Mambo magumu kwa AFC, Majimaji, Lyon


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

TIMU nne za soka kati ya 12 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara zinapumua kwa shida; tatu Zitashuka hadi daraja la kwanza mwishoni mwa msimu.

Ruvu Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Ruvu mkoa wa Pwani, African Lyon ya Dar es Salaam, na timu mbili za wananchi, AFC ya Arusha na Majimaji ya Songea, zina hali ngumu katika msimamo.

Makocha wamejitahidi kufanya marekebisho katika safu zao, lakini kila zinapoingia dimbani hupokea kipigo na kuendelea kukaa chini ya mstari wa kushuka daraja.

“Tunafanya marekebisho, tuna uhakika mechi zijazo tutacheza vema,” alisema Kaimu kocha mkuu wa Majimaji ya Songea, Peter Mhina. Timu hiyo imepanga kuongeza nguvu kwa Kumchukua Razak Ssiwa aliyewahi kuinoa Yanga.

Ssiwa ambaye amewahi kuwa kocha wa makipa Yanga na Harambee Stars ndiye anatarajiwa kuwa chachu ya Majimaji inayosubiri miujiza kubaki katika Ligi Kuu.

Majimaji ilianza kwa kuchechemea kabla ya kuibuka na kushinda mechi mbili na kutoka sare mmoja kati ya tisa. Ina maana imekubali vipigo sita. Ni hatari.

Katika mechi hizo ilizoshuka dimbani, imefunga mabao mawili tu huku ikichapwa saba hivyo ina deni la mabao matano. Inashika nafasi ya 11 juu kidogo ya vibonde AFC.

AFC iliyowahi kutamba ngazi ya Ligi Kuu ya Bara ilishuka daraja misimu mitatu iliyopita. Timu Hiyo ilijiuliza na kuchanga vema karata zake na ikafanikiwa kurejea Ligi Kuu.

Hakuna ubishi mwenendo ilionao sasa inaelekea kule ilikotoka.

Katika michezo tisa iliyocheza, imeweza kuvuna pointi tano tu baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo miwili. Hatari yake ni kwamba tayari

imejiruhusu kukaa mkiani kwa muda mrefu baada ya kukubali pia kufungwa mabao 12 na kufunga manne, hivyo kutengeneza deni la mabao nane.

Ruvu Shooting, pia ilirejea kwenye Ligi Kuu baada ya kushuka misimu miwili iliyopita. Wenzao wa JKT Ruvu, wanafanya vema kwani wamekutana na vipigo kutoka kwa vigogo tu.

Timu hiyo ambayo iko nafasi ya 10 kutokana na pointi nane ilizojikusanyia, imeshinda mechi mbili na kutoka sare mbili lakini imepokea vipigo vitano.

Shooting inayozikalia AFC na Majimaji, imefunga mabao matano na kufungwa manane hivyo kuwa na deni la mabao matatu.

African Lyon ambayo ilikuwa tishio ilipomilikiwa na Mohamed Dewji, nayo inaonekana kupoteza mwelekeo kwani iko nafasi ya tisa.

Imeshinda mechi mbili, sare tatu na kuweka kibindoni pointi tisa. Hata hivyo, imepachika mabao saba na kukung’utwa 11 hivyo kuwa na deni la mabao manne.

Wakati ligi imebakiza mechi mbili kila timu kukamilisha mzunguko wa kwanza AFC, haiwezi kujinasua hata kama itashinda zote, labda iombee Majimaji, Ruvu Shooting na Lyon zifungwe.

Mabadiliko yoyote katika matokeo ya vibonde hivyo vine yanaweza kuziweka mahali pabaya JKT Ruvu, Toto African na Polisi Dodoma zenye pointi 12 kila moja huku zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa mara nyingine, kinyang’anyiro cha nafasi za juu kinaonekana kwenda kwa Simba, Yanga, Azam FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.

Simba na Yanga zimefikisha pointi 21 lakini Wekundu wa Msimbazi walioshinda mechi saba na kufungwa mbili wamepachika mabao 14 na kufungwa saba wakati vijana wa Jangwani wamefunga mabao 10 na kufungwa moja.

Japokuwa ligi bado ndefu, lakini Azam, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar zinaelekea kujihakikishia nafasi ya kubaki Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa mapendekezo mapya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu tatu zitashuka daraja halafu tano zitapanda kufanya ligi hiyo kuwa na timu 14.
Mwaka 1995 ilipokuwa Ligi Daraja la Kwanza chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilikuwa na timu 12. Mwaka 1996 ilipopandishwa hadhi kuwa Ligi Kuu ilikuwa pia na timu 12.

Timu ziliendelea kupanda hadi zikawa timu 24 ambazo zilikuwa zinacheza katika makundi na hatua ya pili ikawa inachezwa Ligi Kuu ya Nane Bora. Lakini baadaye timu zilipunguzwa na kufikia 12.

TBL walijitoa baada ya kushurutisha Ligi Kuu ya Nane Bora iwe inashirikisha timu sita tu. Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom iliyonufaika na kujitoa kwa TBL haijatoa maoni yake namna itakavyoweza kudhamini ongezeko la timu.

Udhamini, ndio pekee unasaidia timu zisizo na fedha ili ziweze kufika katika kila kituo cha mechi Tanzania Bara. Hebu tazama msimamo huu mpya.

0
No votes yet