Makamba: Hakuna atakayebaki salama


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KUNA msemo wa kiswahili usemao, “Aliye katika nyumba ya kioo hatakiwi kurusha mawe nje.”

Nimeukumbuka msemo huu baada ya kuona mashambulizi ya kibinafsi yanayoendeshwa dhidi ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Kwanza vilianza vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja ambao ama wametumwa ama wanauhusiano wa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake.

Haikushia hapo. Mtendaji mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, naye hakubaki nyuma. Akajitumbukiza katika “siasa za majitaka.”

Akamtuhumu Dk. Slaa, kwamba hafai kuwa rais kwa vile amekiuka kiapo chake cha ndoa dhidi ya aliyekuwa mkewe, Rose Kamili Slaa.

Kwamba kwa vile Dk. Slaa alimuacha mkewe, basi hana sifa za kuwa rais. Je, ni kweli? Tujadili:

Makamba anasahau kuwa miaka miwili baada ya Nelson Mandela kuwa rais wa Afrika Kusini aliachana na mkewe wa kwanza, Winnie-Madikizela Mandela. Mandela na Winnie walitalakiana Machi 1996, miaka miwili baada ya Mandela kuingia ikulu.

Winnie alikuwa ni zaidi ya mke kwa Mandela. Katika vita ya ukombozi, mwanamama huyu shupavu, alisimama bega kwa bega na mumewe na chama chake cha Africa National Congress (ANC) katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukombozi wa nchi yake.

Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, Mandela alitumikia wananchi bila kuwa na mke. Hiyo haikumzuia kufanyakazi za urais.

Mwaka 1998 akiwa anatimiza miaka 80, Mandela alifunga ndoa na Graca Machel, mke wa mmoja wa marafiki zake wa karibu, rais wa zamani wa Msumbiji, Samora Machel, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika vita ya ukombozi. Samora alifariki katika anga ya Afrika Kusini.

Naye, Daniel arap Moi, aliachana na mkewe Lena Moi, kabla hajawa rais wa Kenya. Miaka mitatu baadaye akachaguliwa kuwa rais wa Kenya. Amekaa ikulu kwa miaka 20 bila kuwa na mke rasmi.

Je, Mandela ni kiongozi mbaya kwa vile aliachana na mkewe na hakustahili kuendelea na urais?

Ni Mandela huyu, ambaye ulimwengu utamtambua kwa msimamo wake wa kuunganisha nchi yake iliyokuwa imepasuliwa vipandevipande na siasa za ubaguzi wa rangi?

Je, wananchi wa Arika Kusini walistahili kutomchagua Mandela kwa sababu aliachana na mkewe?

Je, Moi hakustahili kuwa rais wa Kenya kwa sababu aliachana na mkewe na kukaa ikulu kwa miaka 20 bila mke?

Si hivyo tu: Mara kadhaa vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti matatizo ya ndoa ya rais Mwai Kibaki na mkewe Lucy Kibaki; yamekuwa na matatizo.

Imeripotiwa hata Kibaki kuwa na mke mwingine. Naye Lucy mara kadhaa amefanya vurugu hadharani. Amepiga hata waandishi wa habari.

Lakini ni Kibaki huyuhuyu aliyeandika historia katika taifa lake baada ya kusimamia mchakato wa katiba mpya. Matatizo yake ya ndoa yamebaki kuwa yake binafsi na urais umebaki wa wananchi.

Aliyekuwa rais wa Marekani, Bill Clinton alikubwa na kashfa ya uhusiano wa kimapenzi na Monica Lewinsky wakati akiwa madarakani.

Alipokabwa koo na wapinzani wake kutaka aachie madaraka, wananchi wa Marekani walikataa. Walisema, “Mapenzi ni kitu kingine na uongozi ni jambo jingine.”

Clinton ameondoka madarakani baada ya kukamilisha kipindi chake chote cha miaka minane ya urais. Ameondoka akiwa na historia ya kuicha Marekani na heshima duniani.

Walichotaka wananchi wa Marekani ni rais anayeongeza ajira na kukuza uchumi. Anayefanya kila raia wa dunia kukimbilia Marekani kutafuta maisha. Penzi lake na Monica lilibaki suala binafsi.

Mwanamapinduzi maarufu, Ernesto Che Guevara, naye hakubaki salama. Hakuwa na mahusiano imara katika ndoa yake.

Hata hivyo, nani awezaye kusema kwamba Che hakuwa mwanamapinduzi halisi? Nani aweza kusema hakujitolea damu yake kwa ajili ya ukombozi?

Lakini Makamba na chama chake wanajifanya hawayajui haya. Wamejiingiza kwenye siasa ambazo haziwezi kutatua shida za wananchi.

Mtu yeyote anayefanya siasa za namna hii ni lazima ajue athari zake. Kama naye ana mgombea, ni vema akaangalia iwapo mgombea wake hana doa katika maisha yake binafsi.

Kwa mfano, kabla ya Makamba kuanza kurusha mawe kwa Dk. Slaa, lazima kwanza amuangalie mgombea wake, Jakaya Kikwete. Je, ni msafi kiasi gani katika maisha yake binafsi?

Hili ni muhimu kwa sababu, iwapo wapinzani wa CCM watajibu mapigo Makamba anaweza kujikuta anafunika sura kama nyani kwa aibu.

Ningeamini kama CCM iko salama kama mgombea wake wa urais, angekuwa malaika Gabriel.

Lakini, kwa kuwa mgombea wake, ni mwanadamu mwenye jina la Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete, naamini hizi si siasa salama kwake na chama chake.

Nijuavyo mimi, Kikwete ni mwanadamu kama tulivyo sisi wengine sote. Ana mazuri yake na mabaya yake. Na ushahidi kwamba naye ni mwanadamu mwenzetu upo.

Kwenye misiba analia kama tuliavyo sisi. Kwenye michezo hufurahi na kuhuzunika, tunaposhinda na kufungwa.

Ndiyo maana tayari minong’ono imeanza kuibuka ikumhusisha rais. Kama taarifa hizo ni za kweli na Dk. Slaa na chama chake wakaamua kuzitumia majukwani, hakika, taifa nchi haitakalika.

Binafsi, naamini kwamba iwapo viongozi wa CCM wataendelea na siasa hizi za majitaka, wao na chama chao, ndiyo watakaopoteza zaidi kuliko upinzani.

Ni kwa sababu, CCM imekaa madarakani kwa muda mrefu. Maisha ya viongozi wake yanafahamika na kujulikana na kila mmoja.

Wanafahamika wanakwenda vijiwe gani, wanacheza muziki wapi na wana uhusiano na nani.

Baadhi ya wana CCM wanaurafiki wa karibu na viongozi wa upinzani. Wanakula na kunywa pamoja. Hata kile kinachoitwa, “mabomu ya Slaa” mengi yanatoka ndani ya chama chenyewe na serikali yake.

Katika mazingira haya, nani atalaumu Slaa ikiwa CCM imejiruhusu yenyewe kujiingiza kwenye “siasa za maji taka?”

Katika historia ya dunia, watawala wengi wamekuwa na matatizo katika maisha yao binafsi hususani yale ya kimapenzi. Hata Makamba inawezekana akawa na matatizo katika ndoa yake na maisha yake binfasi nje ya ndoa.

Lakini ukweli unabaki palepale, kwamba matatizo hayo hayawezi kuzuia kazi nzuri kufanyika.

Jambo la msingi hapa ni kwamba Watanzania wanataka kupata fursa ya kuchagua kiongozi wa kuwatumikia na kuwapa wanachokitaka.

Wanataka sera zitakazowatoa katika minyororo ya kuchangia gharama za matibabu, karo za shule, maji na umeme. Wataka mtu ambaye anachokisema ndicho akitendacho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: