Mahakama yazuia kufutwa kwa MMD


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

MAHAKAMA Kuu jijini hapa imetengua uamuzi wa serikali ya Rais Michael Sata wa kukifuta chama kikuu cha upinzani cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) kwa kosa la kutolipa ada.

Kutokana na uamuzi huo, Jaji Jane Kabuka amemtaka Msajili wa Vyama, Clement Andeleki aendelee kuitambua MMD, hadi kesi ya msingi itakapomalizika kusikilizwa.

Uamuzi wa Jaji Jane Kabuka ulifanyika Ijumaa baada ya Jumatano Andeleki kutangaza uamuzi wa kuifuta MMD, lakini katibu mkuu wa chama hicho, Richard Kachingwe, na wabunge 53 waliwasilisha ombi la awali juu ya kusudio la kufungua shauri, na wakaiomba mahakama itangaze uamuzi wa serikali kuwa ni batili hivyo usitambuliwe.

“Baada ya kusoma na kufikiria hati ya kuomba korti itoe ufafanuzi, kwa kuzingatia hoja pamoja na kiapo cha kuthibitisha haya, natoa amri na kwamba inatumika kusitisha uamuzi wa Msajili wa Vyama uliotolewa 14 Machi 2012 hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa hadi mwisho,” anasema Kabuka.

Na mwenyekiti wa timu ya wanasheria wa MMD na ambaye amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa Republican, George Kunda, amesema chama kimeanza taratibu za kufungua kesi kwa ajili ya kupata ufafanuzi.

“…chama chetu cha MMD kitaendelea na shughuli zake za siku zote. Wabunge wetu wote 53 wataendelea kufurahia haki na marupurupu na madaraka ambayo yanatolewa na Bunge,” alisema Kunda.

Chama hicho kilichowahi kuwa chama tawala hadi mwaka jana, kilifutiwa usajili wake kwa kushindwa kulipa ada ya usajili kwa kipindi cha miaka 20 ambayo inafika dola za Kimarekani 75,000.

MMD ni moja ya vyama vikongwe nchini Zambia na kilifanikiwa kushika madaraka mwaka 1991, Frederick Chiluba alipomwangusha Kenneth Kaunda wa UNIP. Hivi sasa Zambia inaongozwa na Rais Michael Chilufya Sata wa Patriotic Front (PF).

0
No votes yet