Malipo ya Salma utata


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Salma Kikwete

MALIPO kwa ajili ya safari za Mama Salma Kikwete, anayetumia ndege za serikali kwa safari binafsi, yameibua utata mpya, MwanaHALISI limegundua.

Taarifa zilizofikia gazeti hili zinaonyesha ama hakuna malipo yanayofanywa na CCM au yanafanywa lakini hayaeleweki yanatawaliwa na kasma ipi.

Utata huo umeibuka wiki moja tangu Abdulrahman Kinana, meneja wa kampeni wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), awaambie waandishi wa habari kuwa safari za Salma zinalipiwa na chama chake.

Kwenye Hati ya Madai ya tarehe 14 Septemba mwaka huu, inayodaiwa kutolewa na Mamlaka ya Ndege za Serikali (TGFA) kwa CCM, inaonyeshwa kuwa kasma (vote) inayotawala fedha za mamlaka ni Na. 062.

Lakini kasma inayotajwa haimo katika vitabu vya bajeti vya mwaka huu wa fedha (2010/2011).

Upekuzi makini katika vitabu vyote vinne vya bajeti, haukufanikiwa kuona kasma Na. 062 inayotajwa kwenye hati za madai zilizokaguliwa na mwandishi wa gazeti hili.

Hati zilizokaguliwa ofisini kwa Kinana, Mtaa wa Ohio, ni Na. 00868727 ya tarehe 31 Agosti 2010 inayodai dola za Kimarekani 15,000 na nyingine Na. 00867609 ya 14 Septemba 2010 inayodai Sh. 22,950,000 zote zikionyesha kasma Na. 062.

Vitabu vya bajeti ambavyo mwandishi alipekua ni pamoja na Makadirio ya Mapato (Financial Statement and Revenue Estimates) na Makadirio ya Matumizi ya serikali (Estimates of Public Expenditure Consolidate Fund Services and Supply – Ministerial – Vote).

Vitabu vingine ni Makadirio ya Matumizi – mikoa (Estimates Expenditure Supply Vote – Regional) na Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo (Public Expenditure Estimates Development Votes).

Katika vitabu vyote hivyo hakuna palipoonyeshwa kasma Na. 062 ya wakala wa ndege za serikali.

Ofisa mmoja wa wizara ya fedha ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema ni kweli kasma hiyo na kasma ndogo Na. 1817 zinazotajwa kwenye hati ya madai hazimo katika vitabu vya bajeti.

Amesema katika mazingira hayo, “siyo rahisi kujua malipo yanavyofanyika, kwani fedha inayolipwa kupitia serikali kuingia wakala au kutoka wakala kwenda nje, sharti ionyeshwe inatoka kasma ipi.”

Wakala wa ndege uko chini ya Wizara ya Miundombinu ambayo kasma yake ni Na. 98.

Katika hali ya kawaida, kasma ya wakala ingekuwa chini ya wizara mama au wizara ya fedha ambayo kasma yake ni Na. 50. Lakini haipo popote.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa (TGFA) na Rubani Mkuu, Kennan Mhaiki, amesema kwa kadri anavyofahamu, wakala hiyo iko chini ya wizara ya miundombinu.

Alipoulizwa ni ipi kasma ya wakala wake, alisema anachojua ni kwamba wapo chini ya Miundombinu, basi.

Alipoambiwa kuwa kasma iliyoonyeshwa, Na. 062 ndiyo ya wakala wake, Mhaiki amesema mambo ya bajeti yanashughulikiwa na watu wengine na kuhusu kiasi kilicholipwa na CCM amesema “hayo ni mambo ya serikali na siwezi kuzungumza kila kitu.”

Kwa mujibu wa hati ya madai ya 14 Septemba, CCM inadaiwa dola 3,000 kwa saa (sawa na Sh. 22,950,000) kwa safari ya Salma ya Jumapili, 12 Septemba 2010.

Hati inaonyesha kuwa ndege ilikodishwa kwa saa tano tu na kuonyeshwa kwamba inakwenda Mwanza na kurudi (DAR –MZ-DAR). Lakini ndege hiyo ilitua Musoma saa 8.05 alasiri.

Kwa hesabu ya haraka, kila saa moja iligharimu Sh. 4,600,000 pamoja na kutoa mji ambao haukutajwa kwenye hati ya madai.

Mtoa taarifa wa gazeti hili amethibitisha kuwa ndege iliyompeleka Salma Musoma, iliondoka yapata dakika 40 mara baada ya kutua.

Haikufahamika iwapo mabadiliko ya njia yalifahamishwa kwa waoangoza ndege ambao huwasiliana na marubani juu ya hali angani na abiria waliowabeba.

Mfanyakazi mmoja wa uwanja wa ndege ameliambia gazeti hili kwamba anapokuwemo Salma, marubani huwa wanasema, “On board, on board, First lady, first lady!” – kwa maana kwamba wamebaba mke wa rais.

Kinana alimwambia mwandishi huyu kwamba tayari CCM imelipa Sh. 139,995,000 kwa wakala na kwamba wanalipa mara kwa mara. Fedha hizo zililipwa kupitia benki ya CRDB.

Alipoulizwa iwapo fedha anazolipa zinafika kunakohusika, Kinana alisema, “Ninachoweza kusema ni kwamba fedha tumelipa na zimeingia serikalini. Suala kwamba kasma Na. 062 haipo katika vitabu vya bajeti, mimi silijui.”

Wiki iliyopita mwanasheria mashuhuri nchini, Mabere Marando alisema amepokea maombi kutoka kwa watu binafsi na asasi za kijamii, vikimwomba kufungua kesi dhidi ya Mama Salma kwa “matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma.”

Alisema Mama Salma anatuhumiwa na wateja wake kwa kutumia magari na “usafiri mwingine wa serikali, ikiwamo ndege, kuzunguka nchi mzima kumfanyia kampeni mumewe,” ambalo ni suala la binafsi. Aliahidi kumburuza mahakamani.

Ofisa wa bunge aliliambia MwanaHALISI kuwa kasma Na. 062 iliyotajwa na wakala ilikuwa katika vitabu vya bajeti vya mwaka 2006.

“Ilikuwa inatumiwa na kamisheni ya mawasiliano iliyokuwa chini ya wizara ya mawasiliano na uchukuzi. Kasma hiyo hivi sasa imefutwa,” ameeleza.

Amesema iwapo serikali itakusanya na kutumia fedha nje ya kasma iliyo wazi na chini ya wizara husika, kuna uwezekano mkubwa wa fedha hizo kuingia katika mifuko isiyohusika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: