Masikini Mtikila


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version
MCHUNGAJI Christopher Mtikila

MCHUNGAJI Christopher Mtikila, ambaye yuko hapa kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa mbunge wa jimbo la Tarime, amefanya kazi kubwa kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuliko chama chake.

Mtikila ni mwenyekiti wa Democratic Party (DP) ambaye hadi sasa amejizolea sifa ya “Mwanasiasa mtibuaji,” kwa kurukia vyama vya upinzani kuliko chama tawala.

“Hapa tunaona ana kazi moja,” anaeleza mwanachama wa Chadema; “Kuchafua mgombea wetu na kuimarisha kauli za jeuri na kashfa za CCM dhidi ya chama chetu.”

Vyama vyenye ushindani mkuu katika uchaguzi wa Tarime ni Chadema na CCM. Wakati mgombea wa Chadema ni Charles  Mwera  Nyanguru, mgombea wa CCM ni Christopher Ryoba Kangoye.

Vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi ni NCCR-Mageuzi na DP cha Mtikila ambacho ufuasi wake jimboni ni mdogo.

Tangu aingie uwanjani wiki iliyopita, Mtikila amevalia njuga Chadema, akitaja kiongozi mmoja baada ya mwingine kuwa walihusika na mauaji ya Wangwe, kazi ambayo mvunaji mkuu wa matunda yake ni mshindani mkuu wa Chadema – CCM.

Mtikila, katika andishi alilosambaza wilayani Tarime, na katika hotuba zake, anadai kuwa yeye na wenzake wamefanya uchunguzi wa kesi ya mauaji ya Wangwe kwa “nguvu za maombi maalum kwa Mwenyezi Mungu.”

Ni kauli hizo na marudio yake ya mara kwa mara ambazo zimefanya baadhi ya wasikilizaji wake kuguna, kumpuuza na wakati mwingine kusababisha waondoke kwenye mikutano yake.

Wiki iliyopita, katika uwanja wa shule ya msingi iliyoko Sabasaba mjini Tarime, Mtikila alishukiwa na mzigo wa mawe kutoka kwa baadhi ya wasikilizaji wake; kumjeruhi kichwani na kusababisha ashonwe nyuzi tatu.

Mashambulizi ya Mtikila na DP yamefanya wananchi wafikirie labda ana uhusiano wowote na CCM. Lakini ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hotelini kwa Mtikila kunjulia hali, imetafsiriwa kwa hisia tofauti ingawa ingeonekana ya kawaida katika mazingira tofauti.

Andishi la Mtikila analosambaza hapa si jipya. Alilitoa Dar es Salam kwa wandishi wa habari wiki mbili zilizopita na kutaja watu wengi kuhusika na kifo cha Wangwe.

Hata hivyo, hakuna tarifa zozote juu ya Mtikila kuhojiwa na polisi kuhusu madai yake ambayo hakika yangeweza kuisaida polisi katika kuendesha kesi.

“Kwamba polisi wamedharau, kwa wiki tatu sasa, kauli za Mtikila, ujue na wao wameona anapiga miayo tu,” amesema Maulid Kabarega aliyejitambulisha kam mkazi wa mjini tarime.

Lakini kinachowashangaza wengi ni Mtikila kutosema chochote juu ya chama chake. Vyama vinajinadi kufanya hili na lile lakini yeye anazungunmzia kifo cha mbunge wa zamani na kumalizia kwa kusema anataka wananchi wachague mgombea wake ili aendeleze ya Wangwe.

Makali ya kauli za Mtikila yaliyomo katika andishi lake analonadi Tarime, yanafanana na kauli zilizomo katika andishi lingine liloko mahakama kuu katika moja ya kesi zake.

Katika andishi hilo kuna kauli ambazo haziwezi kuandikwa kwenye vyombo vya habari na madai mengi ambayo hayawezi kuthibitishwa dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.

Katika masikio ya wengi wilayani Tarime, kauli za Mtikila zinafanya wazazi wengi kujiuliza anayezitoa ana ulinzi gani na kwa nini hawajaona CM inamkemea au kumshambulia kama inavyofanya kwa vyama vingine.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: