Makamba kinara wa uongo Biharamulo


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Gumzo
Atumia ubabe wa CCM kutishia wapiga kura
Yusuph Makamba

NGWE mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueneza uwongo imewadia. Kiongozi mkuu katika hili ni yuleyule, Yusuph Makamba, katibu mkuu wa chama hicho.

Ni kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Biharamulo Magharibi, mkoani Kagera.

Akiwa ameangaliwa na kamera za televisheni, vinasa  sauti vingine na waandishi wa habari, Makamba alifanya kufuru.

Aliwaambia waliohudhuria mkutano wake kwamba “kosa kubwa ambalo wakazi wa Biharamulo walifanya na limewagharimu sana katika miaka mitatu, ni kuchagua mbunge wa upinzani.”

Alikuwa akirejea kuchaguliwa kwa Phares Kabuye wa Tanzania Labour Party (TLP) aliyenyakua ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Akitoa macho kama aliyekurupusha swala, makamba aliwaambia waliokuwa wakimsikiliza kuwa kuwa kwa wananchi kuchangua mpinzani walikuwa wamechagua kujinyima maendeleo.

Hakuna aliyemshangilia Makamba. Kila mmoja alionekana kupigwa na baridi kali huku wakimshangaa. Alirudia kauli hizo mara mbili na wakati wote kauli zake hazikupokelewa kwa makofi kama alivyotegemea.

Hilo la kutoshangiliwa linatafsiriwa na wakazi wa Biharamulo kuwa ni kung’amua kuwa Makamba alikuwa anawatukana wananchi ambao wakati huo alikuwa akiwaomba kura.

Katika kinyang’anyiro cha Biharamulo, washindani wakuu ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichosimamisha Anthony Mbassa na CCM inayowakilishwa na Oscal Mukassa.

Wakazi wa Biharamulo wanajua kuwa jimbo la Busanda ambako CCM ilitangazwa kushinda katika uchaguzi mdogo mwezi mmoja uliopita, lilikuwa na mbunge wa chama hicho kikongwe, lakini halina maendeleo yoyote.

Busanda hakuna umeme. Wakazi wake wanaona umeme kwenye migodi wakati wao wanawasha vibatari vinavyounguza nyumba zao za nyasi kila kukicha.

Busanda kuna madini lakini wananchi hawapewi leseni za kuchimba. Leseni wanapewa watu kutoka nje ya nchi huku wananchi wanaendelea kuwa masikini zaidi; kuwa watumwa kwa wazungu waliowafukuza mwaka 1961.

Uchafu wote huu waliovishwa wananchi wakazi wa Busanda ulifanywa wakati wa ubunge wa CCM tangu uhuru hadi juzijuzi tu alipofariki Faustin Kabuzi Rwiromba.

Je, uwongo huu utapenya vichwa vya wapigakura wa Biharamulo? Hapana. Wananchi wanajua kuwa shida na umasikini wao havikuanza jana. Hata Anatory Choya, ambaye amekuwa bungeni kwa tiketi ya CCM, tena kwa vipindi miwili, alikuwa akipakata dhiki hizi na kuzilea kama CCM ilivyotaka.

Uongo wa Makamba basi, huenda usifanikiwe. Wananchi wa Biharamulo siyo wajinga. Hilo Makamba analijua vema. Lakini anatumia karata nyingine; nyingi ni za kijinga na kufedhehesha, lakini ni juhudi za mwamba ngoma.

Tayari wiki mbili za kampeni za uchaguzi zimeanza kuwa ngumu kwa chama cha Makamba ambacho kipo madarakani kwa karibu nusu karne.

Wala Makamba na viongozi wenzake hawawezi kujitapa kwamba bado wako imara. Ya Busanda, mkoani Mwanza, siyo lazima yawe ya Biharamulo.

Ahadi ambazo watawala wameshindwa kutekeleza kwa miaka 40 ndizo wamepeleka Biharamulo kama chambo cha kunasia kura.

Hata kabla kampeni kukolea, tayari Makamba ametishia msimamizi wa uchaguzi, kwamba akitangaza Chadema kuwa mshindi katika uchaguzi huo, “basi ajue hana kazi.”

Bali wananchi wa Biharamulo wanaijua vema CCM. Wanaelewa kauli za Makamba zinatokana na kiwewe na woga wa kushindwa.

Vitisho vya Makamba vyaweza kuwa vile vya mfamaji. Lakini si haba. Wakazi wa vijijini na miji midogo nchini hawakuzoea kukemewa, kukaripiwa wala kushurutishwa na viongozi wa ngazi za juu.

Wanajua wakuu wao wa vijiji, kata na wilaya ambao tayari wamewazoea na hawawaogopi tena. Sasa inapokuwa utawala wa juu umeungana na ule wa chini katika vitisho, hali hii inaweza kuathiri hata uamuzi wao wakati wa kupiga kura.

Hadi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatoa tamko lolote juu ya kauli za Makamba. Hili linazua mashaka iwapo tume hii, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, bado ni huru au imewekwa mfukoni na watawala.

NEC inajua kuwa vitisho vya Makamba vinaweza kuvuruga uchaguzi. Inajua kuwa kwa kauli ya Makamba wananchi wanaweza wasijitokeze kupiga kura kwa vile tayari ametoa maelekezo kwa  msimamizi kutangaza ushindi kwa chama chake.

Makamba analinda nafasi yake. Wakati anaonya msimamizi wa uchaguzi, anajua fika kuwa chama chake kikishindwa naye pia “hana kazi.”

Uzoefu unaelekeza kuwa CCM ikishindwa inaweza kunyamaza kama ilivyofanya Tarime, lakini katika miezi ya karibuni Makamba amekuwa akituhumiwa, ndani na nje ya chama chake, kutokuwa makini katika utendaji yake.

Hatua ya NEC kuendelea kung’ang’ania kufanya uchaguzi Biharamulo, wakati Makamba tayari ameshamtangaza mshindi, inaonyesha kuwa kinachofanyika Biharamulo ni mchezo wa kuigiza. 

Kutokana na hali hiyo, iwapo watatokea watu na kusema uchaguzi huu umekwenda vizuri na uliendeshwa kwa misingi huru na haki, watakuwa wameishia tu kuangalia zoezi la upigaji kura na matokeo, au watakuwa wameamua, kwa makusudi, kufumbia macho kauli ya Makamba.

Lakini kwa kweli, zoezi zima la uchaguzi huu tayari limevurugwa na Makamba. Wananchi hawatapewa tena nafasi ya kuchagua mgombea wanayemtaka. Vitisho vimekuwa ni vingi.

Katika hilo la kuhakikisha CCM kinashinda, au kutangazwa mshindi, chama hiki kimegeuza uchaguzi kuwa uteuzi.

Katika mshololo wa vituko, tayari Makamba ametangaza hadharani kumfukuza kazi Katibu Jumuiya ya Wazazi wa CCM, wilaya ya Biharamulo, Mussa Mwevi.

Mwevi anatuhumiwa kutoa siri za chama chake kwa washindani wake wakuu katika uchaguzi huo, Chadema.
 
Alimwita msaliti. Akamtaka akabidhi kadi ya chama chake, Jumuiya ya Wazazi na kitambulisho cha kazi kwa afisa wa chama hicho.

Makamba alimtaka ofisa huyo aende kufunga virago vyake tayari kwa safari ya kurudi kwao akisema ameshamfukuza kazi na kuongeza, “Tutakutana huko Dar es Salaam tukiishamaliza uchaguzi nikupangie kazi nyingine.”

Mashuhuda wanasema ilikuwa ni kama mchezo wa kuigiza, “Makamba alitoa Sh. 100,000 (laki moja) aliyosema kuwa itamsaidia kwa nauli ya kumuwezesha kurudi nyumbani kwao.”

Haijulikani siri zipi ambazo Makamba anatuhumu Mwevi kuzitoa kwa washindani wake, kwani katika uchaguzi wa kistaarabu, kinachoshindaniwa ni kunadi sera na uwezo wa mgombea.

Vinginevyo, Makamba anapanga siri nyingine kinyume na hiyo. Labda siri ya wizi wa kura, au ununuzi wa shahada za kupigia kura au matumizi ya vyombo vya dola kuvuruga uchaguzi.

Kama hayo siyo ambayo Makamba na wenzake wanayojadili na kupanga katika vikao vya siri, basi ni wazi kutakuwa na jingine ambalo hataki kulitaja.

Kama Mwevi angekuwa mwanachama wa TLP, na kwamba aliyechukua jukumu la kumfukuza ni mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema, angalau angeeleweka.

Maana staili hii ya kufukuzana hadharani imebuniwa na Mrema na imekuwa inatekelezwa na yeye mwenyewe ndani ya chama chake kila alipochaguliwa au alipojichukulia uongozi.

Lakini hii siyo tabia ya CCM. Inawezekana Makamba ameinakili kwa Mrema. Bali Makamba na Mrema wanafanana katika kutenda kazi zao.

Huku akionyesha kutokujua sheria, kanuni wala katiba ya CCM, Makamba alimpa Mwevi Sh. 100,000 (laki moja), akisema ni nauli ya kumrudisha kwao.

Makamba anajua kuwa hana uwezo wa kumfukuza Mwevi aliye chini ya WAZAZI bila hata ushauriano na jumuiya hiyo. Lakini amefika mbali zaidi. Mbele ya kadamnasi ametangaza kumvua uwanachama.

Makamba si chama. Ni mtendaji katika chama. Hivyo hapaswi kutenda kinyume na matakwa ya chama na wanachama wake.
Hatua yake inakwenda kinyume na misingi ya sheria na kinyume cha kanuni za utumishi za CCM na jumuiya zake.
 
Hata kama tuhuma alizotwishwa Mwevi zingekuwapo, bado Makamba hakuwa na uwezo wa kuchukua hatua alizochukua.

Akiwa katibu mkuu wa CCM, Makamba  anajua kuwa jumuiya za chama hiki ni taasisi huru zinazojiendesha zenyewe. Msingi mkubwa ni kuwa wakati jumuiya inatekeleza majukumu yake, isiathiri katiba ya chama.

Ndiyo maana jumuiya hizi zina kanuni zake za uongozi, uanachama na hata kanuni za ajira. Kwa mujibu wa kanuni za jumuiya za CCM na hata katiba ya UWT, vipo vikao vinavyohusika na ajira ya mtumishi wa jumuiya hizi.

Hata watumishi wa chama wanaajiriwa na vikao sio kiongozi. Mwenye mamlaka ya kumuondoa au kumuweka mhusika, si  mwenyekiti wa CCM taifa, au Makamba. Ni kanuni na taratibu za jumuiya husika na katiba ya CCM.

Kwa kuzingatia hili, katibu wa wazazi wa wilaya huajiriwa na kamati ya utekelezaji ya taifa ya jumuiya hiyo. Kikao kilichomwajiri ndicho kinachopaswa kupelekewa malalamiko ili kichukue hatua; siyo mtu binafsi.

Bali Makamba amemfukuza kazi Mwevi hadharani. Ni staili ya utendaji wa Mrema.  Inaonyesha Makamba amechoka kazi na hivyo anahitaji kupumzika.

Kama angekuwa hajachoka, Makamba alitakiwa kupeleka tuhuma za Mwevi ndani ya chama na kumshitaki kuwa amehujumu chama kwa kuwambia wananchi wa Biharamulo kuwa  wasimchague mgombea Oscar Mukassa.

Si tuhuma za kukutana na viongozi wa Chadema na kujadiliana mambo ya CCM. Kwani watu makini watamshangaa. Hata Makamba anakutana na wananchama na viongozi wa upinzani. Je, naye anatoa siri za CCM?

Chama cha Makamba ni chama kikongwe. Kimekuwa madarakani kwa miaka mingi; hakiwezi kuhofia majadiliano ya katibu wa jumuiya ya wazazi na maofisa wa ngazi ya chini wa upinzani; hata wangekuwa wa ngazi ya juu.

Tayari wapinzani wa CCM wanadai kwamba Mukassa si raia wa Tanzania. Wanasema ni raia wa Uganda. Madai hayo yametupwa na NEC kwa ukosefu wa ushahidi.

Tatizo kubwa la Makamba ni kule kuwa kigeugeu. Anatumia kanuni na sheria pale anapohitaji kutimiza malengo yake, si kwa maslahi ya CCM.
 
Ndio maana wakati mmoja alisimamia maamuzi ya kumfukuza uwanachama wa Jumuiya ya Vijana (UV-CCM), kada wa chama hicho, Nape Nnauye.

Kwa sauti ya juu, Makamba alihubiri, “UV-CCM wasiingiliwe katika maamuzi yao.” Alisema hakuna mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi ya vijana, bali ni vijana wenyewe.

Alisema UV-CCM wana kanuni zao na miongozo yao; Nape hana pakwenda. Alidai kuwa kwa uamuzi wa Baraza Kuu la Vijana, Nape amehukumiwa “mbiguni na duniani.”

Makamba alijua, kama sote tujuavyo, kwamba kikao kilichomteua Nape kwa nafasi zake ndani ya CCM ni Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC); na kwamba ni NEC iliyokuwa na uwezo wa kumvua uwanachama wake.

Wananchi bado wanakumbuka jinsi Makamba alivyomfukuza kazi aliyekuwa Katibu Msaidizi wilaya ya Hanang’, Daniel ole Porokwa.
 
Lakini jambo moja ni wazi. Kwamba haya yote yanatokea kutokana na mipango na sera mbovu za serikali ya chama kilichopo ikulu.

Huwezi kuwa na chama imara cha siasa na ambacho kinataka kuingia katika ushindani na vyama vingine, kikiwa na mtendaji mkuu wa aina ya Makamba.

Kinachowashanga wengi, ni hatua ya mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kung’ang’ana na Makamba.

Pamoja na kelele zinazopigwa kila kona na wanachama wa chama chake na hata kwa wasio wanachama, bado Kikwete ameshindwa kuchukua hatua ya kumuondoa Makamba katika utawala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: