Makampuni ya mafuta yakoroga Bunge


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 21 July 2009

Printer-friendly version

MGAWANYIKO mkubwa umezuka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, baada ya baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo kupinga "Mpango wa serikali wa kuagiza mafuta kwa pamoja," imefahamika.

Awali wajumbe wote wa Kamati hiyo iliyopo chini ya mbunge wa Bumbuli (CCM), William Shellukindo, walikuwa wanakubaliana na mpango huo, uliolenga kupunguza upandaji holela wa bei ya mafuta nchini.

Taarifa zinasema msimamo wa baadhi ya wajumbe (majina tunayo) umebadilika kutokana na shinikizo lililowekwa na makampuni ya kuagiza mafuta kupitia umoja wao unaofahamika kama TAOMC na kuiweka serikali njia panda.

"Mambo sasa yamebadilika. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge wamekwenda upande wa pili kwa madai ya kulinda maslahi ya taifa," taarifa zinadokeza kutoka ndani ya Kamati.

Utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja nchini ulianzishwa na unaratibiwa na serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Kikao kilichowabidilisha msimamo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Shellukindo, kilifanyika Julai 16 (Alhamisi iliyopita) mjini Dodoma .

Kilikuwa chini ya uenyekiti wa Shellukindo; kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka EWURA, Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) na TAOMC.

"Katika kikao kile, Kamati ilishambulia moja kwa moja Serikali kwa maana ya EWURA na TPDC. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima alipwaya na kushindwa kutetea serikali," taarifa zimedokeza.

Alisema, "Alikuwa ni mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya kusimama na kuiokoa serikali baada ya Malima kupwaya."

Alisema, "Shellukindo alisema msemaji wa EWURA na TPDC ni naibu waziri Malima, ambaye tayari aligoma kuendelea kutetea serikali. Kama siyo Manyanya tayari waagizaji mafuta walishafanikiwa kuisambaratisha serikali."

Ni baada ya makamu mwenyekiti wa TOAMC, Hussein Abdrukadri na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Gapco, K.G.Rai, kuja juu wakitoa madai mazito na kuita, "Mpango huo ni feki."

Manyanya alihoji kwanini EWURA na TPDC wamekuwa kama watoto yatima, huku Kamati ya Bunge ikisikiliza waagizaji mafuta peke yao .

Kauli ya Manyanya ilimfanya Shelukindo kuamka na kutaka kumkatisha, kwa kile alichosema, "Serikali inawakilishwa na naibu waziri Malima," lakini Manyanya aligoma na kuomba kuendelea hadi mwisho, ombi ambalo lilikubaliwa na Shellukindo.

"Mheshimiwa mwenyekiti, naomba niendelee hadi mwisho (Shellukindo anakaa kimya). Hapa naona hakuna maelewano kati ya TOAMC, EWURA na TPDC. Hali hii ya upande mmoja kuzungumza huku upande mwingine ukiwa umekaa kimya naona si mzuri," alisisitiza.

"Mwenyekiti mimi naona hapa ni sawa na baba ukiwa na watoto wawili, mmoja anapewa nafasi ya kujitetea na mwingine amekaa kimya bila kupewa nafasi, (Mheshimiwa Manyanya anaita Shellukindo)," inaelezwa.

Mjumbe wa TOAMC, Anam Mwemutsi, alikanusha makubaliano yote yaliyofikiwa katika kikao cha pamoja kati ya wawakilishi wa TAOMC, wizara ya nishati na madini, TPDC na EWURA.

Kikao kilichoweka makubaliano hayo kilifanyika 10 Julai 2009, mjini Dar es Salaam .

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, mbunge wa Kasulu Mashariki (CCM), Daniel Nsanzungwako, alisema Bunge linajadili suala hilo kwa maslahi ya taifa.

"Ni kweli suala hili linajadiliwa na Kamati. Ni wajibu wetu kama wabunge kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa. Ni mjadala ambao ukifika kikomo, Mwenyekiti wa Kamati (Shelukindo) atatoa taarifa," alisema.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwa kupwaya kwa serikali katika kikao cha Alhamisi iliyopita, kumetokana na kutokuwapo kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

"Ngeleja hakuwapo. Lakini katika vikao vilivyopita, kikiwamo kile cha 2 Julai 2009, alikuwa mbogo kutetea serikali," mjumbe mwingine wa Kamati alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

0
No votes yet