Mahona: Natembea na ushindi Igunga


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
LEOPOLD Lucas Mahona

LEOPOLD Lucas Mahona, mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyepitishwa kuwania ubunge Jimbo la Igunga amesema tayari ana mtaji wa ushindi kutokana na kura alizopata katika uchaguzi mkuu mwaka jana.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Mahona alipata kura 11,321, huku Rostam Aziz wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akishinda kwa kura 35,674.

Mwalimu huyo wa zamani wa shule ya sekondari ya Tirav ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam anadai kuwa kura 11,321 alizopata mwaka jana ndio mtaji anaoingia nao katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika 2 Oktoba 2011 kujaza nafasi iliyoachwa na Rostam Aziz.

Mahona (28) ambaye sasa ni Meneja programu wa shirika la kiroho la Kanisa Katoliki la Pasada, anasema fikra zake ni namna ya kuchota kura kutoka jumla ya kura 35,674 alizopata Rostam ili atangazwe rasmi kuwa mshindi.

Tofauti na mwaka jana walipokuwa wagombea wawili tu, safari hii watakuwa wengi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho katika uchaguzi wa mwaka jana hakikuweka  mgombea, kimemteua Joseph Mwandu Kashindye.

Vilevile Mahona atachuana na Kamishna wa madini Dk. Peter Kafumu aliyepitishwa na CCM. Mwaka mmoja, Dk. Kafumu aliangushwa na Rostam Aziz katika kura za maoni.

Mgombea huyo kupitia CUF mwenye stashahada ya Utawala, Biashara na Uongozi aliyoipata katika chuo cha Dar City College cha jijini Dar es Salaam, anadai uchaguzi huo mdogo ndio utakaothibitisha ukweli wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Hii sasa ni nafasi yangu. Rostam hakunishinda kihalali katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana,” anadai Mahona katika mahojiano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Buguruni kwenye makao makuu ya CUF.

“Wahenga wanasema, kisicho riziki hakiliki. Rostam wa CCM alitumia hila nikabaki mimi pekee kuchuana naye. Baba yangu wa kiroho, aliyenisimamia ubatizo aliniletea ujumbe ili niachie jimbo, nilikataa,” anaeleza.

“Matokeo yake niliporwa ushindi. Rostam hakushinda, na matokeo yake hajamaliza mwaka ameachia jimbo. Hiyo ni mipango ya Mungu, sasa wana Igunga hawana cha kupoteza, yule kijana wao nimerudi.”

Rostam Aziz, kwa mara ya kwanza alishinda kiti hicho katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwaka 1994 kujaza nafasi iliyoachwa wazi na hayati Charles Kabeho. Mbunge huyo alishinda tena mfululizo miaka ya 1995, 2000, 2005 na 2010. Lakini baada ya uchaguzi mwaka jana hadhi yake ilichafuliwa sana ndani ya CCM.

Aprili mwaka huu, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliasisi falsafa ya kujivua gamba yaani ijitazame upya kwa nini ilipata ushindi mdogo katika uchaguzi mkuu uliopita.

Utekelezaji wa falsafa hiyo ulipoanza, aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na Rostam wakatajwa kuwa sababu kwa chama kuporomoka hivyo shinikizo likaanza wajiondoe.

Baada ya misukosuko hiyo, Rostam akaamua kujiuzulu ujumbe wa NEC na ubunge kutokana na alichoeleza kuwa ni kukerwa na siasa uchwara zinazofanywa na watendaji wakuu; Naibu katibu mkuu Bara, John Chiligati na Mkuu wa Idara ya Siasa, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye.

Baada ya Rostam kujiuzulu, mwalimu huyo amemtupia lawama mbunge huyo wa zamani kwamba hakufanya lolote kuondoa wala kupambana na umaskini wa wana Igunga katika kipindi chote cha miaka 17.

“Ukifika Igunga, utalia. Wale watu wa kule ni maskini ingawa wana utajiri wa rasilimali za kutosha.

“Nashindwa kuelewa huyo tajiri wa CCM alikwenda Igunga kufanya nini? Unaweza kusema kwamba kujitoa kwake si mipango yake, ni mipango ya Mungu. Hakufaa kuwa mbunge wa Igunga. Umaskini ndio unaturudisha nyuma, na CCM wanataka tubaki hivyo,” anafafanua kijana huyo ambaye aliteuliwa na Baraza Kuu la CUF Agosti 16, 2011.

Aanasema akishinda atahamasisha wananchi kutumia raslimali zilizopo ili waweze kujiletea maendeleo kwani “Igunga ni wilaya yenye neema ya aina yake. Jimbo lina rasilimali za kutosha kuweza kukomboa maisha ya wana Igunga.”

Igunga ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu na mifugo ya mwaka 2002 ina wakazi zaidi ya 325,547, ina kata 28 ambapo kata za Nsimbo, Igulubi na Igunga zina hazina ya madini ya dhahabu na almasi. Utajiri mwingine ambao anasema haujatumiwa vizuri na watu kujiletea maendeleo ni ng’ombe.

“Ni jimbo lenye ng’ombe wengi na madini ambayo kampuni tatu za kizalendo zimepewa leseni ya kuchimba, lakini hawafanyi kwa ufanisi,” anaeleza.

Aidha, amesema akishinda ubunge atahamasisha wakazi kutumia vilivyo mito na mabonde kwa ajili ya kilimo na bonde mojawapo analoona ni muhimu kwa uchumi wa wananchi na nchi ni bonde la Wembere lililo mpakani mwa Iramba na Igunga.

Vilevile Mahona anasema atahakikisha anafufua minada ya ng’ombe katika kila kata kufikia minne badala ya miwili. Baadhi ya kata ambazo minada imepungua kutoka minne hadi miwili ni Manonga na Igunga wakati Igulubi na Nsimbo umebaki mnada mmoja mmoja.

Kuhusu elimu, Mahona anasikitika kuona idadi kubwa ya wanafunzi inakosa madarasa na madawati na vijana wengi hawaendi shuleni.

Anasema, “Inauma sana unapokutana na kijana mdogo njiani haendi shule. Hakuna hata hamasa ya kushawishi vijana kusoma, hii ni changamoto kwangu kuhakikisha kwamba tunakuwa na elimu bora.”

Changamoto nyingine atakayokabiliana nayo akishinda ni kuhamasisha ujenzi wa shule za sekondari za kidato cha V na VI kwani “Ukubwa wote wa jimbo letu iko moja tu, Igunga Day yenye kidato cha tano na sita. Ni masikitiko.”

“Kwa kipindi changu cha miaka minne ambacho wanachi watanipa ridhaa, nitahakikisha angalau kila kata inakuwa na sekondari ya kidato cha tano na sita, wakiwamo walimu na vifaa vya kufundishia,” anasema Mahona.

Changamoto nyingine ni uboreshaji barabara, kuwapa wananchi maji safi na salama, kupigania mfuko wa kutoa matibabu kwa gharama nafuu wa (CHF) pamoja na kupigania haki, usawa na demokrasia.

“Lakini pia kwa wana Igunga ni kwamba kuna uonevu wa polisi wasaidizi. Kuna vijana wamechukuliwa na kampuni moja ya ulinzi ambao wanasumbua zaidi baadhi ya wananchi kwa kuwapakazia kesi. Sasa hilo nalo mimi mwenyewe nitafanyia kazi,” anasema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: