Mahakama yanyonga serikali


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version
Serikali pwaa
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeipa serikali mtihani wa kutaka ikamate na kushitaki askari polisi waliohusika hasa na mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge, mkoani Morogoro na mkazi wa Dar es Salaam.

Mtihani huo umetokana na tamko la Jaji Salum Massati ambaye kwa saa tano alisoma hukumu ya kesi ya mauaji ya watu hao waliouliwa na askari wa jeshi la polisi 14 Januari 2006.

Jaji Massati ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, alisema washitakiwa wote tisa waliotolewa ushahidi mahakamani kwamba walihusika na mauaji hayo, hawana hatia yoyote.

Alisema upande wa mashitaka, ambao ni serikali ikishirikiana na Jeshi la Polisi lenye jukumu la kukamata na kuchunguza, pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) mwenye mamlaka ya kuchunguza ushahidi na kushitaki, umeshindwa kuthibitisha mashitaka waliyofungua dhidi ya maofisa hao.

Wafanyabiashara waliouliwa kikatili eneo la Msitu wa Pande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa kile ambacho Polisi walisema walikuwa majambazi, ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi, Mathias Lukombe na dereva wao wa teksi, Juma Ndugu.

Baada ya serikali kutoridhika na ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Polisi kwa maelekezo ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Rais Jakaya Kikwete alimteua Jaji Mussa Kipenka kuongoza tume ya uchunguzi mpya.

Ripoti ya Jaji Kipenka ilisukuma kukamatwa kwa aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), Abdallah Zombe ambaye wakati huo alikuwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP).

Jaji Massati, baada ya kutathmini ushahidi wa mashahidi 37 na vielelezo 23 vilivyowasilishwa na upande wa mashitaka, pamoja na kuzingatia ushauri wa wazee wa Baraza, alisema katika hukumu yake, iliyosikilizwa na mamia ya wananchi, kwamba anawaachia washitakiwa wote kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Alisema licha ya mahakama hiyo kuwa na shaka kuhusu kuhusika au kutohusika kwa washtakiwa na mauaji hayo, namna vifo vya wafanyabiashara vilivyotekelezwa, haionyeshi kwamba walioletwa mahakamani ndio waliohusika.

Hata hivyo, jaji Massati alikiri kuwa waliouawa walipigwa risasi kwa bunduki aina ya SMG eneo la msitu wa Pande siyo kwenye ukuta wa Posta Sinza kama walivyodai washitakiwa walipokuwa wakijitetea; tena wala hawakuwa majambazi.

Akasema, "Ila ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka haujaishawishi mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hawa."

"Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa vifo vyao havikuwa vya kawaida na isingewezekana wote wapigwe eneo moja kisogoni. Kama kweli kulikuwa na mapambano, hakuna ushahidi ulioeleza kuwa washtakiwa waliopo mahakamani hapa ndio walifanya hayo," alisema.

Alikiri kwamba damu iliyopatikana eneo la tukio ilichunguzwa na Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika ilikuwa ya binadamu. "Lakini hiyo haitoshi kuwatia hatiani washitakiwa na swali linabaki kuwa ni nani waliohusika kuwaua wafanyabiashara."

Jaji Massati alisema mahakama pia imejiridhisha kuwa wafanyabiashara waliouawa hawakuhusika kabisa na uporaji katika tukio la Bidco kama ilivyokuwa imedaiwa na washtakiwa.

Haijajulikana iwapo serikali itakata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, lakini Mwanasheria wa Serikali, Justus Nyaishozi, alisema jukumu lao ni kuwasilisha hukumu kwa wakubwa zao ambao ndio wataamua hatua inayofuata.

Jaji Massati ambaye alikosoa kwamba hakukufanyika uchunguzi makini wa tukio, alitoa fursa ya rufaa iwapo jamhuri haikuridhika na hukumu.

Walioachiwa huru baada ya kukaa rumande miaka mitatu mfululizo tangu walipokamatwa, mbali na Zombe, ni Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya Kinondoni, Christopher Bageni, Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki, Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew.

Wengine ni Koplo Emmanuel Mabula, Konstebo Michael Chonza, Koplo Abeneth Saro, Koplo Rajabu Hamisi na Koplo Festus Gwabisabi.

0
No votes yet