Malipo Dowans ni marafiki wanaolipa marafiki


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version

RAIS wangu tukubali kuwa kikombe cha Babu Mchungaji Ambilikile Mwasapile wa Sumunge, Loliondo kinatibu maradhi mengi kuliko aliyoyataja na anayoyafahamu.

Waliopata kikombe wamepata ahueni ya maradhi yao na sasa wanaendelea kuishi kama wenye afya njema ingawa hatujui hatima yao itakuwaje!

Ujio wa kikombe cha Babu umewafanya watu wote kupatwa na ganzi na kusahau sakata la kampuni ya Dowans kulipwa mamilioni ya shilingi.

Hakuna anayezungumzia tena malipo ya kampuni hiyo; si serikali wala wananchi. Hata wale waliojitia ‘fyatu’, wamekuwa kimya kabisa.

Serikali nzima ya awamu ya nne imehamia Samunge, kifikra na kimwili. Imejizatiti kuimarisha kikombe hiki cha kiimani na hivyo kupata muda wa kupumua hata kama ni kwa taabu. Barabara inajengwa. Mjini giza kijijini, umeme wa jua!

Dowans haikuwa mchezo. Iliiweka serikali ya awamu ya nne katika maji ya shingo ikawa imebaki imesimamia ncha za vidole vyake vya miguuni.

Kama viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wangeendelea na kashikashi yao bila kupoozwa na kikombe cha Babu, leo hii nina hakika tungekuwa tunazungumza mengine.

Malipo ya Sh. 94 bilioni kwa Dowans yaliitikisa nchi. Sababu za kuitikisa nchi mtu hawezi kuzieleza akaeleweka vizuri mbele za watu wasio timamu naye asifikiriwe hamnazo au amenunuliwa. Lakini mtu mwenye haki hutumia haki bila kujali wengine watasema nini juu yake.

Hatujui yanayoendelea serikalini baada ya kupata unafuu huu wa shinikizo. Lakini sitashangaa baada ya watu kurejea kutoka Samunge wakakuta stakabadhi zinazoonyesha kuwa Dowans wamekwishalipwa. Ishara ni hizi, mitambo hiyo inadaiwa imenunuliwa na kampuni ya Symbion Power ya Marekani.

Tuachane na Symbion Power. Dowans wakilipwa sitalia! Kuna watu wanadhani Dowans wasipolipwa vidonge vitaongezeka katika hospitali zetu au utapatikana unafuu wowote katika elimu na huduma za jamii. Vivyo hivyo, Dowans wakilipwa hakuna kitakachopungua.

Rais wangu, uliposema, “Lazima ieleweke kuwa tukishaamua jambo kwa pamoja wizarani au katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wetu sote hata kama wewe ulikuwa na mawazo tofauti, wote tunao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea… hatutegemewi kuendelea kuupinga baada ya hapo. Kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja” ulijipambanua vizuri.

Kwa kauli hii, ni dhahiri umekiri mambo mawili makubwa. Kwanza, ni kweli kwamba suala la mkataba tata wa Richmond lilijadiliwa katika vikao vya baraza la mawaziri na hivyo kila kilichotokea ulikifahamu.

Pili, umedhihirisha jinsi ulivyojiimarisha katika kuhakikisha unaona Dowans. Ni kutokana na kauli yako kwamba “niseme nini, alichosema waziri mkuu ndiyo hichohicho.”

Waziri mkuu Mizengo Pinda alisema, “Inauma sana, lakini sharti kwa hali inavyokwenda Dowans ilipwe.”

Hilo likifanyika, aliyekuwa Sipika wa Bunge Samwel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti Kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond, lazima watuambie, kwa nini walishinikiza serikali kuvunja mkataba na Dowans kama hawakujua kuwa Dowans ndiyo Richmond?

Kama hivyo ndivyo mwenye Dowans atakosaje kuwa ndiye mwenye Richmond? Kwa nini Watanzania wasiichukulie kauli ya rais wao ya kuikana Dowans na wamiliki wake kuwa ni kauli ya kutaka kuonyesha kuwa Dowans siyo yake? Lakini hoja ya kuonyesha kisicho chako kuwa siyo chako inatoka wapi?

Duniani kote heshima ya kiongozi yeyote iko katika uadilifu wake kwa matendo. Ikitokea duniani, mkuu wa nchi akasema kuwa pamoja na vyombo vyote vya intelijensia – usalama wa taifa, polisi, mgambo na sungusungu – haijui kampuni inayokamua uchumi wa wananchi wake kila mwezi, utakuwa uthibitisho wa jinsi nchi hiyo ilivyokosa kiongozi makini.

Wanaopiga kelele kumtaka Rais wangu aachane na marafiki zake, watambue kuwa hawana haki kwa hilo. Walikotoka hawajui. Walichofanya pamoja hawajui.

Mtu anayetajwa kuhusika na Dowans, Rostam Aziz na Rais wangu hawakukutana barabarani. Waelimisheni wananchi ni kwa vipi serikali ya Rais wangu itakapoilipa Dowans, malipo hayo hayatawanufaisha marafiki wa Rostam, akiwemo Rais wangu. Kwani wanaolipa ni nani na wanaolipwa ni nani? Si marafiki wanalipa marafiki au ni marafiki wanalipwa na marafiki?

Rais wangu, kwakuwa Fred Mpendazoe amesema Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe walikusaliti wewe na chama chako, ukiilipa Dowans na wao wakaukosa urais wa 2015 huku ukiwa umeshindwa kumfukuza Edward Lowassa kutoka CCM watakuona na wewe umewasaliti.

Uhasama wenu utadumu kwa muda mrefu. Heri uhasama huu kuliko ule wa marafiki zako ambao wakati mnafanya mema mlikuwa pamoja na hata mlipomtumikia shetani mlishirikiana. Mbaya zaidi hata familia zenu zinajua kuwa ninyi ni marafiki, hawa wakuja wametokea wapi?

Leo Watanzania wanajua kuwa Bunge lilipotoshwa na kamati ya Dk. Mwakyembe. Ripoti yake ilikuwa ndefu lakini haikumtaja mwenye Richmond.

Bunge na wananchi waliaminishwa kuwa Richmond ililetwa au ilikuwa mali ya Rostam. Naye alipohisi hivyo akaomba mwenye Richmond atajwe bungeni, lakini Sitta kwa sababu binafsi akakataa.

Bunge kwa mamlaka ya Spika liliwaficha Watanzania na taifa kwa ujumla mhusika mkuu wa sakata la Richmond. Likawaacha waanze kukisia watu mbalimbali hata wengine ambao sio. Baadhi wakadai ni ya Rais, wengine wakaamini ni ya mwanaye lakini hakuna aliyeweza kuthibitisha.

Dowans ilikuja nchini kama mvua ya kiangazi. Mvua ya kiangazi haina mawingu. Unapoanza kujiuliza mvua imetoka wapi, utakuwa umekwishalowa na mvua imeshakatika.

Kipande cha serikali kilichonusurika kuvunjika mwaka 2008 (baada ya Lowassa kujiuzulu) kwa ukweli uliofichwa na Dk. Mwakyembe kiwaambie Watanzania, Dowans ilishinda lini zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura Tanzania.

Kampuni moja ikishindwa zabuni si inatangazwa upya? Toka lini zabuni ikarithiwa kutoka kampuni nyingine? Kwanini baadhi ya wafanyakazi na njia za mawasiliano zilibaki zilezile na kumhusisha mtu yuleyule aliyehusishwa na umiliki wa Richmond?

Kwa nini Dk. Mwakyembe na Sitta walikishinikiza kipande cha serikali walichokinusuru kuvunja mkataba wa Dowans kama hawakujua kuwa Dowans ndiyo Richmond?

Je, siyo kweli kuwa kipande cha serikali kilichoileta Richmond ndicho kilichoileta Dowans? Yakijibiwa maswali haya kwa uhakika, Watanzania watajua kuwa Richmond na Dowans ni kitu kimoja majina tofauti. Vipi Symbion Power?

Hata kama Dk. Mwakyembe hataki kueleza wananchi kile alichokificha, wananchi wanajua ukweli, kwamba mwenye Richmond ndiye mwenye Dowans; yu miongoni mwa kipande cha serikali kilichonusuriwa kwa hatua yake ya kuficha ukweli.

Serikali iliporomoka yote, alibaki Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais wa wakati ule Dk. Ali Mohamed Shein.

Tuwe wajasiri wa kutamka kuwa Dowans lazima italipwa kwa sababu wahusika ni walewale – ni marafiki wanaolipa marafiki. Wakiwa serikalini watakuwa walipaji, wakiwa katika umiliki watakuwa walipwaji.

Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatika kwa simu Na. 0713334239, emaili ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: