Makamba, Londa "waingia mitini"


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 February 2009

Printer-friendly version
Wakimbia kesi yao dhidi ya mbunge
Yusuph Makamba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuph Makamba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, Salum Londa, wameingia mitini katika kesi yao dhidi ya mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Halima Mdee.

Makamba na Londa tayari wamewasilisha barua kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta kuomba kuondoa mashitaka yao dhidi ya Mdee.

Haikufahamika mapema kwa nini Makamba na Londa wameamua kuondoa shauri hilo, lakini taarifa zilizofikia gazeti hili zinasema “wameshindwa kujenga hoja maalum ya mashitaka yao.”

Makamba na Londa walimshitaki mbunge viti maalum (Chadema) katika Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wakidai amewakashifu na kuwadhalilisha.

Taarifa kutokana duru za bunge zinasema viongozi hao wamefuta mashitaka yao wakati Kamati ikiwa bado inaendelea kushughulikia suala hilo. 

Mdee alisema bungeni kuwa Londa ambaye ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni ameuza viwanja Na. 965 na 996 vilivyopo eneo la Kawe, Dar es Salaam kwa mwekezaji wa kigeni kinyume cha taratibu.

Alisema pia kuwa Londa analindwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba vinginevyo uongozi wa halmashauri yake ungekuwa umemchukulia hatua.

Lakini kabla Kamati ya bunge haijahitimisha kusikiliza shauri hilo, taarifa zinasema Makamba na Londa “wamekimbia kesi yao.”

Taarifa nyingine zimeeleza kuwa kitendo cha Makamba na Londa kuondoa shauri lao kinatokana na taarifa zilizovuja kwamba Mdee ana ushahidi usiopingika juu ya madai yake.

Aidha, imefahamika kuwa sakata hilo likitanuka kupitia bunge litawapa nguvu madiwani na viongozi wengine Kinondoni ambao wamekuwa wakiweka shinikizo kwa Londa kujiuzulu.

Bila kutaja ni hoja gani iko mezani, MwanaHALISI lilimuuliza Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila kutaka kujua ni hatua gani zinachukuliwa pale walalamikaji wanapokuwa wameondoa shauri lao kwenye Kamati.

Dk. Kashilila amesema anayeleta shauri ana haki ya kuliondoa, lakini kwa kuwa limeishafika kwenye Kamati na Kamati imeanza kulishughulikia, lazima Kamati itoa taarifa yake.

Kuhusu waliofuta mashitaka kulipa  gharama za Kamati za kusikiliza shauri, Dk. Kashilila amesema gharama zote zinalipwa na bunge.

MwanaHALISI inayo nakala ya barua ya Makamba ya 31 Desemba 2009 ya kuomba kuondoa mashitaka dhidi ya Mdee. Barua iliandikwa siku 14 baada ya shauri hilo kuanza kusikilizwa.

Katika barua hiyo yenye Kumb. Na. CMM/ PF. 36002/106 VOL IV/ 30 kwenda kwa spika wa bunge,  Makamba anasema machungu ya kutuhumiwa “yameisha.”

“Nashukuru kwamba umeonyesha mwito juu ya malalamiko yangu, lakini kwa kuwa muda umepita sasa na hata machungu niliyoyapata nimeshaanza kuyasahau, ninaomba kwa idhini yako kuyaondoa malalamiko hayo na kutoendelea nayo,” ameandika Makamba.

Hata hivyo, Makamba anakiri katika barua hiyo kwamba hakuwahi kuhudhuria kwenye kikao cha Kamati ingawa alipata barua ya wito.

Sababu zilizotolewa na Makamba ni kama zile zilizotolewa na Londa. Barua ya Londa ya 17 Junuari 2009 inasema, “Nilituma barua kwako juu ya kauli ya mheshimiwa Mdee, lakini kwa kuwa muda mrefu na suala hili limeshaanza kusahaulika, naomba kukutaarifu juu ya kuondoa hoja hiyo.”

Londa alifika mbele ya Kamati tarehe 14 Januari 2009.

Baadhi ya nyaraka ambazo Mdee aliwasilisha mbele ya Kamati na ambazo zinaweza kuwa zilisababisha Makamba na Londa kuingia mitini, ni taarifa za ndani za vikao ambavyo vilikuwa vikimsulubu Londa.

Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iko chini ya mwenyekiti, Anne Kilango Malecela ambaye ni mbunge wa Same Mashariki.

Juhudi za kumpata Kilango na Spika hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: