Makamba hatihati


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 September 2008

Printer-friendly version
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba amevutwa shati na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

Ni kutokana na sakata la Nape Nnauye, mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Makamba alishiriki kikao cha Baraza Kuu mkoani Dodoma ambapo alishinikiza wajumbe kumvua Nape uwanachama, kwa hoja kwamba “Nape ametukana viongozi wake.”

Baadaye Makamba aliwambia waandishi wa habari kwamba Nape hawezi kukataa rufaa, duniani wala akhera.

Hata hivyo, siku mbili baadaye Kikwete alikiambia kikao cha NEC kwamba Nape anaendelea na nyadhifa zake zote na kwamba yaliyotokea UV-CCM aweza kuyakatia rufaa katika chama.

Bali hatua ya Makamba ya kwenda kusimamia maamuzi batili katika UV-CCM, inadhihirisha jinsi kiongozi huyo alivyopoteza mwelekeo.

Lakini kwa wanaomfahamu hawakushangazwa na hatua yake hiyo. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na tuhuma nyingi dhidi ya Makamba.

Wengine bado wanakumbuka kauli zao za awali pale alipopewa kazi hii kwamba viatu vya ukatibu mkuu havikuwa vinamtosha wakati huo; na havijamtosha mpaka sasa.

Hapo alipojifikisha Makamba panahitaji ujasiri wa aina ya pekee ili abaki katika kiti chake.

Makamba anakabiliwa na tuhuma za kushabikia mkataba wa hovyo wa ujenzi wa kitega uchumi cha Umoja wa Vijana (UV-CCM).

Akiwa mtendaji mkuu wa CCM, ametetea mkataba huo kwa kusema Baraza la Wadhamini chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa “lilifanya kazi zake kupitiliza.”

Lakini Kamati Kuu (CC) ya CCM imetupa hoja za Makamba.  Imesema mkataba aliokuwa anaupigia chapuo, una mapungufu mengi. Hata pale ulipobadilishwa bado haukukidhi mahitaji.

Ni mapungufu hayo yaliyosababisha wajumbe kukubaliana na hoja ya  kuundwa tume kuuchunguza mkataba huo.

Makamba hakujali kelele na vilio vya wajumbe kadhaa wa Baraza la Wadhamini, akina Yusuf Mohammed, William Lukuvi, Dk. Mary Nagu na Willison Masilingi, kwamba hawajawahi kupitisha mkataba ambao  Lowassa anadai aliusaini pamoja nao.

Masilingi alifika mbali zaidi na kuita mkataba huo kuwa ni wa “hovyo.” Si hivyo tu, Makamba hakusikiliza hata kilio cha wenyeviti 15 wa mikoa wa UV-CM ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu ambao walikana kupitisha mkataba huo.

Kama hiyo haitoshi, Makamba hakumsikiliza hata mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete ambaye naye alisema mkataba huo haukuwa na maslahi kwa UV-CCM.

Makamba amepoteza sifa ya kuwa mtendaji mkuu wa CCM kutokana na kutetea watuhumiwa wa ufisadi.

Hatua hiyo ya Makamba tayari imezusha msuguano kati yake na wanachama wengine wanaotaka mafisadi waondolewe katika chama.

Miongoni mwa tuhuma mpya za hivi sasa ni ile iliyotolewa bungeni na mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Halima Mdee ambaye alimtuhumu Makamba kumlinda Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa.

Makamba anatuhumiwa na wabunge wa chama hicho kuwa anaendesha siasa za kinafiki kwa kupandikiza chuki na kuendeleza makundi miongoni mwao.

Tuhuma za wabunge hao zilikuwa ni moja ya ajenda ya mkutano kati ya wajumbe wa NEC na wabunge uliofanyika Juni mwaka huu, mjini Dodoma.

Taarifa kutoka duru za bunge zinasema ajenda ya kumshitaki Makamba kwa NEC ilizimwa na Makamba mwenyewe baada ya taarifa hiyo kuvuja na kumfikia.

Ni katika kikao cha wabunge na wajumbe wa NEC, Makamba alitetea hadharani watuhumiwa wa ufisadi wanaotumia majukwaa ya chama kujisafisha.

Ajenda ya kumkataa Makamba iliibuliwa tena majuzi katika kikao cha Kamati ya uongozi ya Wabunge wa CCM.

Ndani ya kikao hicho, wabunge walimchachamalia mwenyekiti wao, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kumtaka kufikisha ujumbe kwa rais.

Makamba anatuhumiwa na baadhi ya viongozi wenzake, wakiwamo wajumbe wa CC, kwamba anachochoea kundi moja la wanachama walioshindwa katika uchaguzi ndani ya chama kupinga matokeo yaliyowapa ushindi wagombea wengine.

Mkakati wa Makamba katika suala hili ni kufyeka wanachama ambao hawakuwa “wanamtandao,” anasema mwanachama mmoja wa CCM ambaye hakutaka kutajwa jina.

Baadhi ya wanachama ambao uchaguzi wao unadaiwa kupingwa kwa ufadhili wa Makamba ni pamoja na Dk. Abdallah Kigoda aliyegombea ujumbe wa NEC kupitia mkoa wa Tanga.

Mwingine ambaye Makamba anatuhumiwa kufadhili na kuhujumu kisiasa, ni Profesa Mark Mwandosya, ambaye katika uchaguzi ndani ya chama aligombea ujumbe wa NEC kupitia mkoa wa Mbeya.

Mwandosya alimshinda kwa mbali Tom Mwang’onda, mbunge wa kuteuliwa na mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Colnel Apson.

Mjumbe mwingine ambaye Makamba anatuhumiwa kumsakama ni mwanasiasa mkongwe, John Malecela.

Makamba anadaiwa kumhusisha Malecela na kushindwa kwa mwanachama wa kundi la mtandao aliyesimikwa na Edward Lowassa, Fulgence Saria.

Malecela, Profesa Mwandosya na Dk. Kigoda ni miongoni mwa wanachama 11 wa CCM waliogombea urais mwaka 2005 na kushindwa na rais Kikwete.

Ni katika mahusiano haya, uwezekano wa Makamba kusalimika katika nafasi yake unakuwa mdogo mno. Kuendelea kwake kuwepo madarakani kutadhoofisha zaidi chama na kukatisha tamaa wanachama na viongozi wengi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: