Makamba zigo zito CCM


Josephat Isango's picture

Na Josephat Isango - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version

KAMA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakufa kabisa, Katibu Mkuu wake, Yusuph Makamba atapaswa kuwa mtu wa kwanza kuwajibika.

Hasikii, haoni aibu. Ana maamuzi ya kipuuzi. Anasababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe – ndani ya chama na ndani ya nchi.

Na ingawa inasemekana uzee ni dawa, huu wa Makamba ni sumu! Kwa staili yake ya uongozi, Makamba atakapostaafu ataagwa na watu wengi sana watakaokuwa wanashangilia kuondoka kwake.

Amefanya na kusema mengi ya kipuuzi huko nyuma, likiwamo la juzi kuhusu vurugu mkoani Arusha.

Ni yeye pekee aliyeshangilia vifo vya raia waliopigwa risasi na bunduki. Ni yeye pekee aliyejitokeza kupinga kwa nguvu ushauri wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, aliyetaka CCM na CHADEMA wajadiliane badala ya kupigana kuhusu mustakabali wa Arusha.

Ni yeye pekee aliyebeza kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha aliyetoa ushauri kama wa Lowassa – ingawa alichelewa hadi vurugu na vifi vikatokea – kwamba suala la Arusha ni la kisiasa, hivyo limalizwe kisiasa, kwenye meza ya majadiliano.

Miongoni mwa viongozi wakuu wa CCM, ni Makamba pekee aliyebaki kumtetea – walau hadharani – Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Tanga, Mary Chatanda, ambaye alipiga kura katika uchaguzi haramu wa Meya wa Jiji la Arusha, kinyume cha utaratibu.

Ni Makamba pekee aliyewashambulia viongozi wa dini, hasa maaskofu, waliotoa kauli kulaani vurugu hizo, na kusema hawamtambui meya haramu wa Arusha, na kwamba hawatampa ushirikiano.

Katika hali inayoonyesha upeo mdogo sana wa Makamba kuhusu kazi za viongozi wa dini, Makamba anasema maaskofu hao, “wavue majoho yao” ili wafanye kazi ya siasa!

Hana uwezo wa kuona dhambi kubwa iliyotendwa na Mkurugenzi wa Jiji, ya kula njama na serikali na CCM dhidi ya wananchi wa Arusha kwa kusimamia uchaguzi haramu na kuchagua meya haramu, na hivyo kusababisha manung’uniko na malalamiko yaliyoifikisha Arusha hapo ilipo.

Ni Makamba pekee ambaye haelewi hata maana ya kauli ya kidiplomasia ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, aliyesema “tukio la Arusha ni la bahati mbaya na halitajirudia tena.”

Ingawa ni kweli kwamba si la bahati mbaya, lakini ni dhahiri limemgusa na kumtia aibu rais, na anatamani lisijirudie tena, hata kama hana mipango wala mikakati ya kulizuia.

Na ingawa serikali yake ndiyo ilichochea yote yaliyotokea Arusha, kiongozi makini hawezi kushangilia maafa kama haya, tena hadharani. 

Makamba na Chatanda, ambaye pia aliwadhihaki viongozi hao wa dini kwa kauli ile ile, wamegeuka mitambo ya kuchochea siasa za chuki.

Ndiyo maana Waziri Mkuu mstaafu John Malecela amejitokeza kuwataka viongozi wa CCM wawaombe radhi maaskofu kwa kauli za akina Chatanda.

Ikumbukwe kuwa licha ya nafasi zao za uongozi, maaskofu nao ni wapiga kura. Hivyo, kwa nafasi yao kama viongozi na raia, maaskofu wana haki ya kuhoji mchakato wa uchaguzi wa meya anayesimamia shughuli zinazogusa maisha yao.

Ni ujinga uliokithiri kwa Makamba na Chitanda kufikiri kwamba kazi ya maaskofu inaishia kwenye mimbari kanisani. Ni ujinga uliokithiri kwa viongozi wa siasa kutojua kwamba wananchi wale wale wanaohubiriwa Injili makanisani, ndio hao wanaohujumiwa katika maisha yao ya kawaida.

Ni ujinga wa hali ya juu kama Makamba na Chitanda hawajui kuwa kazi ya maaskofu ni kutakasa roho na miili ya waumini wao.

Ni ujinga usiomithilika kufikiri kwamba maaskofu wanaweza kukemea makoa mengine katika jamii, lakini wakaacha kosa kubwa kama hili linalogusa maisha ya watu, na hasa ambalo limeshasababisha vifo vya raia wasio na hatia.

Naamini maaskofu hawatajibizana na Makamba wala Chatanda, lakini kauli yao itasikika. Ndiyo maana tumesikia Naibu Meya ameshajiuzulu, na akasema wazi kwamba uchaguzi uliomweka yeye na meya madarakani ulikuwa haramu; na akasema pia kwamba anatambua kuwa damu ya wana Arusha imemwagika kwa sababu ya uchaguzi huo huo.

Ni bahati mbaya kwamba wakati makatibu wakuu wengine wanajenga vyama vyao, Makamba anahangaika kukibomoa chama chake. Mifano ni mingi.

Angalau baadhi ya wenzake, ukimuondoa Kikwete, wamegundua kuwa chama chao kinasambaratishwa na Makamba.

Bali itoshe kusema kuwa Makamba na Chatanda hawana uungwana wowote wa kuigwa, bali watabaki tu kama mizigo katika chama chao. Waondolewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: