Majeraha ya udini yataangamiza taifa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

KONGAMANO la kitaifa la Waislamu juu ya kile kilichoitwa, “Kupambana na mfumo Kikristo” lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubelee, jijini Dar es Salaam, 16 Oktoba 2011, limeibua mengi.

Kwanza, limethibitisha madai ya baadhi ya watu, kwamba shutuma, tuhuma na lawama zinazohusu mfumo wa uendeshaji serikali nchini, nyingi hazifanyiwi utafiti wa kutosha.

Kwa mfano, wanazuoni wa kiislamu waliohutubia kongamano hilo la siku moja na kutoa walichoiita, “Waraka mrefu wa utafiti,” wametuhumu kitendo cha serikali kutoa misamaha mikubwa ya kodi kwa taasisi za kikristo zinazotoa huduma za jamii nchini, kuliko ilivyofanya kwa madhehebu ya kiislamu.

Aidha, wanazuoni wanasema serikali imekumbatia mfumo kikirsto; inaendeshwa kikirsto na imewageuza waislamu kuwa watu wa daraja la chini.

Pamoja na mambo mengine, wanatuhumu kuwapo wakurugenzi waislamu wawili tu, kati ya tisa katika wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi; mkaguzi mmoja kati ya wakurugenzi wakuu 11 wa kanda; maofisa elimu wa mikoa watano kati ya 21 na maofisa elimu ya msingi 23 kati ya 125.

Ukiangalia kwa haraka madai haya, unaweza kukubaliana nayo. Lakini ukijipa muda, ukapima na kutafakari kilichopo na kinachodaiwa kuwapo, utaweza kubaini kuwa kilichosemwa, ama kimepotoshwa au waliotumwa kufanya utafiti kuna mambo bado hawajaeleza.

Kwa mfano, serikali haiwezi kuwa inatoa fedha za ruzuku au misamaha ya kodi kwa taasisi zinazotoa huduma za kijamii kwa lengo la kubeba ukirsto. Inafanya hivyo kutokana na kuelemewa na mzigo wa uendeshaji serikali; mzigo unatokana na kufikia ukomo wa kufikiri katika kuhudumia wananchi.

Ukiona serikali haina uwezo wa kujenga na kuendesha hospitari zake yenyewe zinazokidhi mahitaji ya wananchi wake; haiwezi kuendesha shule, vyuo vya elimu ya juu wala vyuo vya ufundi vyenye hadhi na viwango vinavyohitajika, basi ujue hapo kuna tatizo.

Matokeo yake, serikali inaamua kujisalimisha ama kwa wahisani wa nje au ndani. Baadhi yao ni madhehebu ya kidini.

Wakati taasisi za kikirsto zinamiliki msululu wa hospitali zikiwamo Bugando Medical Centre, Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) na hospitari za wilaya karibu 28 nchini nzima, madhehebu ya kiislamu hayana hata hospitali moja ya rufaa, wala hospitali yenye hadhi ya kuitwa hospitali kuu ya mkoa au wilaya. Imeishia kwenye vituo vya afya na zahanati.

Kwa upande wa vyuo vikuu, madhehebu ya kikirsto yanamiliki chuo kikuu cha St. Augustine (SAUTI) cheyenye matawi ya Nyegezi, Bugando, Tabora, Iringa, Mtwara, Moshi na Bukoba.

Vyuo vingine ni St. John Dodoma, Mount Meru Arusha, Kisanji Mbeya, Chuo Kikuu cha Arusha na Tumaini chenye matawi Iringa, Moshi, Makumira Arusha, Lushoto Tanga, Dar es Salaam na Mbeya. Hivi sasa, madhehebu hayo yako mbioni kufungua matawi mawili ya Karagwe na Bukoba mjini.

Taasisi za kiislamu zinamiliki chuo kikuu kimoja tu – Morogoro Islamic University (MIU), tena ambacho kiwanja na majengo yake yalitolewa na serikali. Madhehebu ya kiislamu hayamiliki hata taasisi tano zinazojihusisha na elimu ya juu. Nyingi ya taasisi za kiislamu zinaishia kumiliki shule za msingi na sekondari.

Je, katika hili, serikali yaweza kulaumiwa kwa kutoa misamaha kwa madhehebu ya kidini, kwa kisingizio kwamba wanaonufaika zaidi ni madhehebu ya kikirsto?

Kilichopo ni hiki: Serikali imetoa upendeleo kwa madhehebu ya kidini kusaidia katika eneo hilo, hasa afya na elimu. Yule anayefikisha viwango vinavyotakiwa, ndiye anayepewa ruzuku, bila kujali muislamu au mkristo.

Lakini kuna hili pia. Anayetoa msamaha wa kodi kwa mujibu wa sheria ni waziri wa fedha. Kwa sasa, Mustaph Mkullo; ni muislamu. Ndani ya wizara yake, Mkullo anasaidiwa na manaibu waziri wawili –  mmoja ni muislamu, Pereira Ame Silima. Yupo pia katibu mkuu, Ramadhan Khijjah; ni muislamu.

Mkullo amekuwa waziri wa fedha tangu mwaka 2008 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuunda upya baraza lake la mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa aliyetuhumiwa kuingiza nchi kwenye mkataba tata wa Richmond.

Alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Zakia Meghji. Ni muislamu. Sasa waislamu wanataka kusema, Mkullo anawahujumu? Kunahitajika utafiti wa ziada kuthibitisha hili.

Je, ni taasisi ngapi za kiislamu zilizopeleka maombi ya msamaha wa kodi kwake zikakataliwa? Misamaha hiyo iliyoombwa ilikuwa na thamani ya kiasi gani? Nani aliyeoomba? Ni taasisi za kiislamu au watu waliotaka kuzitumia taasisi hizo kujinufaisha binafsi?

Hata kama wakurugenzi katika wizara hiyo, wengi ni kutoka madhehebu ya kikristo, hiyo haiwezi kuhalalisha madai kwamba yanayotendeka ndani ya wizara hiyo yanatokana na shinikizo la kidini; misimamo ya kidini na waislamu wameathirika kwa kiwango kikubwa na jambo hilo.

Hata hoja ya kuwapo wakristo wengi kwenye wizara ya elimu, inaweza kuonekana imetolewa bila utafiti wa kina. Ndani ya wizara ya elimu, pamoja na wakurugenzi, makamishina na watendaji wengine, yupo waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa. Huyu ni muislamu. Anasaidiwa na naibu waziri, Kassim Majaliwa. Naye ni muislamu.

Hivyo basi, kama madai haya yana ukweli, Dk. Kawambwa na Majaliwa watakuwa ndiyo wanatumika kuhujumu waislamu?

Jambo moja ni muhimu. Waislamu wasiendekeze malalamiko. Bali wajipange kama taifa kutafuta njia ya kujikwamua. Watafute mbinu elekezi zinazojenga hoja za kujadili na kuibua utambuzi, badala ya kuibua malalamiko ya “kusalitiwa kwa waislamu katika siasa za Tanzania.”

Kwa mfano, Rais Kikwete hakuteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais kwa sababu yeye ni muislamu. Alichaguliwa baada ya kuonekana anaweza kushindana na wagombea wengine wa upinzani na kushinda.

Aliposhika nafasi hiyo, akateua wasaidizi kutoka madhehebu mbalimbali, kutokana na jinsi walivyojitokeza kwenye kugombea ubunge na kushinda.

Hivyo basi, kuendeleza madai ya kubaguliwa, kunaweza kuibua madai kutokana madhehebu mengine. Kwamba rais ni muislamu. Makamu wake ni muislamu. Rais wa Zanzibar na makamu wake wawili wote ni waislamu.

Waziri wa fedha, muislamu. Waziri wa ulinzi, naye ni muislamu. Waziri wa utumishi ni muislamu. Waziri wa afya, waziri wa mambo ya ndani na naibu wake, waziri wa uchukuzi na naibu wake, jaji mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), mkuu wa usalama wa taifa, wote ni waislamu.

Wengine wanaweza kufika mbali zaidi. Wakasema, ndani ya Benki Kuu (BoT), manaibu gavana wote watatu, ni waislamu. Bodi ya wakurugenzi yenye wajumbe 10, saba ni waislamu. Kwenye mifuko mitatu mikubwa ya hifadhi ya jamii, miwili inaongozwa na waislamu. Orodha ni ndefu.

Jambo muhimu ni iwapo walionufaika na walioshika madaraka, wamenufaika kwa sababu walikuwa na sifa, au ni kutokana na misimamo ya kimadhehebu?

Tuulizane: Ni waislamu wangapi wamenufaika kwa Kikwete kuwa rais? Kama ni wachache, ina maana amewasaliti? Kama amewasaliti, sasa wafanyeje? Mchezo huu ni mauti yetu sote!

0
No votes yet