Makongoro: Tusihofie Shirikisho


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
CHARLES Makongoro Nyerere

CHARLES Makongoro Nyerere, Mbunge mpya wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ametoa ushauri kwamba ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarike zaidi na zaidi ni lazima nchi wanachama ziheshimiane.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na huenda Sudan Kusini ikawa mwanachama wa sita.

“Isije ikatokea nchi moja kuidharau nyingine kwa sababu yoyote ile. Labda, kama vile nchi ile ni ndogo na nyingine kubwa au nyingine ikajifanya ina wasomi wengi na nyingine ina wajinga,” anasema Makongoro katika mahojiano hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

“Hapana, lazima nchi wanachama ziheshimiane,” anasisitiza.

Mwanasiasa machachari huyu anayefuata nyayo za baba yake mzazi, Mwalimu Julius Nyerere anasema ni katika misingi hiyo tu jumuiya itaishi na kufikia malengo yake ambayo akiwa mbunge atasimamia.

Makongoro anasema kiu yake katika kuingia kwenye bunge hilo ni kutimiza ndoto za kuundwa shirikisho la kisiasa kama nchi wanachama zilivyodhamiria.

Shirikisho la Afrika Mashariki, anasema litafikiwa ikiwa Watanzania wataondoa hofu ya kupotea kwa utaifa wao na kupoteza raslimali zao adhimu ikiwemo ardhi.

“Watanzania tuache woga huu. Inajulikana suala la ardhi ni nyeti, ndiyo maana ni ajenda iliyocheleweshwa kiprotokali mpaka angalau kwa sasa,” anafafanua.

Kabla ya kufikia Shirikisho la Kisiasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanzisha protokali kadhaa ikiwemo ya Umoja wa Forodha, lakini suala la ardhi lililomo katika Soko la Pamoja limekataliwa na Watanzania.

Wananchi walioshiriki mjadala kuhusu ardhi kuwemo katika protokali ya Soko la Pamoja, walipinga vikali kwa maelezo, nchi jirani zinaweza kuja nchini na kumiliki maeneo makubwa na kuwanyima haki Watanzania.

Makongoro anasema inahitajika kila nchi mwanachama ielimishe watu wake kuhusu matumizi endelevu ya raslimali ardhi ambayo kwa Tanzania muswaada wa kuifanya ardhi kuwa huru umepelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete.

“Nina taarifa za kuhusu muswaada wa ardhi kuwa sheria katika makubaliano haya kwamba upo ikulu. Mimi naona ni safi kwa sasa mpaka hapo tutakapokubaliana,” anasema.

Hata hivyo anaonya, “Lakini ardhi isiwe kisingizio cha kuzuia shirikisho la kisiasa la Afrika Masharikia. Tunahitaji nguvu moja.”

“Ni muhimu watu wa Afrika Mashariki kuunganishwa kuwa na sauti moja. Sisi wabunge tunakwenda kusimamia malengo ya jumuiya yetu kuifikisha huko,” anasema.

Makongoro, ambaye kabla ya kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwahi kuwa mbunge kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, anasema bunge hilo ni muhimu kwa sababu litasimamia serikali zote tano katika muundo wake na majukumu katika kuimarisha na kupanua mwenendo mzima wa mtangamano ndani ya kanda.

“Hizo ndizo hasa zilizonisukuma kuwania ubunge EALA kuiwakilisha nchi, watu wake na matakwa yao vilivyo katika bunge hilo. Ni zamu yangu kutoa mchango. Sasa ni wakati mwafaka kuona kwamba malengo mawili yaliyosalia ya jumuiya hii yanatimia, ” anaeleza.

Malengo yaliyosalia ni protokali ya Umoja wa Sarafu na Shirikisho la Kisiasa ambalo ndilo kwa muda mrefu limekuwa likisubiriwa.

"Pia naamini kwamba EALA haina budi kuchukua nafasi yake muhimu katika kutunga sheria zitakazoleta manufaa kwa nchi wananchama.”

“Unajua wakati ule walipoanzisha jumuiya hii, Mwalimu na Milton Obote (Rais wa Uganda) walikuwa makini ukilinganisha na Mzee Kenyatta (Jomo),” anasema mwanajeshi huyo wa zamani.

“Sasa ambao hawakuwa na nia njema, walimwangusha Mwalimu kwani hata Mzee Obote naye akapinduliwa kule Uganda na Idd Amin Dada,” anasema. Mwalimu, Kenyata, Obote na Idd Amin Dada tayari wamefariki dunia kwa miaka tofauti.

Baada ya jumuiya hiyo kuvunjika mwaka 1977, miaka 20 baadaye marais Benjamin Mkapa wa Tanzania, Daniel arap Moi wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda walitia saini kufufua jumuiya hiyo.

Mafanikio kiuchumi ya jumuiya yamekuwa makubwa na Makongoro anaamini mafanikio kisiasa yatapatikana iwapo tu kutakuwa na kuaminiana kuanzia viongozi hadi wananchi na kuheshimiana.

Changamoto nyingine aliyotoa ni juu ya usimamizi wa Ziwa Victoria ambalo limeenea nchi za Kenya na Uganda na Ziwa Tanganyika linalounganisha Rwanda na Burundi ili yachangie uchumi endelevu kwa nchi wanachama.

Yapo madai kwamba baadhi ya nchi wanachama zina kampuni ambazo huvuna samaki wengi na kuuza nje bila kuwa manufaa kwa nchi husika. Upande wa Tanzania kampuni hizo hutoa minofu na kusindika kwa ajili ya kuuza nje ya nchi na masazo maarufu kama mapanki ndiyo huliwa na wenyeji.

Kuhusu hilo Makongoro alisema, “Sina taarifa juu ya kampuni kubwa zinazovua samaki na kuuza nje huku sisi tukibaki na wale samaki unaita mapanki.”

Kwa mtazamo wake anasema kwamba kama samaki wapo kwa wingi basi hizo kampuni hazina budi kuweka utaratibu wa kulipa kodi inayolingana na hicho wanachovuna.

“Lakini si kuruhusu tu wavune kiasi kikubwa na chote kupeleka nje. Aah! hapo hapana, lazima wengine wabaki ili tuwale wenyewe,” anasema na kuongeza kwamba kampuni hizo lazima zibanwe ili zilipe kodi inayostahili na nchi wanachama hazina budi kuimarisha miundombinu.

“Maana tunazihitaji kampuni hizi kwa sababu zinatoa pia ajira ambayo ni malengo ya kila nchi,” anasisitiza.

Makongoro alizaliwa 30 Januari, 1959 akiwa mtoto wa tano kati ya wanane kwa mama Maria na Mwalimu Nyerere.

Kwa sasa makazi yake yako kijiji cha Butiama, kitongoji cha Mwitongo wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara. Ameona na ana watoto wane.

Akiwa na umri wa miaka sita tu, alianza kupata elimu ya msingi shule ya Bunge kabla ya kwenda kuhitimu Isike mkoani Tabora mwaka 1972.

Alipata elimu ya sekondari katika shule ya wavulana Tabora kati ya mwaka 1973- 1976 na baadaye elimu ya juu ya sekondari 1977-1978 kabla ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.

Alijiunga na Chuo cha mizinga ya masafa marefu na roketi cha Odessa, Russia alikotunukiwa stashahada kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Aberdeen, Scotland alikofanya stashahada ya mahusiano ya kimataifa.

Alipata uzoefu wa kisiasa tangu alipokuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana akiwa sekondari. Mwaka 1980 hadi 1990, alikuwa Mwenyekiti wa Shina katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania na ilipofika 1995.

Lakini mwaka 1995 aliwashtua wana CCM alipojiunga na NCCR-Mageuzi na alichaguliwa kuwa mbunge wa Arusha Mjini hadi 1997 alipong’olewa.

Makongoro alirejea CCM na mwaka 2007 akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara mpaka sasa.

0
No votes yet