Makamba apunguza kura CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly version

YUSUF Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anatuhumiwa kupunguza kura za Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Tuhuma hizo zinatokana na malalamiko kwamba Makamba anabeba baadhi ya wagombea ubunge na udiwani na kutokomeza wengine asiowataka.

Kwa mfano, Makamba hajachukua hatua yoyote katika minyukano kati ya Meya wa Dar es Salaam, Adam Kimbisa na mbunge wa Afrika Mashariki, Didas Masaburi.

Inadaiwa Masaburi anataka kumgoa Kimbisa kutoka udiwani wa Kivukoni kwa kutumia ofisi ya CCM ya mkoa wa Dar es Salaam. Malalamiko haya yako ofisini kwa Makamba na yeye hajachukua hatua.

Aidha, katika tawi la Magogoni, Kata ya Kivukoni, katibu wa tawi ameamriwa kukabidhi rejesta ya wanachama wa CCM kwa katibu wa Kata kwa kile kinachodaiwa kutaka kuingiza wanachama wapya watakaombeba mmoja wa wagombea.

Rejesta zilizokabidhiwa ni Na. 0002614 na 0002621 za wanachama 350. Rejesta zilipokelewa na Said Mwanga, Katibu wa Kata. Suala hili linadaiwa pia kuwa mezani kwa Makamba lakini hajalishughulikia.

Katika jimbo jipya la Segerea, ambako mgombea mtarajiwa Makongoro Mahanga, makatibu wa matawi watatu wamesimamishwa uongozi kwa miezi tisa kwa madai ya kupendelea Glorious Luoga anayetaka kuwania jimbo hilo.

Taarifa hizi ziko mezani kwa Makamba lakini bado hajachukua hatua.
Mgogoro mwingine katika jimbo la Segerea ni Mahanga kumwandikia katibu wa CCM wilaya barua Kumb. Na. UK/CCM/10/5 ya tarehe 17 Mei 2010.

Barua inamwelekeza katibu wa wilaya kumwonya mwenyekiti wa CCM tawi la Segerea, Abias Malifedha na Luoga kwa kile Mahanga aliita “kuchafua chama.”

Hata baada ya Luoga kumwandikia Makamba akilalamikia hatua ya Mahanga, katibu mkuu huyo hajachukua hatua.

Vyanzo vya taarifa vinasema tayari katibu wa tawi la Magogoni ametishiwa kubambikiwa kesi, kuhamishwa au kufukuzwa kazi, kutokana na msimamo wake wa kukatalia wafuasi wa Masaburi kuingiza “wanachama feki.”

Madai dhidi ya Makamba yamekuja wakati ofisi yake ikidaiwa kupokea mamia ya malalamiko kutoka kwa wanachama wake wanaodai “kuchezewa rafu” katika mchakato wa kutafuta wagombea.

Kwa mujibu wa waraka kutoka kwa wana-CCM, wakiwamo wabunge, vitendo vya Makamba ni hatari kwa chama tawala katika mwaka huu wa uchaguzi.

Waraka huo wa kurasa tano ambao umesainiwa na wanachama (majina tunayo, umeweka hadharani madai makuu tisa dhidi ya kada huyo mkongwe wa CCM.

Madai hayo ni kutiliwa shaka kwa uwezo wake wa kusimamia maadili ndani ya chama, uwezo mdogo kulinganisha na mamlaka makubwa ya ukatibu mkuu wa CCM na kushindwa kujenga umoja ndani ya sekretarieti ya chama hicho.

Waraka umedai pia kwamba Makamba ni dhaifu kiuongozi na ndiyo maana migogoro baina ya wana-CCM imekuwa jambo lisilokwisha.

Wanachama hao wa CCM wamedai pia kuwa si siri tena kwamba Makamba yuko karibu na kundi la wanachama wa chama hicho wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi.

“Kwa mfano, zimekuwapo tuhuma kwamba makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya wamekuwa wakiwaunga mkono wagombea wanaoungwa mkono na kundi la watuhumiwa wa ufisaidi; lakini Makamba hajachukua hatua yoyote,” unaeleza waraka huo.

Migogoro ya aina hii, iliyozagaa nchi nzima na ambayo haitafutiwi ufumbuzi wa haraka, ina uwezekano wa kupunguza, tena kwa kiwango kikubwa, kura za Kikwete.

Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na Makamba kuzungumzia waraka huu hazikuzaa matunda kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

Hata hivyo, akizungumzia malalamiko miongoni mwa wana-CCM, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa, alisema tayari chama kimeanza kuyashughulikia.

“Sisi kama chama kwa kweli tumeanza kuyashughulikia malalamiko hayo na si kazi rahisi kama baadhi ya watu wanavyotaka ionekane.

“Kwa mfano, tukipata malalamiko ya mtu ni lazima pia tumtafute yule anayelalamikiwa kwa ajili ya natural justice (kumtendea haki). Hatuwezi kuchukua hatua kwa kusikiliza upande mmoja tu.

“Lakini pia kuna mambo mengine ambayo tumeamua tuache sheria ifuate mkondo wake. Kuna baadhi ya malalamiko tumeyapeleka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili wayafanyie uchunguzi na kufanya maamuzi yao kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Hata hivyo, Msekwa alisema chama kitahahakisha malalamiko yote yaliyofikishwa kwao yanapatiwa ufumbuzi kufikia mwanzoni mwa Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, kura ya maoni itapigwa na wanachama mwishoni mwa mwezi ujao.

Matokeo hayo yatapitiwa na vikao vya juu vya CCM na uamuzi wa mwisho utatolewa wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliopangwa kufanyika Agosti 16 mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: