Masaburi hatarini kung’olewa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aweza kufukuzwa kwenye nafasi yake wakati wowote, imefahamika.

Kufukuzwa kwa Masaburi kwenye nafasi ya umeya kunatokana na kushiriki katika vitendo vilivyoitwa “ovu na vya kuhujumu Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).”

Nyaraka kadhaa ambazo MwanaHALISI limezipata zinaonyesha ushiriki wa Masaburi katika kuidhinisha matumizi ya dola za Marekani. 133, 125 mali ya shirika hilo.

Vyanzo vya taarifa vinasema tayari baadhi ya madiwani wakiongozwa na wabunge wa Dar es Salaam, wameanza kujipanga kutaka kumfukuza Meya Masaburi kwenye nafasi yake.

“Inawezekana mchakato huu ukawa mrefu…unahitaji ushiriki wa watu wengi. Lakini nakuhakikishia kutokana na ushahidi uliopo, lazima tutamng’oa,” ameeleza mbunge mmoja wa Dar es Salaam kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Amesema yeye na wenzake hawako tayari kuona rasilimali za Dar es Salaam na taifa zinaporwa na watu wachache kwa kisingizio cha kutafuta uwekezaji.

“Huu ni ufisadi kwa asilimia 100. Nakuambia lazima tuukomeshe kwa kuwaondoa wote wanaohusika na jambo hili,” ameeleza.

Taarifa nyingine zinasema madiwani na wabunge wa Dar es Salaam walikuwa wakutane jana katika “Baraza Maalum la Madiwani” ili kujadili na kutolea maamuzi suala hili.

Masaburi anadaiwa kuendesha kikao cha wanahisa wa UDA na kuteua watia saini wa akaunti ya shirika hilo kinyume na maelekezo ya madiwani ya kusubiri hadi iundwe bodi ya shirika hilo; na kutekeleza mpango wa ununuzi wa mabasi, bila kumshirikisha Msajili wa Hazina.

Inaelezwa kuwa kitendo cha Masaburi kufungua moja ya akaunti za UDA, kuweka waendesha akaunti wapya, kuweka fedha kwenye akaunti hiyo na kuomba benki kuruhusu uhamishaji fedha kwenda akaunti ya kampuni ya magari ya TATA, umechukuliwa na madiwani kuwa uasi kwa yale yaliyokubaliwa.

Baraza la madiwani kwenye kikao chake cha kilichofanyika wiki ya kwanza ya Februari mwaka huu, kiliidhinsha uundaji wa bodi mpya ya UDA.

Kupitia uamuzi wa Masaburi, UDA ambayo iko kwenye mgogoro mkubwa unaotokana na ukiukwaji wa taratibu za ubinafsishaji, imenunua mabasi 30 kutoka kampuni ya TATA ya India.

“Robert Kisena na kampuni yake ya Simon Group Ltd., hawatambuliwi kuwa wenye hisa nyingi katika UDA. Hata kikao hicho hakikuhudhuriwa na mwakilishi wa Hazina,” ameeleza mtoa taarifa huyo.

Mkutano ambao Masaburi aliongoza na kupitisha maamuzi, ulihudhuriwa na Isaac Tasinga (mwanasheria wa Jiji), Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Philip Mwakyusa na Kisena ambaye alikuwa katibu.

Kikao hicho kiliwashirikisha Dk. Masaburi kutoka Halmashauri ya Jiji akiwa mwenyekiti.

Waliowakilisha Simon Group ni Robert Kisena na Venance Matondo. Waalikwa wawili kutoka UDA walikuwa Simon Bulenganija na Said Fikirini.

Walioteuliwa kuwa watia saini kisha kutambulishwa benki ya CBA (Commercial Bank of Africa), ni Robert Kisena, Simon Bulenganija na Said Fikirini.

Nyaraka mbalimbali zilizolifikia MwanaHALISI zinaonyesha kuwa UDA iliomba CBA ihamishe dola za Marekani 133,125  kutoka akaunti yake Na. 102203003 kwenda akaunti ya TATA African Holding (T) Ltd., ambayo ni Na. 8706005450900 katika Benki ya Standard Chartered (Tanzania) Ltd.

Fedha hizo ni sawa na asilimia 25 ya malipo kwa mabasi ambayo UDA imeamua kununua kutoka TATA kwa dola 532,500.

Mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba abiria 40 kila moja, yalitakiwa kuwasili kabla ya 15 Februari 2012.

Siku ambayo UDA waliomba kuhamisha fedha hizo kwa barua Kumb. Na. CBA/REG/01/UDA ya 26 Januari 2012, ndipo waliingiza katika akaunti hiyo Sh. 213,665, 625 (karibu sawa na dola za Marekani 133,125) kwa kutumia hundi Na. 333023.

Naye mwenyekiti mtendaji wa Simon Group Ltd., Robert Kisena amewarukia wabunge wa Dar es Salaam akiwataka kuacha upinzani kwa juhudi zake za kuwekeza katika UDA.

Akiongea na gazeti la Nipashe, Jumatatu, Kisema amesema kabla wabunge hawajapinga juhudi zake, wajiulize nani analipa wafanyakazi wa UDA.

Amesema kampuni yake inatumia Sh. 70 milioni kila mwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi wa UDA.

Msemaji wa Hazina hakupatikana kueleza iwapo fedha ambazo Simon Group anaingiza UDA zinaweza kupotea pale mfumo mpya wa umiliki wa shirika hilo utakapojulikana.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: