Majangili faru wa Kikwete hawa hapa


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Faru weusi wa Serengeti

USALAMA wa Taifa na Polisi wametajwa katika ujangili unaoendeshwa kwenye mbuga za wanyama za taifa nchini, MwanaHALISI limegundua.

Viongozi waandamizi kadhaa pia ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wametajwa katika biashara haramu ya wanyamapori.

Ujumbe wa simu ya mkononi (sms) ni miongoni mwa njia zilizosaidia kupatikana kwa baadhi ya taarifa hizi.

Ofisa mmoja aliyefanikiwa kukwepa mtego wa polisi, alimwandikia mwenzake, “…nashukuru sana…nimewafuata watu nyumbani kwao kwa ajili yako, kumbe una mipango mingine usiniambie, sasa hivi natembea kwa miguu kwa ajili yako…kula vizuri na familia yako, mfurahishe mke wako mimi acha nife ovyo.”

Taarifa kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na jeshi la polisi zinasema, kushamiri kwa ujangili nchini kunatokana na kuhusika kwa baadhi ya viongozi hao wakubwa.

“Nadhani umesikia taarifa za kuuawa kwa faru huko (mbuga ya wanyama ya) Serengeti, utajiri wa ghafla alioupata waziri (jina tunalo) na jinsi twiga walivyopelekwa nchi za nje kwa ndege.

“Hiyo ni kazi ya mtandao mkubwa wa ujangili nchini unaohusisha viongozi waandamizi serikalini, idara ya usalama wa taifa na polisi,” ameeleza ofisa mmoja mwandamizi serikalini.

Anasema idara ya wanyamapori nchini, ni “moja ya maeneo ambayo yanaweza kumtajirisha mtu kwa haraka mno kuliko hata madini.”

Kuibuka kwa habari hizi kumekuja baada ya twiga wawili kutoroshwa nchini kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro na faru wawili kuuawa katika mbuga za wanyama za Serengeti, mkoani Mara.

Taarifa za kuuawa kwa faru zilitolewa na askari waliokuwa doria maeneo ya mlima Ngoma, tarehe 9 Mei 2012.

MwanaHALISI limepata baadhi ya nyaraka zinazothibitisha taarifa za mtandao wa ujangili nchini unaohusisha baadhi ya viongozi wakubwa ndani ya serikali.

Taarifa zinataja jina la kiongozi mmoja katika Idara ya Usalama wa Taifa aliyetajwa kwa jina la David Simwaza, ambaye “…alipenyezwa mbugani kushughulikia majangili, lakini amekuwa mmoja wa majangili hatari nchini.”

Jina la Simwaza limetajwa katika ukurasa wa nne wa taarifa iliyowasilishwa wizarani na kikosi kazi kilichopewa jukumu la kufuatilia ujangili huo.

“Huyu, kama alivyo Peter Matyampula, ni mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Naye alikuwa ni msiri wa usalama wa taifa ambaye walimweka ili aweze kuufumua mtandao mzima wa wafanyabiashara haramu wa meno ya tembo katika Wilaya ya Mpanda,” imeeleza taarifa.

Baada ya kupata “maslahi makubwa toka kwa majangili, aligeuka na kuanza kushirikiana moja kwa moja na majangili,” inaeleza sehemu ya taarifa ya kikosi kazi.

Taarifa ya kikosi kazi inasema, “Katika tukio hili, mtuhumiwa aliwafuata wafanyabiashara hawa haramu ili waje wanunue meno ya tembo Mpanda. Alikuwa akiwasiliana na mtuhumiwa Peter Matyampula aandae mzigo uwe tayari ili wakifika tu waununue.”

Hapa ndipo David Simwanza alimwandikia Peter Matyampula akimlalamikia kuwa “amemuuza” na kwamba “…kula vizuri na familia yako, mfurahishe mke wako mimi acha nife ovyo.”

Taarifa za kikosi kazi zinasema baadhi ya nyara husafirishwa kwa kutumia helikopta ya Jeshi la Polisi.

Sehemu ya mwisho ya taarifa ya hifadhi ya Katavi inasema, “Kwa ujumla watuhumiwa wanaonekana kuwa pamoja na kwamba hawajawahi kukamatwa; ni wafanyabiashara haramu wazoefu katika tasnia hii.”

Taarifa hiyo yenye kichwa cha maneno, “Taarifa ya doria ya Katavi,” ya 17 Juni 2012, inaeleza kuwa “Mtuhumiwa Joseph Ngondo, ana shemeji yake mmoja ambaye ni mmoja wa marubani wa helikopta ya Jeshi la Polisi.

“Huyu husafirisha mizigo yake kwa helikopta hiyo na pia amefanya kazi hii akishirikiana na watu wenye nyadhifa kubwa serikalini.” Taarifa hiyo inataja majina ya watu hao wenye nyadhifa kubwa.

Taarifa inasema wakati Ngondo anakamatwa, alisikika akisikitika kwa kusema, “… sijui itakuwaje kwani RSO Shinyanga (mkuu wa usalama wa mkoa) anamfahamu; na endapo atasikia kuwa amekamatwa kwa tuhuma hizi sijui atajisikiaje.”

Gazeti hili limeshindwa kufahamu haraka uhusiano wa RSO wa Shinyanga na Ngondo kama ni wa kikazi au kindugu. Ufuatiliaji unaendelea.

Aidha, Ngondo ambaye alikuwa mtumishi katika Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuachishwa kazi kwa tuhuma za ujangili, ameonekana kuwa na mawasiliano kadhaa na watu mbalimbali akiwamo aliyekuwa mhifadhi intelijensia wa Serengeti, Festo Kiswaga, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

Inaelezwa katika taarifa hiyo kuwa ni Kiswaga aliyetonya kikosi kazi kwamba Ngondo ni jangili hatari na hujihusisha katika biashara ya meno ya tembo sehemu nyingi nchini.

Taarifa inasema doria iliyofichua mtandao wa ujangili ilifanyika 16 Juni 2012 baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya kundi la “wafanyabiashara wa meno ya tembo.”

Raia hao walielekeza kuwa wafanyabiashara hao, wenye gari aina ya NOAH watakuwa wakienda njia ya Tabora, karibu na kijiji cha Ikondamoyo, ili kuchukua meno ya tembo.

“Baada ya taarifa hiyo, kikosi kiliandaliwa pamoja na gari aina ya L/Rover Tdi SU 38965. Ilipofika majira ya saa 5.30 usiku, kikosi kiliondoka hadi barabara ya Tabora, eneo la kati ya kijiji cha Msaginya na Ikondamoyo, na kuweka mtego,” inaeleza taarifa hiyo kwenye aya ya pili baada ya utangulizi.

Inasema, “Majira ya saa 11 alfajiri gari aina ya NOAH, jeupe lenye usajili Na. T 983 BZJ lilifika hapo na kusimamishwa. Lilikuwa na watu saba (7); kati yao wanawake ni wawili.

“Askari walijitambulisha na kuwaeleza nia yao ya kulifanyia upekuzi…katika upekuzi huo askari walifanikiwa kukamata meno matatu ya tembo yenye uzito wa kilo 31, mzani mmoja na msumeno mmoja,” imeeleza taarifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki, tayari amefikisha taarifa hii kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Anasema watuhumiwa 25 wa mauaji ya faru wa Serengeti tayari wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika waraka wake kwa Pinda, Balozi Kagasheki anasema, “Napenda kuchukua nafasi hii kukuarifu kwamba watuhumiwa 25 ambao ni (sehemu ya) mtandao wa watuhumiwa wa mauaji ya faru kwenye hifadhi ya Serengeti, tayari …baadhi yao wamekamatwa.

Amemwambiua Pinda kuwa majangili wanamiliki kinyume cha sheria, silaha zisizopungua 16 zikiwamo bunduki za kivita aina ya SMG zenye Na. 458 na 375 na bunduki aina ya G3 - Mark IV. Nusu ya silaha hizo ni silaha za kivita…” ameeleza.

Katika kipindi cha 2 Januari na 26 Juni mwaka huu, hifadhi ya Serengeti pekee imefanikiwa kukamata majangili 369 na silaha za kivita aina ya SMG sita, Mark IV moja, shotgun moja aina ya 303. Risasi zilizokamatwa ni aina ya 7.62mm (559), G3 sita (6).

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina miradi mitatu ya kuhifadhi faru, ambayo ni Nyamalumbwa, Moru na Ndasiata, ambako walihifadhiwa faru walioletwa nchini kutoka Afrika Kusini.

Nyaraka zinaonyesha faru walitoweka kwenye hifadhi hiyo ya Serengeti mwanzoni mwa miaka ya 1980, baada ya wimbi la majangili kuvamia eneo hilo kwa kuendesha biashara hiyo bila ukomo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: