Makundi, chuki vyamvuruga rais Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Makamba adaiwa kuhujumu wenzake
Kutoa kauli tata zilizoleta “kadi feki”

KINYANG’ANYIRO cha ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeibua mengi.

Kimepalilia makundi ndani ya chama; kimejenga ufa kati ya wanachama na viongozi na kimechochea migawinyiko miongoni mwa viongozi na baadhi ya wagombea.

Hii ni kutokana na utaratibu mpya wa kura za maoni uliobuniwa kwa lengo la kumaliza kile kilichoitwa, “mianya ya rushwa ndani ya chama.”

Mkoani Arusha, wanachama watano wa chama hicho wamekamatwa wakiwa na mtambo wa kuchapisha vitambulisho vya wapiga kura vinavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mbali na kukamatwa na vitambulisho vya kupigia kura, wamekamatwa na kadi feki za CCM.

Kimsingi wanachama na viongozi wa chama hiki, wametenda yale ambayo hayajawahi kutokea katika chaguzi zote zilizopita.

Kabla ya utaratibu huo mpya, kura za maoni zilipigwa katika ngazi ya wilaya na hivyo kuifanya rushwa kuishia katika ngazi hiyo.

Lakini utaratibu mpya uliolenga kutoa mwanya kwa wanachama wengi kupata fursa ya kuchagua viongozi wao, haukuleta tija iliyokusudiwa.

Utaratibu umezidisha balaa badala ya neema. Umeongeza ufa miongoni mwa wanachama na viongozi wake na wapo wanaodiriki hata kusema, kwamba “umekiweka uchi chama hiki.”

Hata hicho kinachoitwa malalamiko na rufaa hakiwezi kuleta tija. Hii ni kwa sababu hata miongoni mwa walioshindwa kuna walioshiriki “mchezo wa rushwa.”

Hivyo basi, hatua yeyote ya kubatilisha maamuzi ili kubeba walioshindwa, inabidi kuangaliwa vizuri, hasa katika baadhi ya maeneo.

Bali wengine wanafika mbali zaidi. Wanasema kwa jinsi mchakato ulivyokwenda, “CCM kimebaki na makovu ambayo hayawezi kuzibika.”

Katika maeneo mengi, viongozi wa juu wa chama wametuhumiwa kubeba baadhi ya wagombea. Miongoni mwa watuhumiwa wakuu, ni Yusuf Makamba, katibu mkuu wa chama hicho.

Makamba anatuhumiwa na wenzake katika chama kuvuruga zoezi la uchaguzi, baada ya kuruhusu wanachama wote kupigakura.

Ni kinyume na maelekezo ya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake iliyoongeza sifa ya ziada. NEC ilitaka kila mwanachama wa CCM anayetaka kupiga kura, lazima awe na shahada ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Badala yake, amri ya Makamba ya kuruhusu kila mmoja, ilitumika kuchapisha kadi mpya za chama; kuingiza “wanachama feki” na katika maeneo mengi, rejesta za awali zilifutwa na kuanzishwa mpya.

Sasa inadaiwa kuwa agizo la Makamba lililotolewa siku tatu kabla ya siku ya uchaguzi, lililenga kuangamiza baadhi ya wagombea asiowataka na kubeba “maswahiba zake.”

Anayetajwa kuwa mlengwa wa “mpango wa Makamba” ni mtoto wake, Januari Makamba ambaye alikuwa amekabwa koo na William Shelukindo katika jimbo la Bumburi, mkoani Tanga.

Wala hakuna mashaka, kwamba ufa uliojitokeza sasa, umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kauli na matendo ya Makamba ndani ya chama chake.

Jingine ambalo limesababisha ufa, ni hatua ya CCM kulikabidhi suala la uchaguzi mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kwa kuwa imani mojawapo ya CCM ni kuharamisha rushwa, basi ni jukumu la chama chenyewe kulimaliza jambo hilo.

Lakini ikiwa rushwa imeshinda wenye chama, basi hiyo itakuwa ni dalili nyingine ya chama hicho kufikia ukomo wake wa uongozi.

Ni kwa sababu, uhai wa chama chochote cha siasa duniani, unatokana na ridhaa ya wenye chama. Si kazi ya Takukuru kudhibiti wale wanaokiuka maadili ndani ya vyama vya siasa.

Katika mazingira ambayo Takukuru yenyewe inatuhumiwa kushiriki katika vitendo vya rushwa, upendeleo na ukiukwaji mwingine wa taratibu, haikutarajiwa viongozi wa chama hicho, kujianika mbele ya taasisi hiyo.

Ndiyo maana kila kona kuna malalamiko, kwamba Takukuru ilitumwa kufanya kazi maalum kwa watu maalum.

Madai yametapakaa kuwa ni hao waliokuwa wakiwindwa ambao walishughulikiwa. Wale ambao hawakulengwa, hawakuguswa hata kama walitoa rushwa hadharani.

Tayari uongozi wa Takukuru umenukuliwa ukisema kazi ya kushughulikia wana-CCM wanaotoa rushwa, ni ngumu sana.

Hili lilitarajiwa kwa sababu, Takukuru hawana ubavu wa kudhibiti rushwa kwenye familia za watu binafsi.

Swali la kujiuliza: Je, kura hizi za maoni zimekipa fundisho gani CCM? Jibu liko wazi. Ni kichaka cha rushwa. Kimekosa mwelekeo, kimedorora na kinaweza kupotea kama vyama vingine vikongwe vya Afrika.

Hii ni kwa sababu, rushwa ya mwaka 2005 ni toafuati na hii ya sasa. Katika uchaguzi wa mwaka 2005, rushwa ilianzia ngazi ya wilaya na kuingia hadi ngazi ya taifa.

Lakini mwaka huu, rushwa imeanzia ngazi ya chini ya shina na tawi. Hii hi harufu ya bundi kwa chama kikongwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: