Makocha wazalendo wana mafanikio kuliko wa kigeni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly version

KOCHA mkuu wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’, Marcio Maximo alishangilia sana baada ya Jabir Aziz kupachika bao la kufutia machozi dhidi ya Brazil kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mapema mwezi huu.

Alikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo. Kwanza Stars ilinyukwa mabao mengi; pili ile ilikuwa mechi ya kirafiki hivyo bao moja lisingeweza kubadili kitu isipokuwa sifa kiasi.

Ni sifa kwa Jabir kupachika bao dhidi ya mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia na kwa Maximo kwamba ana wachezaji wanaofundishika.

Kama mechi ile ingekuwa ya kusaka ubingwa wowote ule, Maximo asingeshangilia kiasi kile. Mfano ni kocha wa Ghana.

Kocha mkuu wa Ghana, Milovan Rajevac alijizuia kushangilia bao katika matokeo ya 1-1 na Serbia kwenye hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia, Afrika Kusini.

Hakupenda kushangilia bao lililoikandamiza nchi yake. Rajevac aliyechukua nafasi ya Rantomir Antic ambaye anainoa Serbia, aliweka mbele uzalendo kuliko kibarua chake.

Moja ya sababu za kumteua Sven-Goran Eriksson kuwa kocha mkuu wa Ivory Coast ni kuwa na kocha ambaye atakuwa analipwa zaidi ya wachezaji kama kina Didier Drogba. Ubora wake ulikuja baadaye.

Nigeria, pamoja na kwamba kocha mzalendo Shaibu Amodu ndiye aliiwezesha Super Eagles kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (2010) nchini Angola na kufuzu kwenda Afrika Kusini, aliondolewa na nafasi yake akapewa Lars Lagerback wa Sweden.

Kati ya timu zote sita za Afrika zilizoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ni Algeria peke yake iliyomwamini kocha mzalendo Rabah Saadane. Kila mmoja aliona kiwango chao, japokuwa waliondolewa mapema.

Pamoja na imani ya viongozi wa soka kwa makocha wa kigeni, lakini kuna ushahidi uliowazi kwamba makocha wa kizalendo wamezipa timu mafanikio makubwa.

Misri, kwa mfano, imetwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mara saba, lakini mara tano chini ya wazalendo; 1957 alikuwa Mourad Fahmy, 1959 ni Pal Titkos wa Hungary, 1986 ni Mike Smith wa Wales. Mwaka 1998 alikuwa Mahmoud El-Gohary na kuanzia 2006, 2008 na 2010 ni Hassan Shehata.

Ghana imetwaa mara nne, lakini mara tatu ni chini ya wazalendo; 1963 na 1965 alikuwa Charles Gyamfi, 1978 alikuwa Fred Osam Duodo na 1982 alirejeshwa Charles Gyamfi na akatwaa kombe.

Congo alitwaa kombe mwaka 1972 chini ya mzalendo Amoyen Bibanzulu na Algeria ilimtumia vizuri Abdelhamid Kermali akatwaa kombe mwaka 1990.

Mwaka 1992, Ivory Coast ilitamba ikiwa na Yeo Martial na Afrika Kusini Clive Barker akaipa ubingwa mwaka 1996.

Kwa hiyo japokuwa Morocco ilimtegemea (Gheorge Mardarescu wa Romania mwaka 1976, Nigeria iliwika chini ya Otto Gloria wa Brazil mwaka 1980 na Clemens Westerhof wa Uholandi mwaka 1994, wazalendo ndio wamekuwa wakiivusha hadi kwenye fainali hizo.

Mara zote nne Cameroon imetegemea wageni (1984 -Rade Ognanovic, Yugoslavia, 1988 Claude le Roy, Ufaransa, 2000- Pierre Lechanter wa Ufaransa na 2002 Winfried Schäfer wa Ujerumani).

Ushahidi mwingine ni kwa Tanzania. Walioiwezesha Taifa Stars kutwaa Kombe la Challenge kwa mara ya kwanza mwaka 1974 walikuwa wazalendo na ndio hao waliipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1980 (hayati Paul West Gwivaha na Josel Bendera (mbunge).

Tanzania ilisubiri hadi mwaka 1994 Syllersaid Mziray alipoiwezesha Taifa Stars kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili. Mwaka 2001 ni Mziray na Boniface Mkwassa waliotwaa Kombe la Castle.

Hata aliyeteua kikosi kilichokuja kunolewa na Maximo na kufika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani alikuwa Dk. John Msolla. Baada ya kikosi hicho kusambaratishwa, kila mmoja aliona matokeo yake.

Wazalendo wana uchungu, uwezo mkubwa wakipewa kila aina ya msaada, huduma, mshahara mzuri na vifaa kama kwa makocha wa kigeni.

Bila shaka baada ya mrithi wa Maximo, Jan Borge Poulsen wa Sweden kumaliza muda wake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litawafikiria kina Mziray, Mkwasa na wazalendo wengine.

0
No votes yet