Maji Marefu sasa ataka ubunge


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version

NI saa tatu asubuhi ya 13 Agosti 2009, ninakutana na Steven Ngonyani, maarufu kama Profesa Majimarefu. Ni nje ya Hoteli ya Sunrise, mjini Korogwe, mkoani Tanga. Yupo kwenye harakati za kuhamasisha watu washiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, akiwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa jinsi ninavyomfahamu, tangu miaka ya mwanzo ya 1990, Profesa Maji Marefu ni mganga wa jadi. Kwa hiyo, napata tashwishwi. Nataka kufahamu zaidi kama amebadili fani. Ninamwomba tufanye mahojiano, anakubali.

Ninamuuliza imekuwaje awe kwenye siasa wakati, kwa miaka mingi nilikuwa namhafamu ni mtaalam wa mitishamba na mpunga maruhani.

Maji Marefu anasema, “Nilianza siasa mwaka 1995. Mpaka leo hii bado ninaendelea nayo. Kwa mara ya kwanza niliingia siasa nikiwa meneja wa kampeni za uchaguzi wa mbunge wa Korogwe.”

Anasema, “Niliingia kama meneja wa kampeni tu. Nilikuwea nawafanyia kampeni wagombea wengine wa CCM. Mwaka 2000 nikafanywa meneja wa kampeni tena. Mwaka 2002 nikagombea nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa. Nikashinda kwa kura nyingi.”

Maji Marefu anasema kuwa mwaka 2003 aligombea katika Baraza Kuu la Wazazi ngazi ya taifa. Akashinda. Akaendelea na nafasi hiyo hadi mwaka 2007, alishinda nafasi ya Katibu wa Uchumi, Mipango na Fedha wa Wilaya ya Korogwe.

Anasema: “Baadaye nikagombea nafasi ya mweka hazina wa CCM mkoa wa Tanga, nikawa mshindi. Bado nikawa mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Tanga.

“Lakini pia nilichaguliwa kuwa Katibu wa Malezi, Mazingira na Elimu wa Wazazi katika mkoa wa Tanga.”

Mwaka 2005 Maji Marefu aligombea ubunge. Kati ya watu 19 waliochuana naye akaibuka mshindi wa nne. Aliyeshinda kura za maoni wakati alikuwa ni Injinia Laus Omar Mhina.

Hivi karibuni aligombea nafasi katika Baraza la Taifa la Wazazi, kwenye nafasi tano za Tanzania Bara. Walikuwapo wajumbe 15, na walitakiwa wajumbe watano. Maji Marefu akawa miongoni mwa washindi watano.

Maji Marefu anazungumzia uprofesa wake na jinsi ulivyo tofauti na wasomi wengine ambao ni maprofesa.

“Mimi ni profesa katika fani yangu ya uganga wa jadi. Mimi sikupitia chuo kikuu na wala hatulingani na maprofesa wengine wa vyuo vikuu. Kuitwa Profesa Maji Marefu ni kutokana na vituko nilivyovifanya kutokana na mitishamba.

“Mambo ambayo nimeyafanya kwa kutumia mitishamba hakuna profesa yeyote wa ngazi ya chuo kikuu anaweza kuyafanya. Cheo hiki sikupatia hapa nchini. Nilipatia nje ya nchi wakati nikifanya vituko, ikiwa ni pamoja na kumbadilisha mtu jinsia yake na kumweka ya mtu mwingine.”

“Vituko vingine vipo. Kuna wakati watu wanamtangazia mtu kafa, anawekwa msukule, mimi ninamrudisha mafichoni, alikofichwa na wachawi. Kuna mambo mengi makubwa nimeyafanya,” anasema.

Maji Marefu anajivunia fani yake ya uganga wa jadi. Anasema kati ya watu waliobakia hivi sasa kwa Tanzania, ambao wanaweza kujigamba kama waganga halisi wa mitishamba na mambo mengine ya asili, ni yeye na Sheikh Yahya Hussein.

“Lakini wengine wote, tulioanza wote kazi hii wengine ni marehemu, wengine bahati mbaya wameokoka. Wale ambao tulitingisha kwa Tanzania nzima alikuwapo marehemu Dk. Misi, Sheikh Yahaya Hussein, Profesa Vulata, na mimi.

“Hao ndio tulikuwapo wakati huo. Tuliitingisha Tanzania hii. Lakini miaka hiyo mpaka leo kumetokea watu wengi sana wanaojidai wanafanya kazi hii. Siwezi kusema kwamba hii ni riziki, kwa hiyo mtu akiitafuta asipewe, lakini wengi wanatumia migongo yetu hivi sasa.

“Mimi ninakwambia kuna watu wanatumia jina langu sana kunadi biashara zao. Wapo Tanzania, Uganda na hata Kenya. Kuna watu wanajiita Maji Marefu. Wateja wakienda kuwachunguza kama ni yule tunayemjua anatoka Tanzania, wanakuta siyo wenyewe,” anasema.

Kuhusu uchaguzi unaokuja na mipango yake, anasema: “Mimi kama kiongozi wa kimkoa, mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Tanga na mweka hazina wa CCM mkoa wa Tanga, nitagombea ubunge tena mwaka ujao katika jimbo la Korogwe Vijijini.

“Ninayo nia, nguvu na uwezo wa kuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini, kwa sababu ninaamini wananchi wako na mimi. Nitashinda.”

Anasema kwamba ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge baada ya kushawishiwa na wanachi wa Korogwe Vijijini, kwamba awakilishe jimbo hilo bungeni.

“Wamenishawishi kuwa nigombee kwa kuwa wawakilishi wao mara baada ya kuchaguliwa hupotea. Hawaonekani jimboni. Hivyo wameamua kunipa nafasi hiyo mimi. Nina imani nao.”

Mbunge wa sasa wa Korogwe Vijijini ni Lause Omar Mhina, na kwa hiyo kama mbunge huyo ataamua kugombea tena basi atapambana na Profesa huyo.

Hata hivyo, Maji Marefu anasema kipindi hiki kazi yake kubwa imekuwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika mahojiano ya wiki iliyopita alisema kuwa angehakikisha anapita sehemu mbali mbali za Korogwe ili kuwahamasisha wananchi waichague CCM, ili wawe na wenyeviti wengi wa serikali za mitaa, ambao wanatoka kwenye chama hicho tawala.

Kwa miaka mingi Profesa Maji Marefu amekuwa akifanya shughuli zake za mitishamba katika nchi mbali mbali, akiwa na ofisi zake Nairobi, Korogwe na Dar es Salaam.

Lakini kutokana na uchaguzi wa serikali za mitaa na harakati nyingine za kisiasa, amekuwa akipatikana zaidi mkoani Tanga, hasa wilayani Korogwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: