Makinda: Kielelezo cha uwezo wa mwanawake


Evetha L. Sway's picture

Na Evetha L. Sway - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

MBUNGE wa Njombe Kusini, Anne Semamba Makinda (CCM) ameweka rekodi nyingine. Baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, sasa amekuwa spika kamili.


Makinda ndiye ataongoza muhiili huo mojawapo wa dola baada ya kushinda kiti hicho kwa asilimia 74 na kuchukua nafasi ya Samwel Sitta aliyetemwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uteuzi.


Katika upigaji kura Makinda alimshinda mwanasheria wa kujitegemea, Mabere Marando. Kwa uteuzi huo, Tanzania imekuwa nchi ya tano barani Afrika kuwa na spika mwanamke.

Anafuata nyayo

Gambia ni kati ya nchi za mwanzo kupiga hatua hiyo kwa kuteua wanawake katika nafasi ya spika. Kwanza Bunge liliongozwa na Belinda Bidwell, halafu akaja Fatoumata Jahumpa-Ceesay ambaye alitimuliwa mwanzoni mwa Januari 2009 na nafasi yake sasa imechukuliwa na Elizabeth Renner.


Mapinduzi ya kifikra ya Gambia haraka yaliigwa na nchi nyingine za Afrika kwa kuwapa wanawake nafasi ya kuongoza Bunge.


Rwanda inasifika kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake katika vyombo vya maamuzi. Baada ya kuwa na asilimia 33 ya wabunge wote kuwa ni wanawake, Oktoba 6, 2008 ilimteua Rose Mukantabana kuongoza muhimili huo wa dola.


Januari 2009 Ghana ilimteua Joyce Bamford-Addo na
Oktoba 2009, Botswana ilipata spika wa kwanza mwanamke Margaret Nasha.


Uteuzi wa wanawake kushika nafasi za juu Afrika sasa ni jambo la kawaida na ni ishara ya kuondokana na fikra potofu kwamba nafasi ya mwanamke ni jikoni. Hata hivyo idadi ndogo ya wanawake wanaojitokea kuomba au kugombea nafasi kubwa kama hizo bado ni tatizo.


Liberia imepiga hatua kubwa zaidi pale wananchi walipomteua mwanamke,  Ellen Johnson Sirleaf kuwa rais wake.

Malengo

Uteuzi wa Makinda kuwa Spika wa Bunge ni juhudi nyingine za Tanzania za kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) kwamba ifikapo mwaka 2015 kuwe na ushiriki na uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika vyombo vya maamuzi.


Baadhi ya wanawake wa Tanzania walioonyesha uwezo na kuaminiwa kuongoza vyombo vya kimataifa ni Dk. Asha-Rose Migiro, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).


Wanawake wengine ni Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka aliyekuwa Mkurugenzi mkuu chini ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat) lenye makao makuu Nairobi, Kenya. Prof. Tibaijuka sasa ni Mbunge wa Jimbo la Muleba.


Mwanamke mwingine aliyewahi kutamba katika ngazi ya kimataifa ni Dk. Getrude Mongella, ambaye mbali na kuwa waziri katika wizara mbalimbali aliwahi kuwa mwanadiplomasia India na kubwa zaidi aliteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya wanawake. Mkutano huo ulifanyika mwaka 1995, Beijing, China.


Baadaye Dk. Mongella alikuwa Rais wa Bunge la Afrika. Na katika ngazi hiyo ya kimataifa yupo, Liberata Mulamula ambaye ni Balozi na Katibu mtendaji wa Sekretarieti ya Mikutano wa Kimataifa ya Nchi katika Maziwa Makuu (ICGLR).

Uthubutu

Baada ya wanawake kufanikiwa katika nyanja hizo za kimataifa, mwaka 1995 Rose Lugendo alijitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania urais. Alichujwa, akateuliwa Benjamin Mkapa aliyekuja kushinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi.


Mwaka 2005, alijitokeza Anna Senkoro, akapitishwa na chama chake cha PPT Maendeleo. Katika uchaguzi ule aliambulia kura 18,783 sawa na asilimia 0.17. Pengine baada ya kuona hakuna uungwaji mkubwa mkono akarejea CCM.


Hao wote wamethubutu na wametumika kama kipima joto juu ya uwezo wa mwanamke. Wiki iliyopita CCM ilimpendekeza Makinda akashinda kiti cha spika.

Uwezo

Kabla ya karne ya 19 mwanamke hakushirikishwa na hakuthaminiwa, badala yake alitazamwa kama kiumbe duni asiyeweza kufanya jambo lolote la maendeleo, kutoa maamuzi katika maisha yake ya kila siku na  hata  kutatua jambo lolote katika jamii inayomzunguka. Mara nyingi alichukuliwa kama chombo cha starehe na mlezi wa familia.                         

Hata hivyo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknologia mwanamke huyu ameweza kujikwamua na kuonyesha umahiri wake katika ulimwengu wa sasa.  Ameweza kujikita katika nyanja mbalimbali katika jamii na kusababisha mabadiliko makubwa katika uchumi wa nchi na ulimwengu kwa ujumla na kupelekea kutambulika na kukubalika katika jamii kama mkombozi wa taifa la sasa.                                    

Aidha ari hii ya kumwezesha mwanamke huyu imezidi kukita mizizi yake katika asasi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali na kupelekea nyota ya mwanamke huyu kung’ara kuaminiwa na wanaume katika nyanja zote.


Kwa miaka mingi mwanamke alinyimwa elimu—haki  yake ya msingi kubaini haki nyingine. Kwa kuwa hakuwa na elimu ilikuwa rahisi pia kumnyima haki nyingine kama vile uongozi, umiliki wa rasilimali, uhuru wa kujieleza.


Mwanamke sasa ni mbunifu mzuri, mgunduzi, mwana sanaa mzuri, mwana filosofia, kwa hiyo ana maarifa na utambuzi wa mbinu za kujikomboa na kuikomboa jamii.


Katika kupambana na matatizo yanayoukumba ulimwengu wa sasa mwanamke huyu ameonekana kuwa mstari wa mbele na kuonyesha matumaini ya mafanikio ya malengo ya milenia ya mwaka 2000 mpaka mwaka 2025.


Ndiyo maana katika suala la uongozi, wanawake wengi wamejitokeza na wanaendelea kujitokeza katika nyanja mbalimbali za uongozi kimataifa na kitaifa na kusababisha mabadiliko ya maendeleo katika kuinua uchumi wa nchi.

Uaminifu

Iko kwenye rekodi kwamba taasisi nyingi zilizoko chini ya usimamizi au uongozi wa wanawake kuna nidhamu ya matumizi ya raslimali fedha.


Katika nyanja za kitaifa zinazoongozwa na wanawake zimekuwa zikiripotiwa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi, mfano Benki ya Wanawake Tanzania ambyo mkurugenzi wake ni mwanamke.

<p> Mwandishi wa makala hii Evetha Sway ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma anayesomea shahada ya uzamili katika taaluma ya maendeleo. 0757-625470</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: