Maji ya mto huu yana sumu


Albano Midelo's picture

Na Albano Midelo - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

MAISHA ya wakazi wa kata za Tingi na Liparamba katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, yako hatarini.

Wanakunywa maji ya mto Lunyere ambayo yamechanganyika na kemikali ya zebaki (mercury) inayotumiwa katika kusafisha dhahabu.

Tayari wataalam wametamka kuwa maji ya Lunyere “hayafai kwa matumizi ya binadamu na viumbe hai vingine.”

Takwimu zilizopatikana makao makuu ya kata hizi mbili zinaonyesha kuna watu wapatao 25,000 katika vijiji vyake 16 ambavyo vinatumia maji ya mto Lunyere.

Wachimbaji wadogo wa dhahabu huchenjulia madini yao katika mto Lunyere na wengine katika vijito vinavyoingia katika mto huo unaotiririkia mto mkubwa, Ruvuma.

Getruda Payovera, ambaye ni afisa wa maabara wa Wizara ya Maji, ofisi za kanda ya Songea, ana kile kinachoweza kuitwa “ujumbe kwa watu wote.”

Anasema zebaki ikinywewa kwenye maji au kuvutwa kwa pumzi, yaweza kuingia moja kwa moja kwenye damu na “...inakwenda kutua kwenye ubongo na kusababisha ubongo kusimama...”

Mwaka 2009 wataalam walifanya uchunguzi wa maji ya mto Lunyere, kutoka kitongoji cha Songeapori.

Uchunguzi ulifanywa na taasisi za Water Laboratory Unity na Chemical and Environmental Services za jijini Dar es Salaam.

Matokeo yake ambayo mwandishi ameonyeshwa, yalionyesha wazi kuwa maji ya mto Lunyere yana “kiwango kikubwa na cha kutisha” cha kemikali ya zebaki  inayoweza kuua binadamu na viumbehai vingine.

Kiwango cha kemikali ya zebaki kilichoelezwa kuwa “ni kikubwa na cha kutisha,” kimewekwa kwa vipimo vya kitaalam kuwa ni Hg/ug 0.02.

Maji salama kwa matumizi ya binadamu na viumbe vingine hai, ameeleza Payovera, yanapaswa kuwa na kiwango cha zebaki cha mg/n.m (mercury not mentioned), yenye maana kwamba hakuna kabisa kemikali ya zebaki katika maji.

Taasisi za uchunguzi zilibaini pia kuwa maji ya mto Lunyere yana kiwango kikubwa cha taka/tope ambacho kinavuka kiwango kinachokubalika kitaifa na hata cha  Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kiwango cha taka ambacho kinakubalika kitaifa kinaelezwa kitaalam kuwa ni etu 30; kiwango cha kimataifa ni  etu 5 – 25. Lakini maji ya Lunyere yana etu 1,141, jambo ambalo Payovera ameeleza kuwa “ni hatari sana.”

Uchimbaji dhahabu wa mtu mmojammoja ulianza mwaka 2004 katika kijiji cha Darpori na ndio mwanzo wa uchafuzi wa mto Lunyere kwa kemikali ya zebaki.

Uchafuzi umeenea katika vyanzo vya maji vilivyopo kwenye milima ya Sufuri A na Namba Tisa, nchini Msumbiji na katika kijiji cha Darpori kilichopo mpakani, upande wa Tanzania.  

Mto Lunyere hupita katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba inayounganisha Tanzania na Msumbiji, kisha kuungana na mto Ruvuma na kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi.

Mwandishi aliingia nchini Msumbiji hadi kijiji cha Mpapa kilichopo kata ya Lupilichi mkoa wa Lichinga na kuona vyanzo vya mto Lunyere katika vilima vya Sifuri A.

Katika vijiji vya Mpapa, Kitonga na Namba Tisa, wachimbaji wanasafishia vifaa vyao vya uchenjuaji dhahabu, vyenye kemikali, katika mto Lunyere.

Wilbert Mahundi, mwenyekiti wa Mfuko wa Wachimba Madini (Tanzania Mineral Mining Trust Fund – TMMTF), anasema  zebaki inaweza kusababisha kansa ya tumbo, ini, koo na ngozi.

Anasema zebaki ni nzito, haiyeyuki kwa urahisi na hugota chini ya vyanzo vya maji kama mto na kuvutia viumbehai kama samaki kuila.

Mtaalamu katika Shirika la Utafiti na Maendeleo Tanzania (TIRDO) anayehusika na mazao ya mizizi, Anselimo Moshi, anatahadharisha kuwa mazao ya mizizi, kama vile muhogo, yasilimwe karibu na maeneo ya machimbo ya madini au mabondeni ambako zebaki inatumika na kutiririkia kwenye maji.

Anasema zebaki hufyonzwa kwenye maji hayo na huweza kuwa na madhara yaleyale kama iliyonywewa kwenye maji au kuliwa kwenye samaki.

Uvundikaji mihogo kwenye maji ili kutengeneza makopa, anaeleza Moshi, haustahili kutumia maji yenye zebaki kwani huweza kubakiza sumu ndani ya chakula hicho.

Dk. Salla Paul, mkuu wa Chuo cha Maofisa Tabibu, Songea anataja baadhi ya dalili za aliyeathirika kwa zebaki kuwa ni pamoja na mwili kuwa na vidonda vya mara kwa mara, ukurutu, kupoteza kumbukumbu, macho kupoteza uwezo wa kuona na homa za matumbo.

Dalili nyingine ambazo zinatajwa pia na Dk. Joseph Mapunda wa chuo hicho, ni viganja vya mikono na wakati mwingine mwili mzima kuwa na rangi ya njano; mwili kukosa nguvu, kukosa hamu ya kula, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kutapika, maumivu ya kichwa ya mara kwa mara, kwikwi na kiu isiyoisha.

Kuhusu samaki, Wilbert Mahundi anasema mfumo wa chakula wa samaki hauna uwezo wa kuyeyusha zebaki; kwa hiyo kama anakunywa kemikali hiyo, basi sumu inaendelea kubaki mwilini mwake siku zote.

Amesema, mtu ambaye atakula samaki mwenye zebaki, anaweza kupata madhara kwa kuwa “utayarishaji samaki kwa ajili ya chakula, iwe kwa kupika au kuchoma, hauna uwezo wa kuondoa kabisa zebaki ndani ya samaki.”

Mbali na binadamu, maji yenye kemikali ya zebaki kutoka vijito vya Mkurusi na Mihomba na yanayoingia Lunyere, yanatumiwa na wanyama katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba na viumbe hai walioko katika mito hiyo.

Miongoni mwa wachimba dhahabu wanaochangia sumu katika mito Lunyere na Ruvuma, ni Watanzania wapatao 10,000 walio katika machimbo madogo ya dhahabu nchini Msumbiji.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Darpori kilichopo kata ya Tingi, wilayani Mbinga, Rafael Mapunda anasema tangu ameanza kutoa vibali vya kuruhusu Watanzania kuingia nchini Msumbiji kwa ajili ya kuchimba na kununua dhahabu, “takwimu zangu zinaonesha wamevuka wachimbaji wanaokaribia  10,000.”

Awali, wachimbaji wengi walikuwa katika kijiji cha Darpori chenye vitongoji vya Lunyere, Songeapori, Tanzania One na Njarambe. 

Serikali mkoani Ruvuma ilipotumia nguvu za sheria kuzuia matumizi ya zebaki, wananchi wengi wakakimbilia Msumbiji ambako hakuna katazo la uchimbaji kwenye vyanzo vya mito.

Shughuli zote za uuzaji na ununuzi wa madini kutoka Tanzania na Msumbiji, zinafanywa na raia wa nchi zote mbili katika kijiji cha Darpori.

Mwandishi aliwakuta wachimbaji, katika vikundi vya watatu au wanne, kwenye kitongoji cha Songeapori upande wa Tanzania, ambao wanaendelea kuchimba dhahabu na kutumia zebaki katika kuisafisha. Maji yenye zebaki yanatiririkia mtoni Lunyere. 

Uchafuzi wa mto Lunyere unafanywa na wananchi wa Tanzania na Msumbiji.

Ngwatura Ndunguru, afisa mkuu mstaafu katika wizara ya maliasili na utalii; na aliyewahi kuwa mbunge Mbinga Mashariki, anasema ufumbuzi wa uchafuzi wa Lunyere sharti ufanywe kwa kuhusisha nchi zote mbili.

Anapendekeza kila nchi kuchukua hatua za kuzuia uchafuzi, lakini anasema itabidi mikataba ya maji ya kimataifa itumike ili kupata ufumbuzi wa uchafuzi wa Lunyere na hatimaye mto Ruvuma ambamo yanatemwa maji yenye kemikali hatari.

0784 765917, albano.midelo@gmail.com
0
No votes yet