Makamba, Nchimbi waumbuka


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 16 September 2008

Printer-friendly version
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Emmanuel Nchimbi

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba wameumbuka.

Tarehe 5 Oktoba 2008, Makamba na Nchimbi wanadaiwa kuitisha kikao cha Baraza Kuu la UV-CCM mjini Dodoma, kuagiza, kuchochea na kushinikiza wajumbe wa baraza hilo kumfuta uanachama Nape Nnauye.

Madai ya Makamba na Nchimbi yalikuwa kwamba Nape “amedhalilisha viongozi wake.” Hii ilitokana na Nape kuamua kukosoa hadharani mkataba wa kinyonyaji wa umoja huo.

Nape, Mjumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), alisema tarehe 22 Julai mwaka huu kuwa Baraza la Wadhamini la UV-CCM, chini ya Edward Lowassa liliingiza jumuiya hiyo katika mkataba unaonuka ufisadi na usio na manufaa kwa jumuiya.

Alisema Baraza la Wadhamini halikuwa na mamlaka ya kufikia maamuzi hayo kwa sababu “Baraza Kuu la UV-CCM, lenye mamlaka ya uamuzi wa mwisho, lilikuwa halijaridhia mkataba huo.” 

Sasa imefahamika kuwa siyo UV-CCM bali Lowassa na Nchimbi ndio waliingia  mkataba na makampuni mawili ya M.M. Integrated Steel Mills (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL), yote ya Dar es Salaam katika mazingira ya utata.

Hata hivyo, mara baada ya Kamati Kuu (CC) wiki iliyopita, kugoma kusaini mkataba na kuunda tume ya watu watatu kuupitia upya, watetezi wa mkataba wamekuja na madai mapya. Wanasema, “Nape amehukumiwa kwa kusema uwongo.”

UV-CCM ni chombo cha waumini katika siasa moja na malengo yake. Haikutarajiwa viongozi wa umoja huo kufukuza muumini mwenzao kwa kauli sahihi ambayo hata viongozi wakuu wa chama wamekubali mantiki yake.

Pili, hoja ya Makamba kwamba Nape alizungumza nje ya vikao vya chama chake, haina msingi wa kisheria na wala haiwezi kuhalalisha uharamia uliolengwa kufanywa. Tuone mifano.

Muasisi wa TANU na CCM, Mwalimu Julius Nyerere alizungumza hadharani udhaifu wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba na John Malecela aliyekuwa Waziri Mkuu.

Mwalimu alitunga hata kitabu kilichowashambulia viongozi hao wawili. Hakuulizwa na mtu yeyote, wala hakufukuzwa katika chama.

Mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa David Msuya na Fredrick Sumaye, wametoa kauli za kumuonya Makamba hadharani.

Hatujasikia Makamba akiwakemea au kuwauliza Msuya na Sumaye, “Ninyi mlikuwa mnakuja Dodoma; ni wajumbe wa NEC, kwa nini mnazungumza mkiwa Kibaigwa? Kwa nini msisubiri vikao vya chama?”

Makamba hajawauliza. Hatawauliza. Hawezi kuwauliza na hana haki ya kuwauliza, pale wanapokuwa wanatoa maoni yao juu ya jambo la maslahi kwa chama chao na taifa kwa ujumla.

Tatu, hata kama ingekubaliwa, kama Nchimbi anavyoimba, kwamba Nape ameadhibiwa kwa “kusema uwongo,” ushahidi uliopo unakana hilo.

Hadi sasa, karibu wajumbe wote wa Baraza la Wadhamini wa UV-CCM wamekana kuona hata kushiriki kupitisha mkataba huo. Hilo linafanya mkataba uwe wa Lowassa na Nchimbi.

Hapa mwongo ni nani kati ya Nchimbi, Lowassa na Makamba kwa upande mmoja na Nape kwa upande mwingine? Jibu sahihi la swali hili ndilo linawaumbua wabaya wa Nape.

Ona wenyeviti 15 wa mikoa wa UV-CCM ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Vijana  tayari wamenukuliwa na gazeti la MWANANCHI wakikana kupitisha mkataba.

Ni hali hii ya mkataba wa Nchimbi na Lowassa iliyopelekea Nchimbi, Lowassa na Makamba kunywea katika kikao cha NEC mjini Dodoma pale Mwenyekiti Jakaya Kikwete alipokuwa analitolea hoja suala la Nape.

Tatu, hata kama Nape angekuwa na makosa, kama ambavyo Makamba na Nchimbi wanataka kuaminisha umma, adhabu iliyochukuliwa, ya kumg’oa, ilikuwa kama kuua sisimizi kwa kutumia nyundo. Haikuwa sahihi.

Nne, utaratibu umekiukwa. Hatua ya kumfukuza kiongozi ndani ya UV-CCM na mzazi wake CCM ni kwanza kuwa na onyo, ndipo karipio au karipio kali kabla ya kipindi cha uangalizi na baadaye hatua ya kufukuza muhusika.

Hilo halikufanyika. Kutofanyika huko ndiko kunaleta mashaka juu ya haraka iliyokuwepo katika jambo lililohitaji mjadala.

Tano, kuingiza hoja ya kumbana na kumfukuza uanachama Nape wakati wa kipindi cha uchaguzi na wakati yeye ni mgombea, kunaleta mashaka juu ya hatua hiyo.

Hapa hakuna atakayeshindwa kuona kuwa hatua ya haraka dhidi ya Nape ililenga kumkosesha fursa ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa umoja huo.

Sita, utaratibu ni kwamba mashitaka hutolewa kwa maandishi. Kabla mtuhumiwa hajahukumiwa, sharti apewe nafasi ya kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mambo haya yote hufanyika kwa maandalizi ya muda mrefu ili kuepusha maamuzi ya jazba.

Lakini kwa Nape taratibu hizo hazikufuatwa. Mtuhumiwa amesomewa mashitaka saa 5.30 na kuhukumiwa saa 6. Hapa ni wazi kwamba uamuzi ulikuwa tayari umepangwa.

Saba, wanaomtuhumu Nape wanakuwa walewale wanaoendesha mashitaka, walewale wanaosikiliza kesi na walewale wanaosema, “Nape hawezi kukata rufaa mbiguni wala ardhini.”

Katika madai yake Nape alimtuhumu Lowassa, Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu wa UV-CCM, Francis Isaack kwa kile alichosema, “wameingiza UV-CCM katika mkataba wa kifisadi.”

Nane, katika hali hiyo, Makamba, Nchimbi na Issack walikuwa na maslahi katika kesi ya Nape; hivyo hata kama Nape alikuwa kweli na kesi ya kujibu, Makamba, Nchimbi na Isaack hawakustahili kushiriki katika kikao cha kutoa hukumu.

Tisa, kwamba wahusika walikuwa na chuki na walijawa na uhasama dhidi ya Nape. Hii ndiyo maana Makamba alidiriki kusema, “Nape hana pa kwenda; hakuna kukata rufaa. Amehukumiwa duniani na mbinguni.”
 
Kumi, Makamba ameshindwa kujua kuwa hakuna chombo chochote kinachoweza kuhukumu na hapohapo kikajitangaza kuwa uamuzi wake ni chawa mwisho.

Kama Baraza Kuu lingetaka kujipa madaraka hayo, basi suala la Nape lingeanzia vikao vya chini.

Na hata hapo, na hata kama katiba yao inasema hivyo, utaratibu wa kufikia maamuzi hayo bado unaweza kulalamikiwa na kusikilizwa mahakamani.

Kumi na moja, Makamba ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana kwa nafasi yake. Ilitarajiwa na kwa hakika ndivyo ilivyo, kwamba kazi yake katika baraza la vijana ni kusikiliza na kushauri.

Haikuwa kazi ya Makamba kushiriki hatua yoyote ile ambayo ingetafsiriwa kuwa shinikizo au uchochezi na matumizi ya  kikao cha vijana kupanga viongozi wa kuongoza UV-CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: