Makamba ana ajenda gani?


Abel Ndekirwa's picture

Na Abel Ndekirwa - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Mtazamo
YUSUF Makamba

YUSUPH Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ana ajenda gani dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta?

Wiki mbili zilizopita, Makamba akiwa katika rangi mbili mithili ya kinyonga alikwenda nyumbani kwa Sitta na kushusha sifa ambazo hata Sitta mwenyewe alipigwa na butwaa.

Kwamba Makamba yuleyule aliyetangaza mara baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa atadhibitiwa, ndiye aliyekwenda Urambo na kutaka wananchi kumrejesha tena Sitta bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka kesho.

Kauli Makamba aliyekuwa Urambo ni tofauti sana na aliyekuwa Dar es Salaam alipoulizwa kisa cha NEC kumkaba koo Sitta.

Ingawa Makamba amekuwa akijificha chini ya kichaka kwamba anapambana na ufisadi, lakini yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono ufisadi.

Ndiyo maana baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo ilitoka na maamuzi yaliyozua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi juu ya wale wanaopambana na ufisadi, Makamba alitamba kwamba NEC na CCM ina ubavu wa kmdhibiti Sitta.

Ndani ya NEC, Sitta aliandamwa kwa kuambiwa kuwa badala ya kuwa refa wa kuendesha Bunge, yeye amekuwa mchezaji akisaidia wabunge wachache waliojipachika wajibu wa kupambana na ufisadi; wakati mwingine akishiriki moja kwa moja kwenye mijadala inayojeruhi serikali.

Hadi sasa kuna kitu kimoja ambacho hakijawekwa wazi. Je, Makamba ameibuka na sura au rangi hii mpya kwa Sitta kwa sababu ya kutambua kukengeuka kwake na NEC, au ni mbinu ya kulizubaisha kundi linalopambana na ufisadi?

Jibu linaweza kuwa hili: Kwamba Makamba ana sura nyingi anazozitumia kwa mambo tofauti. Makamba anataka kudanganya ulimwengu kwamba Sitta hakusakamwa; ndani ya NEC hakukuwa na dhoruba. Hili hakufanikiwa.

Ni wazi kwamba Makamba na wenzake waliozungumza kwa kejeli na ubabe juu ya nguvu za Bunge hawakujua kuwa walikuwa wanavuruga nchi.

Ndiyo maana haikushangaza kuona baadhi ya balozi nchini zikitaka kujua kwa yakini nini hasa nini kilitokea NEC?

Je, NEC ilikuwa imelinyamazisha Bunge ili wafadhili wajue kwamba sasa nini wajibu wa wabunge kuisimamia serikali hasa kwenye eneo la matumizi ya fedha.

Kwa kutambua hivyo wangejua kwamba fedha zao sasa hazina msimamizi na hivyo kufikiria upya kama zitawafikia walengwa ambao ni wananchi au zitaishia kwa viongozi walioamua kuling'oa Bunge meno.

Katika kujenga picha kwamba Bunge bado lina nguvu zake, Makamba anajipitisha kwa Sitta kuonyesha kwamba "kundi" linalokwazwa na vita ya dhidi ya ufisadi halina ugomvi na vita hiyo, kimsingi wako pamoja katika kupambana na kulipa Bunge nguvu ya kung'ata zaidi.

Makamba ametembelea jimbo la Sitta kutaka umma umuone kwenye sura na rangi tofauti na alivyo moyoni juu ya mwelekeo mzima wa vita dhidi ya ufisadi.

Kwa maana hiyo, watu wanapaswa kujua, akiwamo Sitta, kwamba anachofanya Makamba ni kufunika kombe ili mwanaharamu apite, lakini kisasi cha watu wasiotaka vita ya ufisadi iendelee kamwe hakiwezi kudaiwa kimekwisha kwa hatua hii ya Makamba. Bado kipo kinachemka na kinatafuta njia ya kulipuka na kubabua wapinzani wao.

Kwa hali hii basi, ziara ya Makamba kwenye jimbo la Sitta haiwezi kuruhusiwa kupumbaza fikra huru na zinazotaka mabadiliko ya kweli.

Makamba huyu alithibitisha muda mrefu kwa maneno na matendo amejiegemeza kwa watu wanaohisiwa kuwamo katika kundi la mafisadi.

Ni kwa maana hiyo rangi za Makamba zinapaswa kuogopwa na kuchukuliwa kwa tahadhari kali, hizi ni mbinu za kuzubaisha mpinzani katika mapambano ili kumpa pigo la kushutukiza, kwa hali hii kiongozi huyo ni lazima atazamwe kwa macho makali na kuchunguzwa nyendo zake zote.

Kwa ninavyomfahamu Makamba, atapayuka tu kusema lililo moyoni mwake muda si mrefu ujao. Tusubiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: