Mama Salma Kikwete: Kitanda cha ikulu kina kunguni?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Gumzo

MKE wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, ametonesha wengi. Ni pale alipokumbusha yaliyomkuta alipokwenda hospitali kujifungua mtoto wake wa kwanza.

Alisema alipofika katika hospitali hiyo ya serikali, wauguzi walimlaza sakafuni. Walimdharau na walimuona kama mtu asiyekuwa na thamani.

Alisema, “Sitasahau kamwe hali niliyokutana nayo wakati ule nilipokwenda kujifungua mtoto wangu wa kwanza katika hospitari ile ya serikali. Kwa kweli, nilinyanyasika sana.”

Hata hivyo, Mama Salma hakutaja jina la hospitali alikosema alikwenda kupata huduma ya uzazi. Hakutaja jina la muunguzi aliyesema alimdhalilisha kwa “kiwango cha kusikitisha.”

Alichosema ni kuwa wakati hayo yanamkuta, mumewe Rais Kikwete alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa; yeye alikwenda katika hospitali hiyo kama mtu wa kawaida.

Alisema kilichomsaidia kupunguza machungu, kujibiwa vizuri na kuhudimiwa tofauti na wenzake, ni pale wauguzi walipotambua kuwa yeye ni “mke wa waziri Kikwete.”

Mama Salma alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, alipokuwa akizungumza na wauguzi wa hospitali ya Mbuzii, wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Alitoa wito kwa wauguzi kuacha tabia ya kunyanyasa wagonjwa ili wanawawake wengi waweze kujifungulia hospitali. Alisema kitendo cha wauguzi kutoa lugha chafu, kinakatisha tamaa wagonjwa.

Alichokutana nacho Mama Salma kabla ya mumewe kuingia madarakani, tena akiwa waziri muhimu katika serikali, bado kinatendeka hadi sasa.

Karibu katika hospitali zote za serikali, madaktari, wakunga na hata manesi, wamekuwa wakituhumiwa kunyanyasa wagonjwa, kuchukua rushwa na kutenda kazi kinyume cha taratibu.

Hata hivyo, ukweli una baki palepale, kwamba matatizo mengi yaliyopo katika hospitali za umma, yamesababishwa na watawala.

Wala Mama Salma hawezi kusema kuwa haya yamekuja kwa bahati mbaya au yamesababishwa na ubinafsi wa wakunga. Matatizo mengi katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya hadi zile za mkoa na rufaa, yametokana na serikali kushindwa kuziboresha hospitali zake za umma.

Kwa mfano, nani asiyejua kuwa mkunga mmoja anayefanya kazi katika hospitali ya serikali anahudumia karibu wagonjwa 40 kwa siku? Si hivyo tu, hospitali hizo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa, vitanda na chakula.

Baadhi ya hospitali, zikiwamo zile za jijini Dar es Salaam – Mwananyamala, Amana na Temeke – mkunga mmoja anaingia kazini saa kumi na mbili jioni na anatoka saa moja asubuhi.

Humo utasikia, mama mjazito huyu analalamika, “nesi naumwa.” Mwingine anasema, “nesi njoo unisaidie.” Huku wengine wakiwamo wale waliofurika hadi kwenye sakafu, wakilalamika na kutaka msaada wa muuguzi, kana kwamba muuguzi huyo anatumia mafuta kuzunguka.

Je, katika mazingira haya ya uchovu wa mkunga; mazingira ya kukosa fedha ya kununua kitumbua; mazingira ya kutokujua wanawe wanakwenda vipi shule na watakula nini; mkunga au mganga atapata wapi nguvu ya kujibu kwa sauti ya unyenyekevu?

Katika mazingira ya mganga au nesi kushindwa kufahamu wapi atapata fedha ya kodi ya nyumba, kutojua nauli ya basi itatoka wapi – yake na familia yake; mganga au muunguzi anawezaje kutoa huduma inavyotakiwa wakati kichwani kumejaa shehena ya matatizo?

Nani asiyejua kuwa wafanyakazi hawa wamo katika mazingira magumu na hatarishi, huku wakilipwa ujira kiduchu usiyokidhi mahitaji ya wiki moja?

Tatizo hili la uhaba wa vitendea kazi limezikumba hospitali zote nchini, ikiwamo ile inayoitwa, “hospitali ya taifa Muhimbili.” Ni katika hospitali hiyo inayoitwa ya rufaa wagonjwa wanalala hadi chini.

Watumishi hawa wa serikali wanaotakiwa na Mama Kikwete kuwa na lugha nzuri, serikali haijawahakikishia usalama wao kazini. Hawana bima za maisha au zile za ajali; hawana hata uhakika wa kulipwa mafao yao kwa wakati pale wanapomaliza mikataba yao ya kazi.

Kuna hili pia. Katika mazungumzo yake na waauguzi hao, Mama Salma amenukuliwa akisema “wanawake wote wana thamani sawa.”

Hata hivyo, kauli yake hiyo inakinzana na ukweli halisi. Kwanza, kama wanawake wote ni sawa, mbona yeye alipotambuliwa na daktari kuwa mke wa Kikwete alikubali kuacha wenzake wamelala chini?

Kama wanawake wote wana thamani sawa, kwa nini hakuwaonea huruma wenzake ambao aliwakuta wamelazwa sakafuni, badala yake alikubali kunyanyuka na pengine hata kuondolewa mmoja wa wagonjwa ili kupisha mke wa mheshimiwa? Uko wapi usawa anaodai kuupigania?

Kama yeye aliyenyanyaswa kiasi hicho hivi sasa ni First Lady, amefanya nini kupitia nafasi yake kuokoa wanawake wenzake? Je, anadhani kuhubiri huko kwamba alinyanyaswa kunatosha?

Anaposema, “Mimi mwenyewe yamenikuta haya…” alikuwa anakusudia nini? Kwamba haya ni mambo ya kawaida yanaweza kumpata mtu yeyote, na hivyo hakuna njia ya kuyazuia?

Kama Mama Salma anapigania usawa na haki za wanawake wenzake, amechukua hatua gani kumueleza mumewe, ambaye tayari chama chake kimepanga kuteketeza mamilioni ya shilingi kumrudisha madarakani?

Je, amemueleza kuwa heri fedha hizo zingetumika kujenga wodi za wazazi na kununua vitanda katika hospitali zetu, kuliko kuzitapakanya kwa kujinadi?

Hakika malalamiko ya First Lady hayawezi kusaidia nchi wala wananchi wa kawaida. Yanaweza kuwa yamelenga kumsaidia Kikwete kulinda urais wake.

Ilitarajiwa Mama Salma atumie kumshauri mumewe vipaumbele ambavyo vinatakiwa kutekelezwa na serikali, badala ya kutumia fedha nyingi kwa safari zenye tija haba.

Angesema kwa mfano, gari moja la kifahari aina ya “shangingi” linalokadiriwa kufikia zaidi ya Sh. 80 milioni linalonunuliwa na serikali ya Kikwete, linatosha kujenga wodi mbili au zaidi zenye uwezo wa kuchukua vitanda 60 kila moja.

Kwamba tukifunga mikanda kwa mfano huo, matanga yataisha mapema. Wananchi wataipenda serikali yao na watakuwa wanafaidi matunda ya uhuru wao.

Mama Salma lazima afahamu kuwa serikali makini, lazima iwe na vipaumbele sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Haiwezi kuwa na vipaumbele vya kuzunguka nchi au mataifa kama vile ikulu kuna kunguni.

Kuna mantiki gani ya kununua mashangingi kwa mabilioni ya shilingi, tena kwa matumizi ya watu wachache serikalini, huku serikali inashindwa kujenga wodi na kununua vitanda vya wagonjwa hadi kusababisha wengine kulazwa chini?

Itakuwa heshima kuu kwa Mama Salma, hasa kwa kuwa anapozunguka ndani na nje ya nchi anatumia rasilimali za taifa, kusaidia serikali kuondokana na ufukura wa fikra na uzembe wa kufikia kushindwa hata kutibu wananchi wake.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: