Majibu ya 'ushindi wa fedha' ni fedheha


editor's picture

Na editor - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TAARIFA zinazidi kufikia vyumba vya habari nchini kwamba harakati za wanasiasa kupita majimboni na kugawa fedha kwa wananchi zinashamiri.

Inaelezwa kwamba vitendo hivyo vinafanywa na wanasiasa wanaotaka kurudi bungeni pamoja na wale wanaotaka kuingia humo kwa mara ya kwanza.

Vitendo hivi vinashamiri katika kipindi tulichopo cha kuelekea uchaguzi mkuu. Baadaye mwaka huu, Watanzania watachagua rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge na madiwani na wenzao wanaoishi Zanzibar pia watachagua rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hata kwetu MwanaHALISI, haipiti wiki bila ya kupata watu waliopiga simu na kulalamikia vitendo hivi.

Tunapokea taarifa hizi kupitia njia ya ujumbe mfupi wa simu na pia kwa mpigaji kuongea. Utasikia mtu anasema, “Bwana Mhariri hebu tusaidie; kwani ni halali wanasiasa kupita majimboni muda huu na kutugawia fedha.”

Mpiga simu anayeishi Ubungo, Dar es Salaam, ambaye ni mtu mzima wa umri anasema ameona wanasiasa aliowaita “wakubwa wa serikalini” wakigawa fedha kwa wananchi mtaani kwao.

Anatuarifu kwamba wananchi wengi hupewa Sh. 5,000 kila mtu na wachache hupewa Sh. 10,000 kwa mtu. Sasa wananchi wanajiuliza, “hivi kampeni za uchaguzi zimeanza?”

Ukweli ni kwamba kampeni hazijaanza. Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, kampeni huanza rasmi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza wagombea iliowapitisha kugombea.

Utamaduni wa kutafuta kura kwa hongo haufai na hauwezi kupewa nafasi katika nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora.

Pale mgombea anaposhinda kwa nguvu ya fedha zake, ina maana tunajenga utaratibu kwamba Mtanzania asiyekuwa na fedha za kuhonga wapiga kura, hana haki ya kuchaguliwa.

Uongozi wa kununua siku zote huzaa viongozi wenye kiburi. Hawa hawawezi kuwajibika kwa wapiga kura wao. Kutoka kwao utumishi bora huwa ndoto. Bali wananchi watasaga lami na kuishia kulalamika hadi miaka mitano imalizike.

Tunapinga fedha kuamua nani wawe viongozi. Tunasihi wananchi wakipewa fedha wapokee kwa furaha lakini siku ya uchaguzi ikifika, wasizitazame badala yake wachague kiongozi wanayeamini atawatumikia kwa moyo.

Wakikubali kuendeshwa na fedha, basi wamejimaliza wenyewe maana viongozi wanaopata kura kwa fedha, huishia kudhihaki badala ya kutumikia wapiga kura. Hukacha kusikiliza watu bali siku zote majibu ya matumizi mabaya ya fedha ni fedheha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: