Masaburi akalia kuti kavu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Dk. Didas Masaburi

MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi ameliingiza Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA) katika mgogoro mkubwa wa kisheria kufuatia hatua yake ya kukaidi agizo la ofisi ya waziri mkuu, MwanaHALISI limebaini.

Katika hali inayozua maswali mengi Dk. Masaburi aliamua kuitisha mkutano wa wanahisa, akiwemo mwekezaji mpya – Simon Group Limited (SGL) aliyemuuzia kinyemela hisa 52.535 bila kufuata taratibu na katika mazingira yaliyojaa utata.

Dk. Masaburi aliitisha mkutano huo 10 Juni 2011 huku akijua fika kwamba serikali imemuagiza kusitisha “mara moja” mchakato wa kukabidhi shirika hilo kwa muwekezaji.

Ofisi ya Waziri Mkuu, ilimwagiza Meneja Mkuu wa UDA asikabidhi shirika hilo kwa anayejiita muwekezaji. Barua ya ofisi ya waziri mkuu kwenda kwa meneja wa UDA ilikuwa na Kumb. Na. CAB. 185/295/01/27. Iliandikwa  28 Februari, 2011 na ilisainiwa na E.G. Mgendera.

Mgendera katika barua hiyo alieleza “Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebaini uuzaji wa hisa za UDA ambazo hazijagawiwa unafanyika kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma (2004).”

Anasema, “Unashauriwa kuwasiliana na Consolidated Holding Corporation (CHC) ili kupata ushauri wa namna bora ambayo hisa hizo zinaweza kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika kisheria.”

Nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Mkurugenzi wa Jiji.

Aidha, Dk. Masaburi aliitisha mkutano wa kukabidhi UDA mikononi mwa muwekezaji bila kushirikisha serikali; alichukua uamuzi huo ili “kutimiza maelekezo ya SGL” waliokuwa wanatamani kwa udi na uvumba udhibiti wa mali za UDA.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya Kambi rasmi ya upinzani bungeni kuituhumu serikali kuuza shirika hilo kinyemelela.

Kambi ya upinzani ilisema aliyeekuwa mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya UDA, Iddi Simba amechotewa na kampuni ya Simon Group Ltd., iliyomilikishwa shirika hilo kiasi cha Sh. 200 milioni “kwa njia ya rushwa.”

Tayari sakata la uuzaji wa hisa za UDA umeibua mvutano mkubwa wa maneno kati ya Dk. Masaburi na baadhi ya wabunge wa jiji la Dar es Salaam wanaotaka uuzaji huo usitishwe.

Kwa mujibu wa nyaraka kadhaa ambazo gazeti hili imezipata, Dk. Masaburi amefanikisha “diri” hiyo bila kushirikisha Msajili wa Hazina, ambaye kisheria ndiye msimamizi wa hisa za serikali katika mashirika ya umma.

Mkutano huo wa 10 Juni 2011 uliokabidhi UDA mikononi mwa muwekezaji ulihudhuriwa na Dk. Masaburi, Isaac Tasinga, mwanasheria wa jiji, Philip Mwakyusa, kaimu mkurugenzi wa jiji na Robert Kisena, mkurugenzi mtendaji wa Simon Group Ltd.

Katika mkutano huo, Dk. Masaburi ndiye aliyemtambulisha rasmi anayeitwa muwekezaji kama ndiyo mwenye hisa mkubwa (Majority Shareholder); hatua ambayo ilikwenda sambamba na kuvunjwa kwa bodi ya UDA.

Siku hiyohiyo ya 10 Juni, Dk. Masaburi alisaini waraka ulioarifu kuvunjwa rasmi kwa bodi ya shirika hilo.

Waraka huo ulioandaliwa katika karatasi yenye nembo na anuani za UDA – Mtaa Bandarini, Eneo la Bandarini, S.L.P 872, Dar es Salaam, ulielekeza pia kuteuliwa kwa wakurugenzi wapya ambao hawatapungua wanne watakaoteuliwa na wenye hisa.

Mtendaji mpya wa UDA kwa mujibu wa waraka huo, ni Simon Masumbuko Bulenganija.

Hata hivyo, Masaburi alitenda hayo bila idhini ya Baraza la Madiwani la jiji la Dar es Salaam.

Kutokana na kugundua udhaifu huo, Dk. Masaburi aliitisha kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi, 29 Juni mwaka huu – siku 10 baada ya shirika kukabidhi muwekezaji – kutaka kuhalalisha uamuzi wake, hatua ambayo imepingwa na baadhi ya wabunge wakisema ni “kinyume cha taratibu.”

Nyaraka zinaonyesha mkataba wa mauziano ya hisa kati ya jiji na SGL ulifanyika 11 Februari 2011.

Katika kile kinachoweza kuitwa kuweka mazingira vizuri, tarehe 6 Juni 2011, Robert Kisena, aliandikia barua msajili wa hazina na mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam akiwataka kuitishwa mkutano wa wanahisa ili kuliokoa shirika hilo.

Kisena, aliyejitambulisha kama Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group Ltd., alisema kutokana na mazingira ya kutoheshimiwa makubaliano ya mkataba kati yake na jiji, wameanza kuwa na mashaka na hata “kukosa imani juu ya mambo mengine tunayopaswa kutekeleza kwa upande wetu.”

“Kwa hali hiyo, tunadhani njia pekee ya kuokoa shirika na kulinda haki zetu ni kwa wanahisa wenyewe kuingilia kati kwa kuitisha kikao maalum (extra ordinary meeting) ili kufanya maamuzi ya mustakabali wa shirika,” aliandika.

Alisema hatua hiyo ilikuwa inatilia mkazo uzingatiaji wa Ibara ya 4.4.1 ya mkataba wa mauziano ya hisa kati ya pande hizo mbili.

Kisena ndiye aliyeandika barua siki hiyohiyo kumjulisha Idi Simba kuvunjwa kwa Bodi yake ya Wakurugenzi.

MwanaHALISI limefahamishwa uuzaji wa UDA umegubikwa na utata. Kwa mfano, mchakato wa uuzaji wa UDA ulianza mwishoni mwa mwaka 2010, lakini ulipamba moto wakati Dk. Masaburi aliposhika kiti cha umeya Februali 2011.

Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa meya wa jiji la Dar es Salaam, aliyebeba Masaburi hadi katika klabu maarufu ya Saigon, Kariaokoo Dar es Salaam, ni Iddi Simba.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: