Makamba kapata wapi uwezo kunyamazisha wananchi?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, amenaswa kwenye ndoana za kampuni ya kufua umeme ya Symbion Power LLC.

Ni zaidi ya miezi sita sasa tangu Makamba ajipe sura ya “ofisa uhusiano” wa makampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company (LLC), Dowans Holdings SA, Dowans Tanzania Limited (DHL) na sasa Symbion Power.

Aidha, hii ni mara ya pili tangu Makamba achaguliwe kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kupiga marufuku wanasiasa kuingilia mradi wa kuzalisha umeme wa Richmond na dada yake Dowans.

Sasa Makamba amewaambia waandishi wa habari Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, kwamba kamati yake haitaruhusu wanasiasa kuingilia mradi wa umeme wa kampuni ya Symbion Power, kwa kile alichodai “siasa ndizo zimelifikisha taifa katika giza.”

Alisema tayari wamiliki wa kampuni hiyo wamelieleza hilo katika mazungumzo yao na TANESCO.

Kauli ya Makamba ilikuja siku moja baada ya Paul Hinks, aliyejitambulisha kuwa meneja mtendaji wa Symbion Power kueleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kwamba kampuni yake tayari imenunua mitambo ya kampuni ya Dowans.

Kwanza, kabla ya Makamba kutaka wanasiasa kutoingilia mkataba kati ya Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) na “kampuni yake” – Symbion Power LLC – ni sharti afahamu kuwa kampuni hiyo imenunua mitambo ya kampuni ya Dowans iliyozua mgogoro na serikali.

Wamiliki wa Dowans wanataka serikali kuilipa zaidi ya Sh. 90 bilioni na wamesajili mahakamani tuzo yao waliyoshinda katika mahakama ya kimataifa ya Usuluhishi ya Migogoro ya Biashara (ICC).

Shauri hilo bado liko mahakamani. Katika mazingira haya, serikali sharti iutazame mkataba huu kwa macho mawili.

Pili, kabla ya Makamba kutaka “kampuni yake” kutoingiliwa, ni vema akaelewa kuwa mvutano wa Dowans na TANESCO umezaa kesi ndani ya kesi zikiwemo zilizofunguliwa na Kituo cha Huduma za Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Ni ndani ya kesi hizo, mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam ilitoa amri inayopiga marufuku uuuzaji wa mitambo ya Dowans bila idhini yake. Imetaka lolote lisifanyike bila kupatikana kwa idhini ya mahakama.

Sasa tayari imethibitika kuwa makampuni ya Symbion Power na Dowans katika hicho wanachoita “kuuziana mitambo” hawakutekeleza maagizo ya mahakama.

Msingi wa amri ya mahamaka umelenga kuipa nguvu ya kisheria hoja kuu iliyopo mahakamani, kwamba wananchi ambao ndio wenye serikali wanapinga wanaosema wanaidai serikali.

Hivyo basi, wanaiomba mahakama impuuze aliyewasilisha madai na imuamuru kulipa fidia ya hasara iliyopatikana na gharama za kesi iliyofunguliwa.

Tatu, kabla ya Makamba kukubali kujiingiza kwenye ndoana za Dowans zilizorushwa kupitia Symbion Power LLC, angejipa muda wa kujirejesha katika historia ya kampuni hii.

Kama angefanya hivyo, angeelewa kuwa Dowans iliyouza mitambo yake imerithi mkataba wa kuzalisha umeme wa kampuni ya Richmond ambayo Bunge la Jamhuri, ambalo Makamba analitumikia, limethibitisha kuwa kampuni hiyo ilikuwa ya kitapeli.

Dowans na Richmond – kampuni iliyopewa mkataba kwa upendeleo, huku ikiwa haina fedha, utaalam wala historia ya kufua umeme – zilibadilishana mkataba 23 Desemba 2006 kinyume cha sheria za nchi.

Nne, kampuni inayoitwa Dowans Tanzania Limited (DTL) haitajwi popote wakati wa Richmond na Dowans ya Costa Rica zikibadilishana mkataba. Kuibuka kwa kilichoitwa Dowans Tanzania Limited, kulifahamika mara baada ya “dili” la kuiunganisha Dowans Holding S.A na TANESCO lilipofanikiwa.

Bali, Dowans Tanzania Limited iliyoanzishwa mwaka 2006 na mmoja wa wakurugenzi wake akiwa Brigedia Jenerali Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi ndiyo inayodai kumiliki mitambo iliyopo Ubungo.

Brigedia huyo anayedaiwa kuwa alikuja nchini Februari 2011 na kutembelea mitambo yake, aliwaambia waandishi wa habari nchini, “Ni mimi pekee ninayemiliki mitambo ya Dowans iliyopo Ubungo.”
Lakini mwenye nguvu ya kisheria (Power of Attorney) – kushitaki na kudai serikali Sh. 94 bilioni za Dowans – ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Nguvu ya kisheria alionayo Rostam haikutolewa na Brigedia Al Adawi. Ilitolewa na Bernal Zamora Arce anayejitambulisha kuwa rais wa kampuni hiyo. Naye anasema, “Mimi ndiye mwenye Dowans Holdings SA ya Costa Rica.”
Haya yameandikwa kwa muda mrefu. Ama Makamba ameyasoma na kuyadharau au anadhani wabunge na wananchi wana uelewa mdogo. Au anataka kusema haramu inaweza kuzaa halali?

Tano, makampuni ya Richmond na Dowans yako mahakamani nchini Marekani yakivutana juu ya uhalali wa umiliki wa mitambo ya Ubungo. Richmond imeeleza mahakama kuwa sehemu ya mitambo ile ni mali yake na hivyo inataka mahakama iamuru Dowans kuipa sehemu ya malipo yatakayopatikana kwenye tuzo au kwenye uuzaji wa mitambo. Shauri hili nalo bado halijamalizika.

Je, hapa wananchi hawastahili kujadili mustakabali wa fedha zao? Hawastahili kujua nani anayelipwa fedha zao? Hawapaswi kuhoji, kama Richmond itanufaika na fedha za umma, inakuwaje serikali ikalipa kampuni feki na papohapo ikaridhia kufunga mkataba uliorithiwa na makampuni feki?

Sitta, Richmond ndiyo iliingiza kilema katika ndoto za kisiasa za mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kwa “kuibeba” kampuni hiyo isiyokuwa na sifa. Ni Richmond inayotaka kutumiwa sasa na wenzake katika chama kumuweka nje ya vikao muhimu vya maamuzi ya chama chake.

Ripoti ya Bunge ilimtuhumu moja kwa moja Lowassa, kukiuka maagizo ya serikali. Serikali wala Lowassa hawajakanusha madai ya Bunge.

Aidha, Richmond haikupatikana katika mchakato wa wazi. Ilibebwa. Ripoti ya Bunge na nyaraka kadhaa za serikali, vinathibitisha kuwa Richmond haikuwa na sifa ya kufanya kazi iliyoomba.

Je, inawezekana maelezo ya Makamba katika hili yamelenga kumkosha Lowassa kwa kuwa sasa inaweza kuchukuliwa kuwa uamuzi wake wa kuipa kazi Richmond umesaidia taifa kuondoka katika giza?

Je, hiyo ndiyo kazi ambayo ametumwa kuifanya? Kama ndiyo, hiki kinachofanywa na sekretarieti ya chama chake – kujivua gamba – wananchi wakichukulie vipi? Je, ni kweli kuna dhamira ya dhati au kiini macho?

Makamba anajua kuwa pamoja na kwamba serikali haikuwahi kuipa kampuni ya Richmond malipo ya awali, lakini iliidhamini katika mabenki. Ililipiwa kile kilichoitwa “Hati ya Dhamana” (Letter of Credit - LC). Ni hati hiyo ya dhamana iliyotumika kununulia baadhi ya mitambo iliyopo Ubungo na ndiyo iliyounda Dowans inayozungumziwa sasa.

Haingii akilini kuwa Bunge ling’amue kuwa Richmond ni kampuni hewa, halafu Makamba asijue. Huu utaitwa mchezo mbaya wa kuigiza hadharani.

Lakini ukiacha hilo, haikutarajiwa kuwa Makamba ambaye mwenyekiti wa chama chake, Rais Jakaya Kikwete amemteua kuwa mmoja wa wajumbe wa NEC vijana huku mwenyewe akijitapa kuwa ni damu mpya, ashindwe kukishauri chama chake kutafuta vyanzo vipya vya umeme.

Kwa muda wa miaka sita, tokea Makamba akiwa msaidizi wa Kikwete, serikali imeshindwa kulipatia ufumbuzi suala hilo. Badala yake kila uchao, serikali inahubiri na kuota Dowans.

Je, iko wapi mipango ya umeme ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi ambayo Kikwete na chama chake waliihubiri katika kipindi cha kampeni miezi sita iliyopita?

Au pale Kikwete aliposema, “…suala la mgawo wa umeme litakuwa historia,” alikuwa ana maanisha kuwa alilenga Dowans?

Je, kunahitajika miaka mingapi kuagiza mitambo ya kuzalisha umeme kutoka Marekani au Ulaya na mitambo hiyo kuingia nchini na kufungwa, hadi kila siku hadithi ibaki ileile ya Dowans?

Kama serikali inataka kufunga mkataba wa kuzalisha umeme unaotokana na mitambo ya Dowans, ni vema ingefunga mkataba wa aina hiyo na mmiliki wa Dowans ambaye tayari alikubali kusamehe sehemu ya deni analodai.

Tayari anayejiita mmiliki wa Dowans, Brigedia Al Adawi aliripotiwa kukubali kufuta sehemu ya deni lake ili kuendeleza biashara. Je, hapa serikali haijaliona hilo? 
Kwa kufanya hivyo, serikali ingeweza kuondokana na kesi iliyofunguliwa; deni lisingelipwa; makampuni ya uwakili yasingeendelea kukaba koo TANESCO kwa kudai malipo yao na hata usumbufu wa kwenda na kurudi mahakamani usingekuwapo.

Makamba anafanya siasa; lakini anasema atazuia wanasiasa kufanya siasa kuhusu walionunua mitambo ya Dowans. Anasema nini? Amepata wapi uwezo wa kunyamazisha wananchi kuhusu fedha zao na maisha yao?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: