Majaji kataeni mipaka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

MAJAJI Joseph Warioba na Augustino Ramadhani wanafahamika. Wote wamestaafu kutumikia umma.

Lakini sasa, wamepewa kazi ya umma – kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye wajumbe 30.

Wakati Warioba amestaafu uwaziri mkuu miaka kadhaa iliyopita, Ramadhani amestaafu juzi tu ujaji mkuu wa Tanzania.

Tume ya kusimamia ukusanyaji wa maoni ya wananchi na kuratibu uandikaji wa rasimu ya katiba mpya ya kwanza kushirikisha maoni ya wananchi wenyewe, itaamua mustakabali wa taifa.

Ni kazi nzito nyingine ambayo wanatume wakikubali kuifanya kwa kudhibitiwa na hisia za watawala, wataichezea na hivyo kuchezea maslahi makubwa ya umma na taifa.

Fursa wanayopewa wananchi kutoa maoni haipaswi kuminywa kwa namna yoyote. Tume ihakikishe milango yote ya watu kutoa maoni inafunguliwa.

Kwa kuwa katiba zote mbili zinatambua wananchi ndio wenye mamlaka ya kuendesha nchi, ni ujinga kuwawekea mipaka wajadili hili na waache lile. Tume kataeni kufungwa mikono.

Tunaamini kuwa muungano ndio msingi mkuu wa kuendesha jamhuri iliyopatikana baada ya kuunganishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mwaka 1964.

Kwa hiyo, muungano unahitaji kujadiliwa kwa kina na Watanzania wa pande zote mbili – Tanzania Bara na Zanzibar.

Watu wapendekeze wanavyotaka muungano uwe na siyo kufunika matatizo ya msingi ambayo viongozi wameshindwa kwa miaka yote kuyatatua.

Lipo jambo jingine muhimu – ulinzi wa raslimali za taifa. Kihistoria, raslimali hizi, nyenzo muhimu kwa maendeleo ya nchi na watu wake, hazijasimamiwa vizuri.

Matokeo yake, uhuru wa nchi umebaki jina tu lakini wananchi wanadhoofika kwa umasikini na ufisadi wa raslimali zao.

Kwa kuyatazama hayo, ndipo tunapowaona majaji Warioba na Ramadhani, pamoja na wajumbe wenzao, walivyo na kibarua kigumu.

Wajenge dhamira njema. Wasikilize umma na wazingatie maoni na matakwa yao. Mwisho waheshimu vile wanavyotaka kuongozwa katika miaka mingine kadhaa ijayo.

0
No votes yet