MARTINA KABISAMA: Bila tume huru hakuna uchaguzi huru


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Asasi zasema yapasa itokane na katiba mpya

“BILA ya katiba mpya itakayotupa mwongozo wa kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, Tanzania tutachelewa kushuhudia uchaguzi huru na wa haki,” anasema Martina Kabisama.

Kabisama ni Mkurugenzi wa Mtandao wa taasisi zinazotetea haki za binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRiNGON). Lakini, katika nafasi yake ya mwenyekiti wa Umoja wa asasi 17 zisizo za kiserikali nchini (TACCEO), Kabisama anasema asasi hizo zimebaini haja ya kuwepo mfumo ulio wazi katika kupanga na kusimamia uchaguzi.

Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Kabisama anasema uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga, mkoani Tabora umethibitisha imani hiyo.

Kabisama anasema yaliyoshuhudiwa na taasisi hizo 17 wakati wa uchaguzi huo, kimtizamo, yamefuta uhalali wa uchaguzi uliokwisha kwa Dk. Dalaly Peter Kafumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutangazwa mshindi.

“Kulingana na upungufu uliojitokeza katika maeneo mengi kama tulivyoshuhudia, sehemu ya mashitaka yetu tutayapeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mengine serikalini. Lakini vilevile haya yote tunayashitaki kwa wananchi,” anasema.

Kwanini wapeleke masuala hayo kwa wananchi? Anasema wananchi ndio wahusika wakubwa maana ndio wenye dhamana ya kuendesha nchi yao. Ni wao wanaoamua uongozi wanaotaka; wao ndio wenye kuamua chama cha kuwaongoza.

“Sisi tunachokifanya ni kuwafungua tu macho wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na katiba mpya… ile yenye kubeba dhana ya kuwa na tume huru ya uchaguzi. Bila ya hivyo, vilio vyao vya kukosa haki havitakoma popote pale utakapofanyika uchaguzi ukiwemo wa 2015 iwapo hatutakuwa tumerekebisha kasoro hizi,” anasema.

Kabisama anaelezea mfululizo wa kasoro za msingi walizozibaini katika uchaguzi mdogo wa Igunga ikiwemo ile iliyohusu tofauti au mkanganyiko wa takwimu za wapiga kura walioorodheshwa katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi.

Anasema wanamtuhumu Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Igunga, Protace Magayane kwa kuonyesha udhaifu mkubwa kwenye suala la idadi kamili ya watu waliotakiwa kupiga kura.

Kwanza ni kama ametulaghai, anasema. “Awali alituambia kwamba takwimu zitakazotumika ni zile zilizotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Idadi ya wapigakura walioandikishwa mwaka jana ni 177, 077, lakini Oktoba 3 mwaka huu akatangaza idadi mpya ya wapigakura 171,019.”

Anasema takwimu hizo zinaonyesha tofauti ya watu 6,058 kutoka idadi aliyotangaza Magayane.

“Ni hapa ndipo tunalalamika kwamba kunahitajika marekebisho makubwa ya taarifa ya maboresho mapya ya daftari la kudumu la wapigakura,” anasema Kabisama ambaye wiki iliyopita alitoa taarifa ya awali ya uangalizi wa uchaguzi wa Igunga.

Anasema asasi 17 zilizojumuika kama waangalizi wa uchaguzi huo, zilibaini vitendo vya kuhongwa kwa wapigakura kwa kuwapa vitu kama vile pombe na ahadi ya kuwagawia nyama.

Ahadi kama hizo zilitumiwa na vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo kwa ajili ya kukusanya shahada za kupigia kura za wananchi. “Hili lilitekelezwa kwa kununua shahada moja kwa mpaka Sh. 15,000 suala ambalo ni uvunjaji wa sheria,” anasema.

“Baadhi ya wanasiasa na vyama vyao walitumia umasikini wa wananchi kununua shahada nyingi za kupigia kura na wakati mwingine walipewa kwa kubadilishana na fulana,” anasema.

Anasema watendaji wa vijiji walikutwa wakigawa mahindi kwa wapigakura kama mbinu ya kushawishi wamchague mgombea wa “chama chao.”

“Yapo tuliyoyashitaki kwa Tume (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) lakini mengine tuliwaarifu maofisa wa TAKUKURU. Inasikitisha hawakutoa ushirikiano wa kudhibiti vitendo hivi,” anasema.

Kabisama anasema zipo kasoro zilizobainika wakati wa upigaji kura. “Siku ya kupiga kura baadhi ya wapigakura walinunuliwa pombe na wagombea na kunywa pombe yao jirani na kituo cha kupigia kura. Wapo waliopewa nyama.

Uchunguzi wao anasema uligundua baadhi ya watu walifika kwenye vituo wakiwa wamekunywa pombe na kudanganya kwa watendaji wa tume kuwa hawajui kusoma wala kuandika na hivyo waruhusiwe kuingia na watu wa kuwasaidia kupiga kura zao.

“Cha ajabu walipokataliwa na wasimamizi wa vituo, walibadilika na kusema ‘naona nitaweza peke yangu kujua kupiga kura yangu ninapotaka.”

Kasoro nyingine ameitaja ya watu kadhaa kushindwa kupiga kura ingawa walifika vituoni na shahada zao; waliambiwa na wasimamizi kuwa majina yao yalishafutwa kwani majina hayo yamekutwa wenyewe wamefariki dunia siku nyingi.

Kituo cha Shule ya Msingi Nanga, watu 15 walirudishwa kwa madai hayo na katika kata za Mgondavile, Mbutu na Nyandekwa kila kituo watu wawili walikumbwa na mkasa huo.

Kabisama anasema waangalizi wao walishuhudia kampeni ikifanywa siku ya uchaguzi eneo la Ibutamashuzi, Kata ya Mbutu.

Rafu nyingine anasema zilifanywa na wasimamizi wa vituo ikiwemo kutangaza mgombea fulani amejitoa hivyo kuashiria kuwa kuna mgombea hana mpinzani.

Kabisama anasema hawakuona sababu ya msingi ya msimamizi wa uchaguzi kuchelewesha tangazo la matokeo wakati ingewezekana iwapo walitumia fursa ya maendeleo ya kimtandao.

Anasema kunahitajika usimamizi makini wa sheria ya uchaguzi na zile zinazolinda usalama wa wananchi ili kuepusha matukio yanayoweza kuchochea vurugu.

Alitoa mfano wa vurugu zilizotokea wakati wa kampeni ikiwemo kukutwa makundi ya vijana wafuasi wa vyama wakitembea na mapanga mikononi na kiongozi kuonesha silaha kiunoni.

SAHRiNGON ina uzoefu wa kutuma watu wake kwa ajili ya kuangalia uchaguzi katika nchi mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Ilishirikiana na taasisi 16 ambazo baadhi yake ni Tamwa, WLAC, Tanlap, Wildaf, Fordia, HakiMadini, MPI, Accorf, ZLSC, PF, Tahurifo, YPC, Leat na LHRC.

0
No votes yet