Masikini serikali!


editor's picture

Na editor - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI imefunga milango na madirisha. Haitaki tena majadiliano na madaktari juu ya mazingira ya kazi na ujira.

Hii inakuja baada ya mgomo wa madaktari na utekaji na utesaji kinyama wa Dk. Steven Ulimboka, mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania.

Ni kama Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa asiyekubaliana naye amejifukuza kazi. Tishio kali!

Lakini ndani ya gazeti hili, daktari mmoja amenukuliwa akisema, “…wakati mwingine ninamwangalia mgonjwa, nina uwezo wa kumwokoa, lakini hakuna vifaa. Anakufa mbele yangu.”

Huo ni upande mwingine ambao serikali haijaangalia. Yenyewe imekazania kusema “…madaktari wanataka posho! Posho! Posho!”

Daktari anayenukuliwa anaona bila vifaa, hospitali yake ni kituo cha mwisho; mahali pa kusubiria kifo. Serikali haitaki kusikia hilo. Sasa serikali imeona, kwa vitendo kuwa ingekuwa na vifaa, Dk. Ulimboka asingepelekwa Nairobi na, au Afrika Kusini.

Serikali inaona kila siku, kwamba kama kungekuwa na vifaa, viongozi wake wasingekuwa wanapiga foleni kwenda kutibiwa nje. Kinachokosekana si maarifa, bali zana na mazingira bora ya kazi. Serikali haitaki kusikia.

Sasa serikali inasema italeta madaktari kutoka nje ya nchi. Kwamba tayari imetenga Sh. 200 bilioni kuwagharamia.

Serikali imefanya lini makubaliano na madaktari hao? Hizo fedha serikali imezitoa wapi kulipa watu wa nje? Maandiko matakatifu yaliishaonya: Usichukue chakula cha watoto na kumpa mbwa!

Je, madaktari wa nje watakuja na vifaa? Kama hawatakuwa na vifaa si watakuwa wanafanya utalii tu wa kujifunza lugha au kufanya tafiti za kuendeleza utaalam wao?

Tunatangaziwa haraka kuwa baadhi ya madaktari wamekubali kurejea kazini. Hivi serikali inaamini wanakwenda kufanya kazi kwa moyo uleule?

Serikali yoyote ikifunga milango ya mawasiliano, hata kwa njia ya migomo; inakuwa imeziba mifereji ya fikra na matumaini ya muwafaka. Yanakuwa maisha ya kuvimbiana.

Tunaitaka serikali kufanya mambo yafuatayo: Kwanza, iunde tume huru ya kuchunguza waliomtendea unyama Dk. Ulimboka. Pili, iwasikilize madaktari. Tatu, ituhakikishie kuwa italinda uhai wetu na mali zetu.

0
No votes yet