Masikini Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version
Mjumbe wa Baraza la Wadhamini amkana
Dk. Nagu naye adaiwa kutoshiriki mkataba
Aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa

MGOGORO kuhusu mkataba wenye utata wa Umoja wa Vijana wa CCM umeingia katika sura mpya baada ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini kuukana, MwanaHALISI limeelezwa.

Hatua hii inamweka pabaya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM aliyeweka saini mkataba huo.

Taarifa za ndani zinasema ni Lowassa na Amos Makala, aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa UV-CCM ambao wanajua kilichofanyika, lakini wajumbe wengine hawakuitwa kwenye kikao chochote kupitisha mkataba huo.

Gazeti hili liliripoti mwezi mmoja uliopita, kwa mara ya kwanza, kuwa Baraza la Wadhamini la UV-CCM chini ya Lowassa lilisaini mkataba wenye thamani ya zaidi ya Sh. 30 bilioni, kati yake na makampuni mawili ya uwekezaji, bila wenye chama kujulishwa na kuridhia.

Mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Yusuph Mohammed Yusuf ameliambia gazeti hili kwamba hakushiriki kupitisha mkataba huo uliosheheni utata.

Yusufu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), alisema, “Baraza la Wadhamini halijawahi kukutana kupitisha mkataba huo.”

Alisema yeye hafahamu na wala hakumbuki kama Baraza la Wadhamini chini ya Lowassa iliwahi kukutana na kukubaliana juu ya kusainiwa kwa mkataba huo.

“Mimi ni mjumbe wa Baraza. Kama mkataba ni ule mlioandika kuwa ulisainiwa 2 Januari 2007, hakika siufahamu; sikuwahi kukutana na wenzangu na kukubaliana kusaini mkataba huo,” amesema Yusufu.

Akihojiwa kwa njia ya simu, Yusufu aliliambia gazeti hili, “Mimi ni mtu makini. Nimeona kitu hicho majuzi tu (Juni mwaka huu). Sijashiriki kuamua juu ya mkataba wa uwekezaji.”

Yusufu amesema walipelekewa mkataba na kuelezwa kuwa ni “maelewano” na kusema kuwa waliyapitia na “tukaagiza, kwa vile yalivyo sharti yapelekwe katika CC ya chama chetu.”

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Baraza hilo zinasema Lowassa alijichukulia maamuzi hayo mazito, huku akiwa tayari amejulishwa athari ya uamuzi wake.

Wiki iliyopita MwanaHALISI liliripoti Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akisema mkataba wa mradi wa ujenzi wa kitegauchumi cha UV-CCM una dosari nyingi, haukubaliki kama ulivyo na akaagiza utekelezaji wake usitishwe.

Rais alisema katika mawasiliano na Katibu Mkuu wa CCM Yusuf makamba kuwa mkataba umebainika kuwa na mapungufu mengi ya kisheria ambayo lazima yarekebishwe “ili tusipoteze maslahi katika mradi huu.”

Mjumbe mwingine wa Baraza la Wadhamini, Dk. Mary Nagu ameripotiwa kutoshiriki kuandaa au kupitisha mkataba huo.

Nagu ambaye ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko hakupatikana kujibu maswali yetu kwa kuwa yuko ziarani Afrika Kusini, Uturuki na Hispania.

Hata hivyo taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa watu walio karibu naye zinasema, “Mama Nagu tayari amejulisha kutohusika”  katika mkataba huo. Hakusema amemjulisha nani na lini.

UV-CCM imeingia mkataba na makampuni mawili ya M.M. Integrated Steel Mills (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL), ya kujenga kitega uchumi kwenye kiwanja Na. 108/2 bila kushirikisha Baraza Kuu la umoja huo.

Mkataba kati ya pande mbili hauna ukomo wa muda, hauelezi UV-CCM watapata nini hasa na umemilikisha ardhi kinyume cha sheria ya nchi.

Wiki iliyopita mjumbe wa  Bodi ya Wadhamini aliyeng’olewa kinyemela, Wilson Masilingi, alisema hajawahi kuona mkataba wa kinyonyaji kama wa UV-CCM na kuuita “mkataba wa ovyo.”

Katika hatua nyingine, taarifa zinasema awali mkataba huo ulifikishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika, kwa lengo la kupata baraka zake.

“Ndiyo mkataba ulifikishwa kwangu kabla ya kusainiwa. Nilimwambia Nchimbi kwamba, mimi siwajibiki kwao, lakini kwa kuwa wamekuja kuomba ushauri, basi nikawaambia mkataba hauna maslahi kwa umoja wao,” alisema mtoa taarifa akimnukuu Mwanyika.

Katika sakata hili, kwa mara nyingine, nyundo imeelekezwa kwa Lowassa, Makamba, Mwenyekiti wa UV-CCM Emmanuel Nchimbi na Mweka Hazina wa sasa wa CCM Amos Makala ambaye kwa maelezo ya nyongeza imefahamika kuwa “alikuwa shahidi tu wa Lowassa.”

Aidha, Beno Malisa, Kaimu Katibu Mkuu wa UV-CCM, huenda naye asisalimike uzito wa nyundo ya kisiasa na kisheria.

Wakati Lowassa anasaini mkataba, Malisa alikuwa Mwanasheria wa UV-CCM; mtaalam mwenye jukumu la kupitia mkataba na kutoa ushauri kabla ya kusainiwa. Hakufanya hivyo.

William Lukuvi, mjumbe mwingine wa baraza hakupatikana kutoa maelezo yake juu ya kushiriki au kutojua lolote kuhusu mkataba huu. Juhudi za kumtafuta zinaendelea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: