Makamba atuhumiwa kuchochea migogoro CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 March 2009

Printer-friendly version
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba

Kazi ya Kamati ya Bunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushughulikia malalamiko na matamshi ya mbunge wa Mvomelo, mkoani Morogoro, Suleman Sadiq, sasa imekuwa ndogo.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, 10 Februari 2009, mjini Dodoma, Sadig alimtuhumu Mwekahazina wa chama hicho, Amos Makala akisema “anatumia vibaya fedha za chama.”

Hata hivyo, wiki moja baada ya Sadiq kumtuhumu Makala, ameibuka tena na kukana kwamba hajawahi kutoa tuhuma hizo, jambo ambalo limezidi kumuingiza katika matatizo na chama chake.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Sadiq kukana kauli yake aliyoitoa Dodoma umetokana na maelekezo ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba.

“Ndiyo ukiangalia utetezi wa Sadiq mara moja utabaini kwamba kuna mkono wa Makamba katika jambo hili,” alisema kiongozi mmoja wa CCM.

Aliongeza, “ Awali Sadiq aliwasilisha malalamiko yake, lakini baada ya Makala kumuandikia Makamba, ndipo Sadiq akajitokeza na kubadilisha kile alichokidai awali,” alisema kiongozi mmoja wa CCM kwa sharti la kutotajwa jina.

Katika barua yake ya 14 Februari 2009 aliyoituma kwa Makamba, Sadiq amekana kwamba ametoa tuhuma hizo dhidi ya Makala.

Hata hivyo, MwanaHALISI linaushahidi kwamba Sadiq alimlalamikia Makala, na kwamba Makala tayari amechukua hatua ya kujibu tuhuma za Sadiq.

Inaelezwa kwamba katika mkutano huo Sadig alimtuhumu Makala kuwa amemgawa na wananchi wa jimbo lake, na kwamba tayari anafanya kampeni za kutaka kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Aidha, Sadiq alimtuhumu Makala kuwa anatumia vibaya wazifa wake wa muweka Hazina kwa kusema ametumwa na CCM kugombea ubunge wa jimbo hilo na tayari ametoa misaada ya zaidi ya Sh. 180 milioni.

Tuhuma nyingine ni Makala kuanzisha kombe la mpira wa miguu linaloutwa Makala CUP katika jimbo lake. Anamtuhumu pia kumjengea uhasama kwa mkuu wa wilaya na viongozi wengine wa chama na serikali.

Katika barua yake ya utetezi, Sadiq anakana baadhi ya tuhuma ikiwamo Makala kutumia vibaya fedha za chama. Hata hivyo, Sadiq anakiri kwamba amewasilisha baadhi ya malalamiko katika kikao hicho. Hayajataji!

Katika kile kinachoweza kuitwa “kupanga kujiokoa,” Sadiq anatupia lawama baadhi ya wabunge akisema wameanza kupungikiwa na maadili ya uongozi kwa kutoa nje ya vikao mambo ya ndani ya chama.”

Anasema, “…Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya sisi wanaCCM tumeanza kupungikiwa maadili ya uongozi kwa kutoa nje siri ya vikao vya chama kama ilivyotokea.”

Aidha, mbunge Sadiq anakana kuandikiwa barua ya onyo na kumtaka Makala kuacha kile alichoita “kusema uwongo.”

“Katibu Mkuu, naomba Makala aache kusema uwongo. Mimi sina barua ya onyo kama anavyoeleza kwenye gazeti la Majira. Vinginevyo athibitishe,” anasisitiza.

Gazeti liliwasiliana na Makala kutaka kufahamu mkanganyiko wa kauli za Sadiq. Aligoma kuingia kwa undani, badala yake alijibu kwa kifupi sana.

“Sina cha kusema. Mimi si msemaji wa chama. Kama kuna kitu, wasiliana na wahusika,” alisema Makala na kusisitiza kam kuna kitu chochote wa kuulizwa ni Sadiq au Makamba.

Naye Makamba hakupatikana kuzungumzia suala hilo. Simu yake ya mkononi ilipopigwa msaidizi wake alimtaka mwandishi kuwasiliana kwa simu yake nyingine ambayo nayo hadi tunakwenda mitamboni haikupatikana.

MwanaHALISI lilipowasilina na Katibu wa CCM mkoani Morogoro, Mary Chitanda kuhusiana na madai kwamba Sadiq aliwahi kuonywa kusambaza taarifa za uwongo na uzushi dhidi ya Makala, aligoma kuzungumza kwa kusema alikuwa katika msiba.

Alisema, “Niko kwenye msiba. Siwezi kuzungumza hilo tafadhari…”. Alipoombwa atoke pembeni kidogo ili aweze kujibu swali juu ya maandishi ya Sadiq, Chitanda alisema, “. Samahani… niko kanisani.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo katika ofisi ya CCM mkoani Morogoro, 20 Aprili 2007, Chitanda alimuandikia barua Sadiq yenye Kumb. Na. CCM/MMG/C/A.60/48/C/106 inayoelekeza kwa Sadiq kuacha kuendeleza makundi ndani ya chama hicho.

“Kamati ya Siasa ya H/Kuu ya Mkoa (Halmashauri Kuu ya mkoa), iliyokutana tarehe 29 Machi 2007 pamoja na mmbo mengine… imeridhika na wewe mwenyewe kwa wepesi wa kukiri mapungufu yaliojitokeza dhidi yako. Hivyo nimeagizwa nikuandikie barua ya kukuelezea mapugufu hayo ili uchukue hatua za kijirekebisha kama ulivyoahidi.”

Barua inamuonya Sadiq kutokuwa mwenepesi wa kusikiliza maneno/majungu kutoka kwa wapambe bila kuchuja. Kwa kufanya hivyo, anaendeleza malumbano na mifarakano isiyokuwa na msingi.

Mbunge mmoja mwandamizi wa CCM ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu mvutano wa Sadiq na Makala amesema hatua ya Sadiq kukana kile alichokisema kinaweza kumuweka mahali pabaya zaidi, kuliko angeamua kufuta kauli yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: