Masha sasa achunguzwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha anatuhumiwa. Anadaiwa kuingilia isivyopasa mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa.

Ni ukweli pia waziri mwenyewe amejieleza kwa angalau kusema hana wasiwasi wowote maana anachokifanya ni “kutekeleza majukumu yake ya uwaziri.” Suala hili linahusu mradi ambao uko chini ya wizara anayoiongoza.

Sasa zipo tuhuma, na nzito, dhidi ya waziri katika serikali na zimeshaelezwa bayana. Baada ya kufichuliwa na gazeti mojawapo nchini, mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa alizichukua na kuzipeleka bungeni kwa njia ya hoja binafsi.

Mkutano wa 14 wa Bunge umekwisha bila ya hoja hiyo kuwasilishwa. Spika amesema ameiahirisha hoja hiyo kwa sababu ameshauriwa na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama  ya Bunge, kwamba ni vema mchakato wa kutafuta mzabuni wa vitambulisho ukaachwa kuendelea na kukamilika.

Kwamba kuruhusu hoja binafsi bungeni kwa wakati huu kuhusu suala hilo, kunaweza kukwamisha mchakato na italeta hasara kubwa na fedheha kwa taifa.

Sisi tunaona kinyume chake. Lakini hata kama ipo sababu nzuri, tunajiuliza hivi mchakato ukikamilika ndio iwe nini wakati tayari umechafuliwa kwa hatua ya waziri?

Uingiliaji mchakato unamaanisha kuwepo dalili za rushwa na ndio tuhuma hasa zinazomkabili Waziri Masha. Sasa inakuwaje mtuhumiwa rushwa asihojiwe eti kwa sababu hiyo itaathiri mchakato?

Mchakato uendelee. Ila kila tukiangalia suala hili kwa makini, tunajikuta wazito wa kukubali waziri abaki kitini kwake huku mchakato unaotajwa kuingiliwa naye, nao ukiendelea.

Wakati mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutengeneza vitambulisho unaendelea, tunaona ni jambo muhimu kuanza uchunguzi dhidi ya Waziri Masha. Ufanywe na haraka.

Hata kama Bodi ya Zabuni tayari imetupa nje mzabuni aliyekuwa akitetewa na Masha, kwa misingi ya kutokuwa na sifa, bado kuna kila sababu ya kuchukulia hatua yule aliyelenga kukwamisha mradi kwa maslahi binafsi.

Kwa kuwa waziri anatuhumiwa kwa hisia za rushwa katika suala linalohusu mradi ulio chini ya wizara yake, ni muhimu asite kuongoza wizara ili kuachia uchunguzi huru.

Serikali ifike mahali ichoke kuendekeza na kuendeleza utamaduni kulinda viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Watanzania hawataki tena utamaduni huu na hakuna sababu ya kuwashurutisha, labda kama serikali yao haiwaheshimu wananchi walioiweka madarakani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: