Mama wa Masha kortini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

MAMA mzazi wa Lawrence Masha, waziri wa mambo ya ndani na mgombea ubunge wa jimbo la Nyamagana, Mwanza, yuko hatarini kuburuzwa kortini kujibu tuhuma za kutoa ushahidi wa uongo katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza.

Taarifa zinasema Laura Masha alitoa ushahidi wa uongo mahakamani, katika kesi ya mirathi iliyofunguliwa na Wiebke Gaetje ambaye anatoka Ujerumani na mtoto wake Mark Alexanda Gaetje.

Wiebke Gaetje ni mjane wa Klaus Gaetje ambaye anatoka Ujerumani. Klaus Gaetje alikuwa mfanyabiashara mkoani Mwanza. Alifariki katika mazingira ya kutatanisha Julai 2004 huko Port Bell, nchini Uganda.

Taarifa zilizothibitishwa na Mark zinasema tayari mahakama ya rufaa nchini imetupilia mbali utetezi pamoja na ushahidi uliowasilishwa na Laura.

Laura alitoa ushahidi katika kesi iliyofunguliwa mwaka 2008 na Mark Gaetje ambaye kwa sasa anaishi Uholanzi.

Mvutano ulifuatia hatua ya Brigitte de Floor, kugushi baadhi ya nyaraka ikiwamo cheti cha ndoa na wosia kwa lengo la kujimilikisha mali.

Tarehe 3 Oktoba 2010, Mahakama ya Rufaa, chini ya uenyekiti wa Jaji Mbwana, ilikubaliana na maombi ya wadai Wiebke Gaetje na Mark Alexanda Gaetje, kwamba Brigitte de Floor hakuwa mke halali wa Klaus Gaetje.

Cheti cha ndoa kinachodaiwa kugushiwa ni Na. E 087887 kinachoonyesha kuwa kimetolewa 10 Oktoba 1999 wilayani Magu, mkoa wa Mwanza. Kimesainiwa na Msajili Msaidizi wa Ndoa, Anthony Jakonyango.

Laura alidai kuwa alishuhudia Jakonyango akifungisha ndoa hiyo wilayani Magu. Jakonyango alikuwa Katibu Tawala wa wilaya hiyo.

Hata hivyo, katika hati yake ya kiapo ya 5 Julai 2008, mbele ya kamishina wa viapo, Elias Kitwala, ambayo gazeti hili lina nakala yake, Jakonyango alikana kufungisha ndoa hiyo.

Anasema, “Mimi nilihama Magu, 20 Mei 1999 kwenda Bukoba, mkoani Kagera. Hivyo kwa vyovyote vile, nisingeweza kufungisha ndoa Magu tarehe 10 Oktoba 1999.”

Jakonyango anasema cheti cha ndoa anachodaiwa kusaini siyo halali.

Klaus Gaetje na Wiebke Gaetje walifunga ndoa tarehe 12 Oktoba 1979 nchini Ujerumani na kuzaa mtoto mmoja wa kiume, Mark Gaetje (28). Mtoto huyo na mama yake wanalalamikia Masha kushirikiana na Brigitte de Floor kutapanya mali yao.

Gaetje anadai kuwa kampuni ya uwakili ya Masha, IMMMA Advocates, imehusika katika kushughulikia baadhi ya nyaraka ambazo zimesaidia “kupora mali” ya marehemu mume wake.

Miongoni mwa mali ambazo Masha anatuhumiwa kusaidia Brigitte de Floor kupora ni vivuko vitatu, viwanja vinne na “baadhi ya magari ya kampuni.”

Vivuko vinavyohusika ni Kamanga, mv Uzinza na mv Karumu. Vyote viko katika eneo la Kamanga mkoani Mwanza.

Taarifa zinasema tayari mipango ilikuwa inasukwa ili kumpatia mama huyo kibali cha kuishi nchini ili kuendeleza kile kinachodaiwa na Wiebke, “urafiki wa damu na waziri Masha.”

Anasema, “Ninajua ukaribu wa familia ya Masha na de Floor. Baba yake Masha amekuwa akipewa misaada na de Floor. Tayari ameipa familia hiyo viwanja vinne ambavyo ni mali ya mwanangu.”

Waziri Masha mara kadhaa alituhumiwa na Wiebke Gaetje kuwa kikwazo katika upatikanaji wa urithi wa mume wake, lakini mwenyewe amekuwa akikana madai hayo.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: