.

Hadi kufikia Julai mwaka huu, nchi 116 duniani zilikuwa tayari ni wanachama wa ICC. Wanachama wa ICC, ni nchi zote 26 za Amerika Kusini, nchi 43 za Ulaya, nchi 32 za Afrika na nchi 15 za Asia.

Jumla ya nchi 34 ikiwemo Russia zilizotia saini makubaliano ya Roma zimekataa kuridhia mkataba wa kuunda mahakama hiyo. Nchi nyingine tatu, Marekani, Sudan na Israel zimejitoa kabisa katika mkataba na zimezikana saini za wawakilishi wao walizoweka katika mkataba wa hapo awali.

Je, katika mazingira haya, nani anaweza kusema ICC imeundwa kwa ajili ya ulimwengu wote?

zakmalang@yahoo.com
0
No votes yet