Makombora ya Dk. Slaa haya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Dk. Willibrod Slaa

UTEUZI wa Dk. Willibrod Slaa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, "unamweka pabaya" Rais Jakaya Kikwete ambaye anatetea nafasi hiyo kwa muhula wa pili, MwanaHALISI limeelezwa.

"Huyu ni mtu makini sana. Haongei bila utafiti na takwimu sahihi. Atatusumbua sana katika uchaguzi huu," amekiri mmoja wa viongozi wastaafu wa ngazi ya juu serikalini.

Amesema, "Hawa watu wamejipanga. Huyu ni mtu anayeaminika. Anaheshimika. Jamii inamfahamu. Anaweza kutoa upinzani; tena si upinzani mdogo."

Dk. Slaa ameteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mgombea urais. Atathibitshwa na mkutano mkuu wa chama hicho mapema mwezi ujao.

Woga uliopo ni kwamba pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwepo kwa miaka mingi na kuwa na uzoefu wa kampeni, Dk. Slaa ana uwezo mkubwa wa kujenga hoja kwa takwimu ambazo CCM haiwezi kuzijibu.

"Hofu yetu ni weledi wa Dk. Slaa katika kusimamia mambo kwa umakini. Haya ni mambo ambayo yanampa nafasi ya kipekee ya kuaminika na kuchaguliwa na wananchi," ameeleza kiongozi mstaafu kutoka serikali ya CCM.

Kiongozi mstaafu ambaye ametaka jina lake lisitajwe amesema kuna uwezekano mkubwa wa Dk. Slaa kumfunika Kikwete mara baada ya kampeni kuanza.

"Huyu bwana hajawahi kugombea nafasi hii. Ni tofauti na wale ambao wameshagombea mara kadhaa na kushindwa ambao sasa tayari wamekosa mvuto. Nasema huu ni mkakati mzuri kwa Chadema, kwani wengi walidhani watachukua mgombea kutoka CCM," ameeleza.

Alipoulizwa amepokeaje uamuzi wa Chadema kumsimamisha Dk. Slaa, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM alijibu haraka, "Ni uamuzi mzuri. Kwa kweli ataipatia heshima kubwa Chadema. Nadhani wamesimamisha mtu mwafaka kwa chama na wananchi kwa jumla," alisisitiza.

Hata hivyo, kiongozi huyo mstaafu alisema, "…lakini nasi katika CCM tumejipanga maana tunamgombea anayekubalika."

Kwa mujibu wa mahojiano ya gazeti hili na wananchi na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali, Dk. Slaa ataibukia kwenye hoja za maendeleo na kushindwa kwa serikali ya Kikwete kutimiza matarajio ya wananchi.

Kwa mfano, umekuwa utamaduni wa CCM kuwaambia wananchi juu ya kile inachoita maendeleo yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hakika orodha yake huwa ndefu, lakini hakuna jitihada za ndani ya CCM za kuhoji juu ya mafanikio hayo.

Tangu Kikwete aingie madarakani, miaka mitano iliyopita, hali ya uwekezaji nchini imezorota; wawekezaji wengi wamekimbia na Tanzania iliyokuwa inasifika kwa kuvutia uwekezaji imeporomoka katika viwango vya kimataifa vya uwekezaji.

Suala hili linaeleweka vema kwa Dk. Slaa na ana uwezo mkubwa wa kulifafanua kwa wananchi - hawa wa vijijini mpaka wakalielewa.

Mwaka 2005, kabla ya serikali ya rais mstaafu Benjamin Mkapa haijaondoka madarakani, Tanzania ilikuwa nchi ya pili nyuma ya Afrika Kusini, katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini kwa kuvutia wawekezaji.

Lakini leo, Tanzania imeporomoka kutoka nchi ya pili katika ukanda huo, hadi kuwa nchi ya pili Afrika Mashariki.

"Mambo yote haya Dk. Slaa anayafahamu na kwa hakika ataweza kuyaibua wakati wa kampeni, jambo ambalo litaipa CCM wakati mgumu," taarifa zinaeleza.

Suala la ujenzi holela wa shule za msingi na sekondari - hasa za kata - limetajwa na viongozi wengi waliohojiwa kuwa litamletea matatizo Kikwete wakati wa kampeni.

Wakati CCM itakuja na takwimu za vyumba vya madarasa, Dk. Slaa atakuja na takwimu zinazoonyesha kuwa madarasa hayo ni matundu tu; hayana walimu wala vitabu vya kufundishia.

Hali ya shule ambazo CCM inajisifia zimeelezwa na mmoja wa viongozi serikalini kuwa "…si lolote. Ni magenge ya kukusanyia watoto wa masikini. Kule hakuna vitabu, hakuna walimu… pamekuwa kama madanguro ya kutilia mimba watoto."

Karata ya Kikwete itakwama pia juu ya masuala yanayohusu wazee na wenye ulemavu.

"Serikali imewatupa mkono. Karibu hospitali zote za serikali hazina dawa. Wajawazito wanapata shida, hata kama wamesamehewa gharama za matibabu, lakini hakuna dawa wala wahudumu."

Hizi zote ni silaha za kisiasa za Dk. Slaa ambaye ni mjuzi wa kujieleza, kufafanua na kuchambua mazingira na hali za wananchi.

Kwa mara ya kwanza upinzani umepata mmoja wa weledi katika hoja za ufisadi. Ni Dk. Slaa ambaye miaka mitatu iliyopita alitoa hadharani orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi nchini.

Bila woga wala aibu, kiongozi huyo wa upinzani alisema anayepinga orodha hiyo ampeleke mahakamani, lakini hakuna aliyethubutu kufanya hivyo.

Safari hii Dk. Slaa amepata uwanja mpana. Hapa ndipo atafafanua kwa wananchi, wizi kuhusu kampuni ya Kagoga, Meremeta, Deep Green na miradi mingine feki iliyotumiwa kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) na hazina.

"Hapa CCM iko taabani. Njia pekee itakuwa kukimbilia kuiba kura. Lakini hilo nalo si jambo salama kwa kuwa ndani ya chama wenyewe wamegawanyika; wanaibiana kura," ameeleza Filbert Kisungu mkazi wa Temeke Yombo, Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu katika CCM wamenukuliwa wakisema wizi wa kura unaweza kuitumbukiza Tanzania katika machafuko kama ilivyokuwa kwa Kenya.

Mmoja wao amekaririwa akisema, tena kwa sauti ya juu, "Wengine hatutakubali hilo. Hatutakubali kuishi nje ya nchi kwa faida ya wachache," akimaanisha vita vinaweza kuzuka na wengine kulazimika kukimbilia nje ya nchi.

Hoja nyingine kuu ambayo itakuwa ya msaada kwa Dk. Slaa ni kupungua au kukosekana kwa nidhamu katika utumishi wa umma.

"Hofu ya kuwajibika imeisha, ndiyo maana makusanyo ya kodi yamepungua kwa kiwango cha kutisha," ameeleza mmoja wa walioomba ubunge kupitia CCM na ambaye anaonyesha anaweza kuhama chama hicho iwapo ataenguliwa kwenye kinyang'anyiro cha sasa.

Mfumoko wa bei utakuwa mzigo mwingine katika kampeni za Kikwete. Kabla utawala wa Mkapa kuondoka madarakani, mfumuko wa bei ulishuka hadi kufikia asilimia saba, lakini leo umepanda hadi asilimia 14.

Mara baada ya Dk. Slaa kutangazwa kuwa mgombea urais, gazeti la kila siku la Mtanzania linalomilikiwa na Rostam Aziz, lilihusisha uteuzi huo na Kanisa Katoliki.

Gazeti hilo likiripoti taarifa hiyo lilisema kwamba Dk. Slaa amefunga mkataba na Kanisa hilo ili kumfanya kuwa rais wa jamhuri kwa faida yake binafsi. Tayari uongozi wa kanisa umekana madai hayo.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alipoulizwa iwapo Dk. Slaa ni mgombea makini wa urais na kwamna anaweza kumtoa jasho Rais Kikwete alijibu haraka kuwa na chama chake kna mgombea makini.

Makamba alisema, "Hayo ni matusi. Kwangu mini Dk. Slaa siyo makini. Tutakutana kwenye kampeni. Labda ni makini kwako."

Naye Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alipopigiwa simu na kuulizwa anamwonaje mgombea wa Chadema alisema anamfahamu na kwamba "anaweza kushindanishwa" na rais Kikwete.

Alisema kampeni "zinaweza kuwa nzuri." Alikataa kufafanua vipi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: