Makamba, Londa roho juu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version
Yusuph  Makamba

UAMUZI juu ya shauri lililofunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuph Makamba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Salum Londa dhidi ya mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (Chadema), unatarajiwa kutolewa katika mkutano wa Bunge ulioanza hapa jana, imefahamika.

Habari za kuaminika kutoka Dodoma zinasema, shauri hilo ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huu wa 15.

Makamba na Londa walimshitaki Mdee kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wakidai amewakashifu na kuwadhalilisha.

Taarifa kutoka duru za bunge zinasema tayari Kamati ya Bunge imemaliza kazi yake na ripoti kukabidhiwa kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Mdee alisema bungeni kuwa Londa ambaye ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni ameuza viwanja  Na. 965 na 996 vilivyopo eneo la Kawe, Dar es Salaam kwa mwekezaji wa kigeni kinyume cha taratibu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Spika Sitta alitarajiwa kupitia taarifa hiyo mara baada ya kuwasili nchini kutoka nje ya nchi juzi na kupanga siku ambayo shauri hilo litawasilishwa bungeni.

Hata hivyo, mara baada ya Mdee kuwasilisha nyaraka mbalimbali kama ushahidi wa kile alichokisema, Londa na Makamba waliandika barua kwa Spika Sitta kuomba kuondoa mashitaka yao dhidi ya Mdee.

Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, hata kama walalamikaji wameondoa shauri lao, lazima Bunge lipewe taarifa juu ya mwenendo mzima wa shauri hilo na uamuzi wake.

Aidha, wabunge watatu wa CCM na wawili wa upinzani wamejipanga kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano huu wa Bunge.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila alipotakiwa kuzungumzia suala la hoja binafsi, alisema alikuwa hajawasiliana na Spika Sitta.

“Spika yupo safarini, sijawasiliana naye. Naomba nitafute kesho (jana Jumanne), labda ninaweza kuwa na la kusema,” alisema Dk. Kashilila.

Taarifa ambazo hazikuweza kuthibishwa zinasema moja ya hoja binafsi huenda ikawa juu ya rais mstaafu Benjamin Mkapa kuhusiana na kiwanda cha mkaa wa mawe Kiwira mkoani Mbeya ambacho anahusishwa na umiliki na uendeshaji wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: