Marmo, Masha wametuachia fundisho


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Laurence Masha

WANANCHI wa Mbulu, mkoani Manyara na Nyamagana mkoani Mwanza, wamechukua uamuzi sahihi. Wamekataa kuburuzwa na wale walijipachika “Umungu mtu” – Laurence Masha (Nyamagana) na Phillip Marmo (Mbulu).

Hawakuchukua uamuzi huo kwa njia ya mkato, hapana! Wametumia njia halali ya sanduku la kura.

Marmo alikuwa ni miongoni mwa wabunge mashuhuri na wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anafahamika hasa kutokana na ujuzi wake wa sheria za kimataifa na masuala ya Bunge.

Ndani ya serikali ameshika nafasi kadhaa. Miongoni mwao, ni naibu spika wa Bunge la Jamhuri na waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).

Aliwahi kuwa mjumbe katika Tume ya Jaji Francis Nyalali ambayo ilikuwa inatafuta maoni ya wananchi kuhusu kurejeshwa ama kutorejshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Ni tume hiyo iliyokuja na maelezo kuwa asilimia 80 ya wananchi wanataka tuendelee na mfumo wa chama kimoja.

Hata hivyo, kutokana na ushawishi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uzito wa matukio ya kihistoria ya mwishoni mwa miaka ya themanini, serikali ikalazimika kukubali kwa shingo upande mfumo wa vyama vingi nchini.

Hivyo, mtu aliyeongoza tume iliyokuta wananchi wanataka chama kimoja anapokuja kuangushwa na mtu kutoka mfumo wa vyama vingi, lenyewe hilo linatosha kuwa simulizi.

Jingine ambalo linatoa somo zito kwa Marmo, ni kwamba ni yeye aliyekuwa mpinzani mkubwa wa kurejesha wagombea binafsi katika mfumo wa kisiasa.

Ni Mbulu ambako historia ya taifa imeandikwa, kwamba aliwahi kusimamishwa mgombea binafsi na kumshinda mgombea wa chama cha Tanganyika African Union (TANU) aliyepigiwa kampeni na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Leo hii wananchi wa Mbulu wanapoamua kumkatalia Marmo kuwa mbunge wao, wanathibitisha kuwa wanayemtaka kuwa mwakilishi wao, ni yule ambaye hayuko tauari kukaa katika kwapa la serikali.

Kwa wengine inashangaza, lakini historia inaonesha kuwa wamewahi kufanya hivyo mara kadhaa. Inawezekana katika muda wa uongozi wake, Marmo alikuwa na mahusiano mabaya na wananchi wake.

Hivyo kwa kuwa hakuchukua jitihada za kuwa miongoni mwao, wameamua kumkumbusha.

Naye, Masha ana somo lake. Linahusu vijana wanaoingia bungeni sasa hivi na hasa wale wanaotokana CCM. Kwamba sauti kubwa katika uchaguzi huu uliokwisha ni kutaka vijana wengi waingie bungeni. Wamefanikiwa.

Lakini hii si sauti mpya na wala haijaanza leo. Mwaka 2005 wakati wa kuingia “rais kijana” Jakaya Kikwete, watu waliamini kabisa kuwa sura mpya za vijana zitaingia bungeni na katika serikali. Ndivyo ilivyokuwa.

Miongoni mwao ni mwanasiasa kijana na ambaye alibeba matumaini makubwa ya vijana wenzake, Laurence Kego Masha.

Masha alikuwa amebeba matumaini ya vijana wengi hasa waliopo nje ya nchi kutaka kurudi nchini kuja kutumikia taifa lao.

Alikuwa ni kioo cha kutazamia kama hawa wasomi waliorudi nyumbani wanaweza kuonesha namna ya uongozi ambao ni wa kisasa na unaoweza kulisaidia taifa kusonga mbele.

Na kwa vile amekulia na kusoma Marekani kulikuwa na imani kubwa zaidi kuwa ataonesha uongozi wa aina ya pekee na wenye tija kwa taifa.

Alianza kama naibu waziri na baadaye akateuliwa kuwa waziri kamili, na hivyo wengi walitegemea kumuona kijana huyo akibeba wajibu wake huo mkubwa kwa unyenyekevu, weledi na uthabiti wa kiuongozi.

Bahati mbaya sana baadhi ya maamuzi aliyochukua yalimuweka kwenye mwanga mbaya. Kwa wakazi wa Nyamagana wakajikuta hawana mahusiano na mbunge wao.

Lakini naamini tatizo kubwa ambalo alikutana nalo mapema zaidi ni kupewa kuongoza wizara nyeti na kubwa kama ya mambo ya ndani.

Ilikuwa ni makosa kwa rais wa Jamhuri kumkabidhi Masha wizara hii. Kibuli kikaanza. Majigambo yakashamiri. Kwa wanaomfahamu wanasema alianza kuota pembe na kutumia madaraka ya umma kujinufaisha binafsi.

Wizara hii nyeti, inahusisha maisha ya wananchi; maslahi ya askari magereza, polisi na uokoaji, haikustahili kukabidhiwa kwa mtu asiye na uzoefu wa uongozi kama Masha.

Kusema kuwa hakuwa na uzoefu, haina maana ya kudharau uwezo wake wa kitaalam au kitaaluma kama mwanasheria.

Mambo ya ndani ni wizara inayohitaji mtu mwenye uwezo mkubwa, asiye na majivuno na mwenye uzoefu na aliyetayari kutenda kazi kwa uwazi na uaminifu.

Masha hakuwa na sifa hizo. Hivyo basi, ilimbidi kwanza kujengea heshima ndani ya jeshi kabla ya kuanza kutimiza wajibu wake. Hadi anamalizia nafasi yake, suala la yeye kuheshimiwa na wale anaowaongoza linabakia kuwa na utata.

Kuna maelezo kwamba naibu wake, Balozi Khamis Kagasheki, amekuwa na mahusiano mazuri na askari na anaheshimiwa na wale anaowaongoza, kuliko waziri mwenyewe.

Ushahidi wa hili, ni kura alizozipata kwenye vituo vya kupigia kura kwenye makambi ya jeshi la Polisi na Magereza jimboni kwake, mkoani Mwanza zinasikitisha.

Hivyo, Masha naye amekuwa ni alama kwa viongozi vijana wengine na hasa wale wanaoingia katika uongozi kupitia CCM na ambao wanabeshwa mizigo wasioweza kuimudu.

Kijana ambaye anajikuta anetetemekewa, anapigiwa saluti na kuwakilisha watu waliomzidi umri mara mbili zaidi, ni majaribu makubwa kwake.

Ni muhimu kwa kijana wa namna hiyo hata kama ni msomi kiasi gani apewe muda kwanza wa kujiandaa kushika madaraka. Inasikitisha kuwa Masha hakupewa nafasi hiyo, badala yake rais Jakaya Kikwete alimuibua na kumkabidhi madaraka ya nchi.

Wala hakumpa nafasi ya kujifunza mazingira ya siasa nchini. Haijulikani ni vigezo gani ambavyo Kikwete alitumia kumpa Masha uwaziri na kumfanya Kagasheki kuwa naibu waziri. Wapo wanaohusisha na hatua hiyo na uswahiba kati ya Masha na mtoto wa Kikwete, Ridhiwani Jakaya Kikwete.

Ni vizuri kwa mfano wabunge wote vijana wanaoingia bungeni mwaka huu wasipewe nafaisi ya kuwa mawaziri wala manaibu. Waachwe wajifunze kuwatumikia wananchi kwanza, wajifunze kutengeneza mawasiliano kati yao na wananchi bila ya mapambo ya ukubwa.

Tukiwaacha hata kwa miaka mitatu ya ubunge ndipo hapo tunawafundisha kujishusha na kukaa na wananchi.

Na kama kweli wana uwezo wa kujifunza basi miaka mitano inatosha kujifunza na kuwapima. Wale watakaohimili miaka mitano ya kwanza na wakarudi kwa kipindi kingine basi hapo ndipo tunaweza kuanza kuwafikiria kuwapa madaraka.

Hata wabunge wazee ambao hawajawahi kushika madaraka, ni muhimu wakawekwa upandeni. Ni kwa sababu wengi wao, wanaingia madarakani kwa kutafuta fedha za kumalizia maisha yao.

Hivyo, katika kuanguka kwa viongozi hawa tunajifunza mambo mengi. Tumejifunza ubinafsi, umimi na kujikweza kwa baadhi yao, kuwa ndiyo chimbuko la wao kutokomea kisiasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: