Masaburi kwenye tope jipya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

HATUA ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk.  Didas Masaburi kuunga mkono ununuzi wa mabasi mapya kwa kampuni ya usafiri Dar es Salaam (UDA), imechukuliwa kuwa “uasi” kwa serikali.

Dk. Masaburi anaunga mkono uamuzi wa kampuni ya Simon Group iliyotangaza mwishoni mwa wiki kuwa imenunua mabasi 30 kutoka kampuni ya TATA ya India ili kutoa UDA katika “janga la kuangamia.”

Taarifa zinasema hatua ya Simon Group kununua mabasi haikushirikisha Msajili wa Hazina ambaye anashikilia hisa za serikali katika UDA.

Ununuzi wa mabasi unafuatia kikao maalum kilichoendeshwa na Dk. Masaburi, kuamua kufungua moja ya akaunti za UDA, kuweka waendesha akaunti wapya, kuweka fedha kwenye akaunti hiyo na kuomba benki kuruhusu uhamishaji fedha kwenda akaunti ya kampuni ya magari ya TATA.

Sasa taarifa zinasema Dk. Masaburi ameongoza kikao cha wanahisa bila kuwapo Msajili wa Hazina anayewakilisha serikali na kuandaa orodha mpya ya watia saini kwenye hundi za UDA.

Simon Group imekuwa katikati ya mgogoro na wizara ya Fedha na Uchumi kwa kile kilichoitwa kuuziwa hisa bila kufuata utaratibu na kampuni “kufanywa mwanahisa kiongozi” katika UDA.

Hatua ya Dk. Masaburi na Simon Group imechukuliwa kuwa ni uasi kwa vile imevunja pia maamuzi ya tarehe 10 Juni 2011 ya Mkutano Maalumu wa wanahisa wa UDA.

Kwenye mkutano huo, wanahisa walikubaliana kuvunja bodi ya wakurugenzi wa UDA iliyokuwa inaongozwa na Idd Simba, kumsimamisha kazi meneja wa shirika, Victor Milanzi na kuwasimamisha watia saini wa nyaraka na hundi za kampuni.

Chini ya makubaliano hayo, hundi na nyaraka zilitakiwa kusainiwa na wanahisa wawili kati ya watatu waliokuwapo; na endapo ungetokea ucheleweshaji wa uteuzi wa watia saini, mwanahisa Simon Group alitakiwa kuendelea kulipa mahitaji ambayo yangejitokeza kwa kushauriana na wanahisa wenzake.

Waliohudhuria kikao hicho kwa upande wa jiji la Dar es Salaam walikuwa Dk. Didas Masaburi (Mwenyekiti), Isaac Tasinga (mwanasheria wa Jiji) na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Philip Mwakyusa.

Kwa upande wa Simon Group, alikuwapo Robert Kisena kama katibu. Hakukuwa na mwakilishi wa Hazina.

Kutokana na hali hiyo, uendeshaji wa shughuli za UDA umekuwa ukitegemea fedha kutoka kwa kampuni ya Simon Group, hali ambayo “imefanya shughuli za kampuni hiyo kuwa ngumu.”

Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena amesema kuwa wamekuwa wakilipa mishahara, mafuta ya magari, mafao ya watumishi waliostaafu na madeni mbalimbali kwa fedha za Simon Group.

Shirika la UDA lilianzishwa na serikali mwaka 1974 na mwaka 1983 msajili wa hazina alitoa asilimia 51 ya hisa kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ili kuisaidia kuwa na vitega uchumi na kuboresha usafiri wa jiji. Msajili wa hazina alibakia na asilimia 49.

Mwaka 2007 kulifanyika kikao cha wanahisa kilichoagiza Bodi ya UDA, kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu, kutafuta mwekezaji. Wizara iliipata Kampuni ya Simon Group Limited ambayo ilijitokeza kununua hisa za serikali lakini ikatakiwa ridhaa ya serikali.

Kabla ya ridhaa hiyo kutolewa, Bodi ya UDA ikauza hisa za serikali ambazo zilikuwa hazijagawiwa kwa Simon Group, badala ya kusubiri msajili wa hazina kuuza hisa zake, wala kuomba ushauri kutoka kwake au kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uongozi wa UDA ulipotaka kununua magari mapya, uliitisha kikao cha wanahisa ili kupata idhini ya kutumia fedha zilizokuwa katika akaunti ya shirika hilo. Msajili wa hazina hakuhudhuria kikao hicho.

“Tuliwasiliana na Msajili wa Hazina lakini alitueleza kuwa alikuwa bado anashughulikia masuala yetu ya kutaka kurekebisha shirika; ndipo sisi (menejimenti ya UDA) tukaamua kuitisha kikao cha wanahisa kuweka mikakati namna ya kununua mabasi hayo,” ameeleza Kisena.

Amesema, “Tulimfuata Dk. Masaburi, tukamweleza mpango wetu na kwamba fedha tunazotaka kuchukua kwenye akaunti ya UDA ni zetu Alituelewa. Tuliketi na tukateua watia saini wengine kutoka miongoni mwetu,”

Kikao hicho kiliwashirikisha Dk. Masaburi kutoka Halmashauri ya Jiji akiwa mwenyekiti; waliowakilisha Simon Group ni Robert Kisena na Venance Matondo. Waalikwa wawili kutoka UDA walikuwa Simon Bulenganija na Said Fikirini.

Walioteuliwa kuwa watia saini kisha kutambulishwa benki ya CBA (Commercial Bank of Africa), ni Robert Kisena, Simon Bulenganija na Said Fikirini.

Nyaraka mbalimbali zilizolifikia MwanaHALISI zinaonyesha kuwa UDA iliomba CBA ihamishe dola za Marekani 133,125  kutoka akaunti yake Na. 102203003 kwenda akaunti ya TATA African Holding (T) Ltd., ambayo ni Na. 8706005450900 katika Benki ya Standard Chartered (Tanzania) Ltd.

Fedha hizo ni sawa na asilimia 25 ya malipo kwa  mabasi ambayo UDA imeamua kununua kutoka TATA kwa dola za Marekani 532,500. Mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba abiria 40 kila moja, yalitakiwa kuwasili kabla ya 15 Februari 2012.

Siku ambayo UDA waliomba kuhamisha fedha hizo kwa barua Kumb. Na. CBA/REG/01/UDA ya 26 Januari 2012, ndipo waliingiza katika akaunti hiyo Sh 213,665, 625 (karibu sawa na dola za Marekani 133,125) kwa kutumia hundi Na. 333023.

Uchunguzi wa MwanaHALISI umebaini kuwa licha ya UDA kutimiza masharti ya benki hiyo, uongozi wa CBA uliingiwa na wasiwasi na kuamua kuandika barua kwa wizara ya fedha kuuliza iwapo malipo hayo yafanyike, hasa kutokana na mgogoro ulioliandama shirika hilo.

Katika barua hiyo, Kumb. Na. Legal/FinanceMinistry/02/12/01 ya 16 Februari 2012 kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, CBA inauliza iwapo serikali inajua mabadiliko ya umilikaji wa hisa za UDA ambao umebadili muundo wake kwa kuingiza Simon Group kama mwanahisa.

CBA ilitaka kujua pia iwapo maombi ya kuhamisha fedha hizo yalikuwa sahihi kisheria na yanatambuliwa na serikali; na iwapo makubaliano ya wanahisa hao yalikuwa na uhalali kisheria na yanawabana wahusika wote, ikiwamo serikali.

Uongozi wa benki hiyo, tawi la PPF House iliko akaunti hiyo, ulitoa siku tano za kazi kusubiri majibu ya serikali, na endapo isingejibu, benki ingefanya malipo hayo.

Dk. Masaburi alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusiana na suala hili, alisema ameamua kufungua akaunti hiyo kwa maslahi ya UDA; ili iweze kufanya kazi kwa kuwa shirika lilikuwa linashindwa kujiendesha.

“Niliona ni busara wafungue akaunti moja yenye hela zao, ili iweze kutumika. Hata kwenye hiyo akaunti hakukuwa na hata senti tano za UDA. Hela zile waliweka wenyewe Simon Group na walitaka kuzitumia,” alisema.

Amesema katika uamuzi huo hawakumshirikisha msajili wa hazina, kwa kuwa hata kwenye kikao cha kufunga akaunti hizo za UDA hakushiriki.

“Tulikaa na huyu Bwana (Kisena) tukakubaliana kama tulivyokubaliana awali,” alisema Masaburi.

Msajili wa hazina Godfrey Msela hakupatikana kutoa maelezo. Kaimu msajili wa hazina aliyetambuliwa kwa jina la Mlaki na ambaye alikuwa na sauti ya kike, alisema yeye ni mgeni ndani ya ofisi hiyo na kwamba hakuwa na watu wa kuuliza nje ya muda wa kazi alipopigiwa simu.

Meneja wa CBA tawi la PPF House ilipo akaunti hiyo aliyejitambulisha kuwa ni Mbilinyi, alisema yeye si msemaji, bali wahusika ni makao makuu ya benki hiyo, ambao hata hivyo hawakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: