Majeraha ya uchaguzi hadi lini?


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
January Makamba

KONGAMANO la siku moja lililolenga kujadili majeraha yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliopita, lilifanyika 5 Mei 2011 katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.

Liliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na  kufunguliwa na mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Lipumba ndiye anayeshikilia uenyekiti wa TCD kwa sasa.

Alikuwa mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Makamba aliyeanza mada yake kwa kusema, “Majeraha mengine ni ya kujitakia,” jambo ambalo liliamsha hisia kuwa mjumbe huyo hakwenda kwenye kikao hicho kwa lengo la kutafuta suluhu bali kutetea chama chake.

Makamba alianza kwa kujichanganya kwa kusema uchaguzi ulikuwa huru na haki, lakini papo hapo akasema ulikuwa na matatizo mengi.

Uko wapi uchaguzi huru na wa haki wakati wananchi waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, hawakukuta majina yao kwenye vituo vya kupigia kura?

Uchaguzi upi ni huru na wa haki wakati katika baadhi ya maeneo ambayo wagombea wa upinzani walikuwa wanaongoza kwa idadi kubwa ya kura, matokeo yalicheleweshwa kutangazwa na yalitolewa baada ya shinikizo la wananchi?

Penye uchaguzi huru na wa haki hakuna wagombea wanaopitishwa tu kwa madai ya kutokuwa na wapinzani, kama ilivyokuwa pia kwa Makamba mwenyewe.

Wabunge takribani 10 waliopatikana kwa njia hiyo, hawawezi kuitwa wawakilishi halali wa wananchi. Ni wabunge waliopatikana kutokana na kuwapo kwa mfumo mbaya wa sheria na mazingira yasiyo huru wala ya haki.

Angalia jijini Mwanza, jimbo la Nyamagana. Kama siyo busara ya Tume ya Uchaguzi (NEC) na uthabiti wa Ezekia Wenje – mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hivi sasa Lawrance Masha angekuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo.

Masha alikuwa ametangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Mwanza, Wilson Kabwe kuwa mbunge aliyepita bila kupingwa.

Uko wapi uhuru wa wananchi kujichagulia mbunge wanayemtaka? Je, haya kama siyo majeraha ya uchaguzi ni nini hasa?

Lakini mada ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitivo cha Sayansi ya Siasa, Bashiru Ally ilifurahisha wengi. Bashiru alitaja sababu saba zilizoleta majeraha ya uchaguzi.

Miongoni mwa sababu hizo, ni taasisi zilizosimamia uchaguzi kuwa chini ya mamlaka ya rais ambaye pia alikuwa mgombea katika uchaguzi uliyopita.

Nyingine ni kutokuwapo sheria inayowataka wagombea ubunge na udiwani, waliopita bila kupingwa, kupigiwa kura; kushuka kwa idadi ya waliojitokeza kupiga kura na madai kuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa ndiye alikuwa mshindi.

Akichambua mada yake, Bashiru alisema NEC ilitangaza watu waliojiandikisha kuwa ni 20 milioni. Lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa takribani 8 milioni.

Alisema kutokana na idadi hiyo, hakuna mwenye kuamini ripoti ya wapigakura ilivyotolewa na NEC.

Kuhusu hatua ya Dk. Slaa kutuhumu idara ya usalama wa taifa kuchakachua matokeo yake na taarifa hizo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, huku idara hiyo ikishindwa kujitetea, ni jambo ambalo limeacha wengi na mshangao.

“Jeraha hili haliwezi kupona kwa kipindi hiki cha miaka mitano, kwa sababu kuu kwamba matokeo ya urais hayawezi kuhojiwa mahakamani,” alieleza Bashiru.

Aliyewaacha washiriki wa kongamano mdomo wazi, ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa. Yeye mbali na kukiri kuwa uchaguzi uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa, alisema CCM kilivunja baadhi ya sheria za uchaguzi na zile za nchi katika kuhakikisha kinaendelea kuwa madarakani.

Kauli ya Tendwa ilikuwa na maana moja: Kwamba alikuwa anaomba nafasi ya kuishi gerezani kwa kuwa yeye na ofisi yake walishiriki kuvuruga uchaguzi.

Tendwa, huku akijua kuwa hakuwa na mamlaka ya kutenda alichokifanya, aliyeruhusu Kikwete kufanya kampeni mpaka saa moja usiku. Alinyamazishwa na NEC baada ya kufuta ruhusa yake.

Lakini wakati hayo yakitendeka, tayari Kikwete alikuwa amevunja taratibu ba kanuni, huku Tendwa na wenzake wakishidwa kumkemea.

Pamoja na kwamba Tendwa hakueleza wajumbe wa kongamano taratibu na sheria zilizovunjwa na CCM, lakini Kikwete na chama chake wanatuhumiwa kutumia fedha nyingi kuliko zile zilizoruhusiwa na  kutumia fedha za umma kwa kampeni za chama chake.

Si hivyo tu. Mke wa Kikwete, Mama Salma Kikwete naye alitumia vyombo vya umma kufanyia kampeni mumewe.

Kasoro nyingine alizotaja zilikuwa ni kuchelewa kufunguliwa vituo vya kupigiakura na kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura. Baadhi ya majimbo na kata zilishindwa kupiga kura siku ya uchaguzi, 31 Oktoba 2010.

Alisema katika baadhi ya maeneo, hasa yale ambayo wagombea wa upinzani walikuwa wanaogoza kwa kura, kulitokea vurugu wakati wa kutangaza matokeo.

Hata hivyo, Tendwa alijitapa kuwa sheria mpya ya gharama za uchaguzi ilileta nidhamu na imeondoa dhana ya ushindi wa kishindo kwa wagombea wote waliokuwa wakitegemea kutumia pesa kushinda uchaguzi.

Akichangia mada ya Tendwa, mmoja wa washiriki wa kongamano hilo alisema, hatua ya msajili wa vyama kukiri kuwa CCM ilikiuka sheria baada ya kuona jahazi linataka kuzama, huku yeye akinyamazia vitendo hivyo, inatosha kumfukuzisha kazi.

Alisema, “Katika nchi ambazo zinaheshimu utawala wa sheria, leo hii Tendwa alitakiwa kufutwa kazi. Lakini kwa kuwa aliowasaidia kuvuruga uchaguzi ndio haohao waliopo madarakani, hatutarajii huyu bwana kuwajibishwa,” alisema kwa sauti ya ukali.

Hata hivyo, washiriki walishindwa kupata ufafanuzi wa maelezo ya Tendwa kwa kuwa wakati washiriki wanaanza kuchangia mada yake, tayari yeye alikuwa ameondoka. Haikuelezwa sababu za kuondoka kwake mapema.

Naye Victor Kimesera, mwakilishi wa CHADEMA alisema, ili uponye jeraha ni vyema kujua kwanza chanzo cha jeraha hilo.

Kwa mfano, Kimesera alisema tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, majeraha ya uchaguzi yamekuwa ni yaleyale na serikali imeshindwa kuyatafutia tiba.

“Tusipokuwa makini na kutafuta chanzo na sababu za majeraha ya uchaguzi, tutakutana tena 2016 baada ya kumalizika uchaguzi mkuu ujao kuzungumza tena juu ya majeraha ya uchaguzi,” alisisitiza.

Alipendekeza kurekebishwa kwa sheria zote zinazotawala uchaguzi; sheria ya gharama za uchaguzi na kuwapo kwa katiba mpya.

Mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema hatua ya NEC kuchelewesha daftari la wapigakura kwa vyama vya upinzani wakati ikilitoa kwa CCM mapema, kulichangia kuvurugwa kwa uchaguzi.

Mtatiro alituhumu asasi ya REDET na Synovet kutoa ripoti potofu juu ya mgombea wao, Profesa Lipumba jambo ambalo alisema lilichangia kupunguza kura zake.

Je, majeraha haya yanaweza kupona wakati anayeyasababisha anaendelea kuyatonesha kila mwaka na kila uchaguzi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: