Maskini Kanali Muammar Ghadaffi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Kanali Muammar Ghadaffi

TAYARI waandamanaji wamedhibiti kikamilifu mji wa Benghazi, mji wa.pili kwa ukubwa nchini Libya. Harakati zimeshamiri kwenye mji mkuu wa Tripoli licha ya vitendo vya mauaji vinavyoendeshwa na vikosi vya ulinzi na usalama vinavyoendelea kumtii Kanali Muammar Ghadaffi, kiongozi wa Libya kwa miaka 42 sasa.

Wakati maandamano yakizidi nguvu huku utawala wa mitaa ya mji wa Benghazi ukiwekwa ili kuratibu usalama wa raia, zipo taarifa kwamba Kanali Ghadaffi alikuwa anafikiria kukimbilia Venezuela ambako amekuwa rafiki mkubwa wa kiongozi wake, Hugo Chavez. Lakini nchini kwake, ndege za kivita zinaua raia kwa mabomu kwa kutumia askari wa kukodiwa kutoka Ufaransa.

Taarifa hizo zinatolewa wakati mawaziri wake wasiopungua watatu wameshajiuzulu na kuunga mkono wito wa kutaka Kanali Ghadaffi ang’atuke na kuruhusu mageuzi ya uendeshaji wa nchi.

Kadhalika, Naibu Mwakilishi wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa, Ibrahim Dabbashi, ametoa wito kwa Ghadaffi kujiuzulu “haraka iwezekanavyo.” Lazima aache kuua raia, alisema Balozi Dabbashi mjini New York. "Anapaswa kusalimu amri na kuondoka Libya haraka," alisema huku akimshutumu Ghadaffi kwa kuua kwa halaliki. Aliomba Umoja wa Mataifa kuwalinda wananchi Libya na kuzuia serikali kupata silaha wakati huu.

Waziri wa Sheria wa Libya, Mustafa Abdul Jalil, alijiuzulu Jumatatu mchana huku akipinga mauaji ya wananchi na matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji. Gazeti la Quryna ambalo wiki iliyopita maandamano yalipoanza lilibeba kauli za kujipendekeza kwa serikali, juzi liligeuka na kuwapa moyo waandamanaji na kuripoti madhila yanayowakuta.

Kufikia usiku juzi, waandamanaji walianza kutinga uwanja wa wazi mjini Tripoli uitwao Kijani. Makabiliano ya uso kwa uso na askari wanaomtii Kanali Ghadaffi yalishuhudiwa. Hata hivyo, baadhi ya askari waliamua kuvua sare, kusalimisha silaha na kuungana na raia kupinga utawala.

Waandamanaji ambao wanasema wazi kuwa wanapigania uhuru, heshima, haki na usawa, hawajali mauaji yanayotokea ya baadhi ya wenzao. Walianza na wameapa wanataka kuhakikisha wanamaliza kazi. Kazi yenyewe ni ya kumtoa madarakani Kanali Ghadaffi.

Tangu juzi walikuwa wanasherehekea mafanikio ya kudhibiti mji wa Benghazi ingawa ni baada ya damu nyingi kumwagika. Hawakutishwa na kauli za vitisho za mtoto wa Kanali Ghadaffi, Saif el-Salam aliyetangaza kupitia televisheni ya taifa juzi kwamba utawala wa baba yake ungali imara na hatashindwa kwani “atapambana hadi risasi ya mwisho.”

Saif alisema Ghadaffi “hatasalimu amri hadi mtu wa mwisho mwanamme, hadi mwanamke wa mwisho na hadi kijana wa mwisho.”

Wakati huo, waandamanaji walikuwa wameutwaa kikamilifu mji wa Benghazi huku wakikiteka kituo kikuu cha usalama cha Katiba ndani ya mji huo.

Awali, waandamanaji walilenga kufikia makazi rasmi ya Kanali Ghadaffi mjini Tripoli baada ya kukusanyika eneo la Kijani. Harakati hizo zilitarajiwa kuongeza nguvu ya hatua za vikosi vya usalama vya serikali kupambana na waandamanaji.

Vyanzo vya habari viliripoti kuwa askari wa kikosi cha mbwa walikuwa wanafyatulia risasi waandamanaji huku wafuasi wa Kanali Ghadhaffi wakitumia malori na magari madogo kupiga risasi waandamanaji na kuwakanyaga wananchi.

Mchana Jumatatu, moto mkubwa uliwaka eneo la ukumbi mkubwa ambao hutumika kwa mikutano mikubwa inayofanana na vikao vya bunge.

Shughuli zote za kijamii zikiwemo shule, ofisi za serikali na maduka makubwa zilisimama wakati huo. Baadhi ya askari wanaomtii Kanali Ghadaffi wakiunda jumuiya mbalimbali zinazomuunga mkono walitanda mitaani kusaka waandamanaji na kuwapiga, kulingana na mmoja wa waandamanaji.

Ghasia kati ya waandamanaji na vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali, zilikuwa kubwa katika jiji la Tripoli lenye wakazi wapatao milioni mbili, ikiashiria kwamba harakati zimeshamiri katika siku ya sita tangu maandamano yalipoanza kwenye miji ya mashariki mwa nchi yakitaka Kanali Ghadaffi aachine ngazi.

Mtoto wake, Seif, alionya kupitia kituo cha televisheni cha taifa kwamba kuna hatari nchi ikatumbukia kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe iwapo maandamano yataendelea. Mtangazaji alikuwa akisema “madimbwi ya damu yanainyemelea Libya na kuigeuza Somalia iwapo amani haitarejeshwa.”

Utawala wa Ghadhaffi umekabiliana kwa nguvu kubwa na waandamanaji katika staili isiyopata kushuhudiwa tangu maandamano ya kupinga tawala za nchi mbalimbali Uarabuni yalipoanza na kufanikiwa kusambaratisha serikali ya Misri na Tunisia. Karibu watu 300 walisharipotiwa kuuawa katika maandamano ya Libya, kulingana na ripoti za madaktari, mashirika ya watetezi wa haki za binadamu na wananchi wanaoishi uhamishoni.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, akizuru nchi jirani ya Misri aliitaka serikali ya Libya kukomesha mauaji ya waandamanaji aliyosema “yanatisha.”

"Tunachoweza kukiona Libya kinatisha na hakikubaliki kwani utawala unatumia mbinu katili za kunyamazisha waandamanaji wanaotaka kuona nchi yao ambayo ni moja ya zinazotawaliwa kwa mabavu na bila ya kutoa uahuru kwa raia inaingia katika mageuzi makubwa.

Mgawanyiko ni hatari kubwa kwa Libya, nchi yenye tofauti nyingi za kimakabila na upinzani kati ya Tripoli na Benghazi. Kanali Ghadaffi amekuwa akiongoza kwa mfumo wa kudhibiti madaraka alioupa jina la Jamahiriya au utawala wa watu.

Mapema, Balozi wa Linya katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu mjini Cairo, Abdel-Moneim al-Houni, ambaye alijiuzulu Jumamosi, alitaka Ghadaffi ashitakiwe pamoja na wasaidizi wake, vikosi vya ulinzi na usalama wanaoshiriki mauaji ya raia.”

"Utawala wa Ghadhaffi sasa ni historia kwa sababu alisaliti taifa lake na watu wake," alisema al-Houni.

Mfululizo wa maandamano nchini Libya, nchi mwanachama wa shirika la wazalishaji wa mafuta (OPEC) na ambayo ni msafirishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Ulaya, umeleta hofu ya kushuka kwa uzalishaji wa mafuta na hivyo kupandisha bei yake katika soko la dunia kutoka dola 1.67 hadi dola 88 kwa pipa.

Wakuu wa kampuni mbili za mafuta, Statoil na BP, walisema wanafikiria kuondosha baadhi ya wafanyakazi wao nchini Libya. Ureno ilituma ndege maalum kwa ajili ya kusafirisha raia zake pamoja na wa mataifa mengine ya Ulaya waliopo Libya. Serikali ya Uturuki ilituma boti mbili kwa ajili ya kuchukua wafanyakazi wa kamapuni za ujenzi waliokwama kutokana na hali ya tafrani. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu walikuwa wanajadiliana kuhusu namna watakavyowasaidia raia zao kuondoka. Makundi ya raia walishambulia raia wa Korea Kusini, Uturuki na Serbia.

Huduma za Intaneti kwa sehemu kubwa zilifungwa, na kuzuia mawasiliano ya simu za kimataifa na hata simu za ndani. Waandishi wa habari hawawezi kufanya kazi yao, lakini walioshuhudia walisema waandamanaji wanahimili vishindo. Wengi wa raia walitoa taarifa kwa masharti wasitajwe kwa kuhofia kuja kukandamizwa.

Italia, iliyoitawala Libya, ina biashara kubwa nchini Libya. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Franco Frattini anasema, "Unaweza kufikiria kuwa na himaya ya Kiarabu karibu na Ulaya? Ni hatari kubwa," anasema. Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Amr Moussa, amesema waandamanaji wana madai ya haki na “wapo katika kipindi cha hatima.”

0
No votes yet