Marekani inafanya dhihaka?


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi
KEJELI, utani au ndio njia ya "wakubwa kuwasiliana?"
Rais Jakaya Kikwete

Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutetea safari zake nje ya nchi, ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa inayoelezea vigezo vya nchi kupata msaada. Havihusu safari za wakuu wa nchi.

Akijibu swali la aliyetaka kujua umuhimu wa safari zake za mara kwa mara nje ya nchi, Rais Kikwete alitoa mifano kadhaa na kusema baadhi ya misaada ya fedha isingepatikana bila yeye kufanya ziara.

Miongoni mwa misaada ambayo rais alisema ni pamoja na ule wa Marekani chini ya Mradi mkubwa wa Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation – MCC).

Rais alitoa maelezo hayo tarehe 9 Septemba mwezi huu na ubalozi ukatoa maelezo kesho yake, tarehe 10.

Mradi wa MCC ulitoa dola za Marekani 11.5 milioni kwa Tanzania kupambana na rushwa na kujenga utawala bora.

Vilevile chini ya mradi huu wa MCC Marekani ilitoa mwaka juzi dola 700 milioni zilizosainiwa na Rais George Bush alipotembelea Tanzania.

Misaada hii kutoka MCC ni kwa nchi ambazo utawala wake unamulikwa na kufuatiliwa iwapo zinafanya vizuri katika utawala bora (kwa viwango vya Marekani).

Imelenga kuzivusha nchi hizo kutoka kiwango cha chini ili ziweze kufuzu kupata misaada zaidi ya uhakika pale zitakapoonekana zimejitahidi na zimeonyesha kupiga hatua.

Katika taarifa yake ya 10 Septemba 2009, bila kuonyesha kwamba unahusisha maelezo ya Rais Kikwete, ubalozi wa Marekani ulieleza kwa ujumla tu, kuhusu nchi zote duniani, ikiwamo Tanzania, zinavyopaswa kuzingatia vigezo vya kupata fedha za MCC, hata kama tayari fedha hizo zimeanza kutolewa kwa awamu.

Kwa mujibu wa maelezo ya ubalozi, safari za viongozi haziwezi kusaidia kupandisha vigezo hivyo au kusababisha kupatikana kwa fedha kutoka mradi wa MCC.

Kwa mfano Februari 2008, MCC iliingia mkataba wa dola za Marekani 700 milioni kwa ajili ya kusaidia sekta mbalimbali nchini baada ya Tanzania kutimiza sehemu kubwa ya vigezo 17 vilivyowekwa na bodi ya mradi huo mkubwa wa kusaidia nchi changa duniani.

Vigezo vinavyotumiwa na MCC na taasisi nyingine za kimataifa katika kutoa misaada na mikopo, ni pamoja na kigezo kikuu cha utawala bora na uwajibikaji, mambo ambayo yalisisitizwa katika taarifa ya ubalozi ya 10 Septemba.

Vigezo vingine ni uhuru wa kiraia, haki za kisiasa, ubora wa utendaji serikalini, kanuni za kisheria, udhibiti wa rushwa, viwango vya chanjo, kuwekeza kwa watu, na matumizi ya fedha katika sekta ya afya.

Vingine ni viwango vya wanafunzi wa kike wanaomaliza shule za msingi, matumizi ya fedha katika shule za msingi, mfumko wa bei, sera za biashara, ubora wa mifumo ya usimamizi wa miradi, usimamiaji wa maliasili na haki katika kumiliki ardhi.

Taarifa za nchi kufikia vigezo hivyo zimekuwa zikipatikana kutoka kwenye taasisi za kimataifa ikiwamo Benki ya Dunia (WB) na Umoja wa Mataifa (UN).

Kwa njia hii, ziara za rais hazina uhusiano wa moja kwa moja na misaada na hazina uwezo wa kubadili au kurekebisha vigezo vya wafadhili, ukiwemo mradi wa MCC.

Taarifa ya Ubalozi, iliyotolewa siku moja baada ya maelezo ya Rais Kikwete, ikinukuu kauli ya bodi ya MCC, haikuitaja Tanzania. Ilielekeza maelezo yake kwa nchi zote zinazopata msaada wa MCC (ikiwamo Tanzania).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao cha Bodi cha MCC, mara baada ya kuzuru Afrika, alikofanya mazungumzo na viongozi wa Cape Verde na Kenya, ambako wananufaika pia na fedha kutoka MCC.

Lakini pia alifanya mazungumzo na viongozi wa Liberia kwa kuwa wao ndio kwanza wanaandaa mpango wa kujiunga na MCC.

Taarifa ya ubalozi ilisema, “Bodi ya Wakurugenzi ya MCC leo imepitia upya hali ya sasa ya msaada wake inaotoa kwa nchi changa katika kupambana na umasikini na kusisitiza umuhimu wa kusimamia maendeleo na uwajibikaji

“….Leo bodi imekumbusha kuwa utoaji wa fedha zake si ‘automatic’ bali ni kwa kuzingatia vigezo….utawala bora na uwajibikaji ni nguzo kuu ya kuondoa umasikini; na nchi itakayozembea katika maeneo haya, si tu kwamba itaathiri upatikanaji wa msaada wa MCC, bali pia itaathirika katika mipango na sera zetu za muda mrefu katika kusaidia uchumi wa nchi zao.”

Ofisa wa MCC, Darius Mans, alikiambia kikao cha bodi kuwa vigezo vilivyowekwa na MCC vikikiukwa misaada inakatwa, bila kujali hatua iliyofikiwa.

Mans alitoa mfano wa nchi za Honduras na Madagascar, ambazo zimekatiwa misaada kwenye miradi yao kutokana na kukiuka vigezo vilivyowekwa, ikiwa ni pamoja na utawala mbovu.

Miradi inayolengwa na MCC kwa Tanzania ni ile ya kupunguza umasikini, na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza kipato cha wananchi kwa kulenga uwekezaji katika sekta za miundombinu, nishati na maji.

Mradi huo wenye awamu tatu unalenga kusaidia kutatua tatizo la usafiri kwa kuboresha barabara ili kuchochea biashara na kusaidia kuwaunganisha wananchi na masoko, shule, vituo vya afya na hospitali.

Aidha, mradi wa MCC unalenga kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuwafikishia umeme wananchi ambao hawajafikiwa na huduma hiyo; na kuboresha huduma ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: