Makala ya Mtangazaji – Porokwa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 30 May 2011

Printer-friendly version
Daniel ole Porokwa

Kwa muda wa takribani wiki mbili sasa, vyombo vya habari vimeripoti maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Mh. Anthony Komu, kwamba Nape Nnauye alikuwa mwasisi wa Chama Cha Jamii (CCJ).

Madai haya yakathibitishwa na aliyewahi kuwa mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe ambaye alitaja watu kadhaa nikiwamo mimi, kuwa walishiriki au waanzilishi wa chama hicho ambacho hakikuwahi kufanikiwa kupata usajili wa kudumu.

Hivyo basi, nimewaita hapa leo hii, ili pamoja na mambo mengine, kueleza ukweli wa hiki ambacho kimeelezwa vizuri na Mheshimiwa Mpendazoe na kimenukuliwa vema na vyombo vya habari, hasa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI.

Nimeamua kufanya hivyo kwa misingi miwili mikuu. Kwanza, sisi kama viongozi ni sharti tuwaonyeshe wananchi wetu na wanachama wa chama chetu njia sahihi tunayotakiwa kupita na tuamini katika hiyo njia tunayoelekea.

Pili, mmoja wa msingi mkuu wa chama chetu, ni kusema ukweli, na kwamba uwongo na fitina ni mwiko kwa viongozi na wachama wa CCM.

Ni kweli niliwahi kuombwa kuwa mmoja wa wanachama waanzishi wa CCJ. Nilikutana mara kadhaa na Mh. Nape Nnauye, Mh. Dk. Harrison Mwakyembe na Mh. Fred Mpendazoe.

Aidha, nilikutana mara moja na Mh. Samwel Sitta baada ya Mh. Nape na Dk. Mwakyembe kunitajia kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa CCJ, nami kutaka uthibitisho wa hicho walichonieleza.

Naye Mh. Sitta alinieleza kuwa nilichoelezwa na Mh. Nape na Dk. Mwakyembe hakina chembe ya mashaka.

Katika mikutano zaidi ya mitano niliyofanya na Mh. Nape na Dk. Mwakyembe wenzangu walinieleza mpango wao wa kuanzisha chama cha siasa kuwa umelenga kuondokana na utawala wa kiimla wa CCM kwa hoja kuwa kilipofikia chama hicho hivi sasa, hakiwezi tena kuaminiwa kukabidhiwa madaraka ya kuongoza dola.

Walisema CCM hakiaminiki tena machoni mwa wananchi na kimepoteza mvuto mbele ya umma; yote haya ni kwa kuwa chama hiki kimekuwa kinaacha ile misingi ilivyoasisiwa na waasisi wake, kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Walinieleza, kihistoria Chama Cha Mapinduzi ni chama cha ukombozi na kilijipa kazi ya kupigania wanyonge, lakini kikafika mahali historia hiyo ikaporomoka kwa kuingia katika mikono ya watu wasiojali, wasiokuwa na maadili ya uongozi na labda wasiowaaminifu.

Wakati wote wa mazungumzo yetu, Mh. Nape na Dk. Mwakyembe walikuwa wakisisitiza umuhimu wa mimi kukubali kujiunga haraka na CCJ, ili kurahisisha upatikanaji wa usajili wa kudumu wa chama hiki, lengo likiwa CCJ kiweze kushiriki katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Hata hivyo, kila muda ulivyozidi kusogea, ndivyo nilivyopata kujua undani Mh. Mwakyembe na Mh. Nape wa kutaka kuanzisha chama chao cha siasa, kwamba kinachowasukuma katika mpango huo, ni matakwa binafsi ya kisiasa na hivyo nikaanza taratibu kuwa mbali na mkakati wao.

Nimeamua kuyasema haya baada ya kuwasikia Mh. Nape na Dk. Mwakyembe wakimkana Mh. Mpendazoe na kimsingi wakikana chama chao – CCJ.

Napenda kuwaambia Watanzania, kwamba CCJ ni chama kilichoanzishwa na kuasisiwa na viongozi hao wawili, pamoja na Mh. Sitta kama ambavyo Mpendazoe alivyoeleza.

Katika mpango huu, mimi niliahidiwa kusaidiwa kugombea ubunge katika jimbo la Monduli kupitia CCJ, huku Mh. Nape akiahidi kusimama katika jimbo la Ubungo.

Nimeyasema haya ili kuondoa unafiki unaojengeka ndani ya chama chetu na taifa kwa jumla, kwamba kuna kikundi cha watu wanaotaka kupotosha umma juu ya uanzishwaji wa CCJ na ujio wake ili umma uwapime na uamue juu ya watu hao.

Mimi kama kada wa CCM niliyefundishwa na kuaminishwa kwamba uongozi ni dhamana na ninayeamini katika misingi ile aliyotuachia Mwalimu Nyerere, nimeamua kuyasema haya ili ukweli ubaki ukweli katika historia ya nchi yetu.

Kuyumba kwa chama chetu na hata kufikia hatua ya kuanza kuporomoka kwa kupoteza nafasi mbalimbali kwa vyama vingine kwa wingi tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi hii, ni kwa sababu ya kuwa na viongozi wenye malengo na agenda zao binafsi, tofauti na zile za chama chetu.

Hii bila shaka inanipa sababu ya kuamini kwamba Bunge la Tisa kama mmoja wa mihimili muhimu wa dola, chini ya Mh. Samwel Sitta lilitumika vibaya kufanikisha agenda nyingine ya kuanzisha chama kingine badala ya CCM.

Ni vema Rais Jakaya Kikwete akajua kuwa ndani ya timu yake, kuna wachezaji ambao wako tayari kujifunga na kuinyima timu yao ushindi. Ni vema akaamua kuachana nao kwa maslahi yake na chama chetu.

Ni maoni yangu kwa dhati kabisa na rai yangu kwa viongozi wa chama, kwamba ni wakati mwafaka watu kama hawa wawajibike au wawajibishwe kwa matendo yao.

Baada ya mimi kushutukia na kutokuwa na imani na minendo ya waasisi wa CCJ na hivyo kujiondoa, nilipata taarifa kuwa baada ya kujiridhisha kuwa chama chao hakitasajiliwa na kuwahi uchaguzi wa 2010, waliamua kufanya mazungumzo na viongozi wa CHADEMA na kukubaliana kuwa wote kwa pamoja watajiondoa CCM na kujiunga na CHADEMA ili kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.

Kwa ushahidi ninaoutoa, ninawachukua hawa niliowataja kuwa si wasaliti kwangu tu, bali hata kwa chama chenyewe. Nisingeshutuka mapema yangenipata yaliyompata Mpendazoe. Ninampa pole sana ndugu yangu Fred Mpendazoe.

Na hili la Mpendazoe ambaye alikuwa mbunge, akaacha mishahara kadhaa na mafao yake kwa makubaliano ya kazi ya pamoja ambayo nilishirikishwa katika hatua za awali na mwisho wake wakamtosa na sasa wanamkana hadharani, ni moja ya sababu iliyonisukuma sana kutoa ushuhuda huu.

Daniel ole Porokwa,
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: