Majeshi ya Gaddafi yafurusha waasi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version

VIKOSI vya jeshi linalomtii kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Ghaddafi vinapata mafanikio katika kulinda utawala wake kwa kurudisha miji na maeneo muhimu yaliyokuwa yametekwa na waasi hasa mashariki mwa nchi.

Walianza na Brega, mji wenye miundombinu mingi ya kusafirishia mafuta. Wanajeshi wa serikali walitwaa maeneo yaliyo karibu kilomita 30 nje ya mji huo, kabla ya kufanikiwa kuwatorosha waasi.

Wanajeshi wa maji, miguu na anga wanashirikiana kulinda maeneo yaliyotwaliwa na waasi ambapo mapema Jumatatu, televisheni ya taifa ya Libya iliripoti kutokea mashambulio makali ya angani yakilenga mji wa Ajdabiya unaokaliwa na watu wengi.

Mji huo ni mmojawapo wa maeneo yanayogawa miji inayoshikiliwa na serikali na kule ambako vikundi vya waasi wameweka makao makuu yao.

Said Ali Bouhilfaya, mhandisi anayeishi mjini Ajdabiya, amekaririwa akisema alikuwa akisikia milio ya mabomu kila baada ya dakika 20, saa kadhaa baada ya milio kusita kidogo wakati wa mchana.

Mabomu hayo yalisikika saa kadhaa baada ya msemaji wa waasi kusema ndege ya jeshi la serikali ilidondosha vipeperushi kwenye mitaa ya mji huo vikishawishi wananchi kutokomeza wanajeshi wanaompinga Kanali Ghaddafi.

"Wakatie huduma ya maji na chakula," alisema msemaji wa jeshi la serikali, Abdul-Bari Zwei.

Majeshi ya Gaddafi yamekuwa yakijitahidi kufukuza waasi na kurudisha maeneo mengi yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi yote yakiwa upande wa mashariki mwa nchi na ambayo ndiyo yenye raslimali kubwa zaidi ya mafuta.

Ingawa televisheni ya taifa imekuwa ikisemekana kutangaza taarifa zisizo sahihi za mafanikio ya jeshi la serikali, ilielezwa kwamba jeshi lake lilishambulia maeneo ya waasi na taarifa zikasema “waasi wamesafishwa kutoka maeneo hayo.”

Waasi wamekuwa wakipoteza maeneo mengi katika siku za karibuni katika hali ambayo ni pigo kubwa kwao katika kampeni ya kuelekea mji mkuu wa Tripoli baada ya kushikilia maeneo mengi ya mashariki.

Waasi wanashinikiza kufungwa kwa anga ya Libya ili kuzuia matumizi ya ndege za kivita. Jitihada zao zinakwenda sambamba na mikakati ya mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yakishawishi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha mpango huo.

Hata Umoja wa Nchi za Kiarabu uliridhia mpango huo katika mkutano uliofanyika Jumamosi ukishirikisha wanachama 22 wa umoja huo.

Wanadiplomasia wa kimagharibi walisema kulihitajika idhini kutoka nchi za kiarabu na Umoja wa Afrika.

Katika hali iliyoshangaza, wanachama wa Umoja wan chi za Kiarabu walisema serikali ya Libya imepoteza uhalali wa kuongoza na kutaka Umoja wa Mataifa uchukue wajibu wake kulinda raia.

Marekani na mataifa washirika wake wamekuwa wakifikiria sana matokeo ya uamuzi wa kuzuia anga ya Libya kutumiwa kijeshi wakati huu kwa kuhofia kughadhibisha Waarabu na ulimwengu wa Waislamu.

Nje ya maeneo ya mji wa Benghazi unaoshikiliwa na wapinzani, mpiga picha wa televisheni ya Al-Jazeera, Ali Hassan al-Jaber aliuawa baada ya kuvamiwa.

Mwandishi Baybah Wald Amhadi alisema gari la timu ya waandishi wa Al-Jazeera lilishambuliwa kwa risasi kutokea nyuma wakati wanarudi kazini kusini mwa mji huo.

Al-Jaber alipigwa risasi tatu mgongoni na ya nne ilimjeruhi sikioni mwandishi mwingine, alisema Amhadi.

"Hata maeneo yanayodhibitiwa na waasi hayako salama sana,” alisema na kuongeza kuwa wapo wafuasi wachache wa Kanali Ghaddafi.

Mapema, mkazi mmoja alikaririwa akisema kwamba kulikuwa na mapambano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi katika mji wa tatu kwa ukubwa wa Misrata, uliopo kilomita 200 kusini mashariki mwa Tripoli.

0
No votes yet