Majanga 6 ya mwaka 200


Charles Nkwabi's picture

Na Charles Nkwabi - Imechapwa 14 January 2009

Printer-friendly version

KWENYE sherehe za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kumeibuka tathimini mpya inayoonyesha waziwazi kuwa Tanzania sasa siyo tena “kisiwa cha amani.”

Mahubiri ya maaskofu na wachungaji wa makanisa mbalimbali kwenye madhabahu wakati wa sikukuu ya Krimasi hawakuona sifa yoyote njema kwa raia wa nchi hii kujivunia zaidi ya kilio na machungu wanayopata Watanzania.

Janga la kwanza ni mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi – Albino.  Mtu mwenye ulemavu wa ngozi hakuomba awe vile alivyo. Kama binadamu mwingine yeyote, albino anayo haki ya kuishi popote bila kupigwa au kisimangwa.  Sina uhakika iwapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiulizwa na viongozi wenzake juu ya mauaji ya maalbino nchini Tanzania na amekuwa akitoa jibu gani.

Wako wapi sungusungu vijijini waimarishe ulinzi albino? Mbona serikali huwa haishindwi na jambo kuhusu ulinzi? Imekuwaje serikali imekubali kushindwa na kuaibishwa na watu wachache wanaoua albino?

Wako wapi polisi? Ziko wapi kamati za ulinzi na usalama za kila kijiji, kata, wilaya na mkoa ziwalinde albino na kudhibiti wauaji. Maswali ni mengi lakini tuishie hapo.

Janga la pili ni wizi uliokithiri kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kashfa kuu ya Richmond. Ni ufisadi mtupu.

Kwa mujibu wa Profesa Mwesiga Beregu, “Utaratibu wa kumkamata mtu mmoja mmoja kujibu tuhuma za wizi wa fedha za EPA waweza kupotosha lengo kwa sababu kampuni zimeanzishwa na jopo la watu na vikao vilikubaliana, tena kwa kuwahusisha viongozi ngazi za juu.”

Janga la tatu ni bei ya mafuta – dizeli, petroli na mafuta ya taa. Bei kubwa za mafuta ndizo zinafanya gharama za maisha kupanda na Watanzania kuelemewa vibaya sana, kwani vipato vyao ni aibu hata kuvitaja.

Wafanyabiashara wasingeachiwa kupanga bei za nishati hii kama wanavyotaka. Matokeo ya hayo ni kwamba hapa nchini, mafuta yanaendelea kupanda bei wakati duniani kote bei inapungua siku hadi siku.

Serikali inawajibikaje katika hili? Kama hailindi masilahi ya wananchi wake, basi imeshindwa kazi.

Janga la nne ni kuongezeka kwa ufa kati ya walionacho na wasionacho. Wataalam wanakadiria kuwa wananchi wapatao asilimia 10 ndio wanashikilia “mali za kumwaga,” wakati asilimia 90 ni masikini wa kutupa.

Hili ni bomu kubwa na baya kuwahi kutokea katika historia ya nchi hii; na siku likilipuka hakuna atakayezima moto wake.

Bomu hili limechochewa na wizi usio na kiwango kutoka serikalini, BoT na mashirika ya umma. Si MKUKUTA, MKURABITA wala MKUKUBITA imesaidia kuleta maisha bora kwa wananchi.

Janga la tano ni migomo ya walimu, migomo ya wanafunzi na kufungwa kwa vyuo vikuu; madai na maandamano ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Hili ni janga linalokuja na sura mbili. Moja ni ile ya kuifedhehesha serikali ambayo imeshindwa kutenda. Sura ya pili ni ile ya kiharakati ya wananchi kuamua kudai haki zao. Ni janga linaloiweka serikali mahakamani.

Janga la sita ni lile la mawaziri watatu kujiuzulu, akiwemo waziri mkuu kufuatia kashfa ya utoaji zabuni ya kufua umeme kwa kampuni ya kitapeli ya Richmond ambayo haikuwa na ofisi, fedha, wataalam wala vifaa/mitambo.

Hili lilifuatiwa na kuvunjwa kwa baraza la mawaziri. Hata hivyo wananchi wametambua umuhimu na uwezo wa vyombo vya habari pale vinapong’ang’ania hadi “kinaeleweka.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: